NA ZAINAB IDDY, DAR ES SALAAM
IKIWA ni siku chache tangu uongozi wa Simba kuweka wazi msimamo wao wa kutocheza mechi baina yao na watani zao wa jadi, Yanga, iwapo itachezeshwa na waamuzi wa ndani, uongozi wa Yanga pia umesema upo tayari kwa jambo hilo.
Simba kupitia Ofisa Habari wao, Haji Manara, hivi karibuni alidai hawako tayari kuona wanaendelea kuonewa na waamuzi anaodai kuwabeba Yanga pindi wanapocheza nao.
Akizungumza na MTANZANIA, katika makao makuu ya klabu hiyo, yaliyopo Mtaa wa Jangwani, Kariakoo, jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Clement Sanga, alisema ili kumaliza tuhuma zinazotolewa dhidi yao, wapo tayari kwa lolote, ili mradi sheria za soka Tanzania zinafuatwa.
“Kama Shirikisho la Soka Tanzania litakubali suala hilo lililotolewa na Simba, sisi tupo tayari, hatuna shaka kwa kuwa tunafahamu hakuna mwamuzi anayetubeba.
“Waamuzi wanafanya kazi yao uwanjani kwa kutafsiri sheria 17 za soka, suala la kukosea ni la kawaida kwa kuwa hakuna aliyekamilika na kila binadamu ana mapungufu yake, sasa wao kama wanachukulia hiyo hali Yanga inabebwa basi walete tu waamuzi wao, sisi tutaingia uwanjani kutimiza jukumu letu, kikubwa TFF wakubaliane nalo,” alisema.
Sanga alieleza kuwa, mpira ni mchezo wa wazi, kama timu haijajiandaa vema ni wazi itashindwa kufanya vizuri uwanjani.