23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga, Simba kunogesha kasi ya ubingwa leo

YangaSimbaJUDITH PETER NA THERESIA GASPER, DAR

VIGOGO wa soka nchini, Simba na Yanga, leo watashuka dimbani katika viwanja tofauti kusaka pointi muhimu ili kulinda heshima na kuongeza kasi ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Mabingwa watetezi na vinara wanaoongoza katika msimamo wa ligi hiyo, Yanga, ambao walijeruhiwa kwa kupokea kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union katika mchezo uliopita, watakuwa ugenini wakichuana vikali na maafande wa Tanzania Prisons katika Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

Mahasimu wao, Simba, ambao wameanza kushika kasi katika Ligi baada ya kupata ushindi wa mechi tatu mfululizo, watawakaribisha Mgambo Shooting katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Yanga, ambao wanashika usukani wa ligi hiyo kwa kufikisha pointi 39 baada ya kushuka dimbani mara 16, wanauchukulia mchezo wa leo kama fainali kwa upande wao, huku wakiwa wamepania kucheza kwa umakini na utulivu wa hali ya juu ili kuendeleza kasi ya ushindi waliyoanza nayo.

Kocha mkuu wa timu hiyo Mholanzi, Hans van der Pluijm, aliliambia MTANZANIA jana kuwa mchezo wa leo unahitaji nguvu, umakini na maarifa zaidi ili kujihakikishia ushindi na kuzikabili changamoto zitakazojitokeza, zikiwemo za uwanja.

Alisema pamoja na safu yake ya ulinzi kupata pengo kwa kuwakosa wachezaji nyota, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani na Haji Mwinyi, amejiwekea asilimia kubwa ya ushindi kutokana na maandalizi waliyofanya.

Hata hivyo, Prisons, wanaoshika nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi, wamepania kulipiza kisasi kwa wapinzani wao, Yanga, kutokana na kipigo walichopata katika mchezo wa mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo.

Kama Yanga wakifanikiwa kupata ushindi, watafikisha pointi 42, lakini wakifungwa watabaki na pointi 39 kileleni ambazo zinaweza kufikiwa na Simba kama wataibuka na ushindi.

Naye kocha msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, alisema haihofii timu yoyote Ligi Kuu, lakini anahofia timu hiyo kufanya vibaya huku akieleza kuwa anachoangalia zaidi katika pambano la leo ni ushindi wa pointi tatu na si wingi wa mabao.

“Jambo linalozidi kunipa matumaini ni namna viwango vya wachezaji wangu vinavyozidi kuongezeka kila siku, baada ya kurekebisha mapungufu waliyokuwa nayo kabla sijaanza kazi kuwafundisha,” alisema Mayanja.

Mayanja alisema tayari ametengeneza kikosi cha kwanza, watahakikisha wanazidisha ushindani ili kutimiza malengo ya kuifanikisha timu yao kuchukua ubingwa msimu huu.

Mayanja aliongeza kuwa mpaka sasa ameshakitengeneza kikosi cha kwanza, ambacho kitaweza kuongeza ushindani na kufikia malengo waliyojiwekea ya kutwaa ubingwa.

Wachezaji wa Simba wanaopewa nafasi zaidi katika kikosi cha kwanza ni kipa Vincent Agban, Hassan Ramadhan ‘Kessy’, Abdi Banda, Hassan Isihaka, Jjuuko Murshid, Justice Majabvi, Mwinyi Kazimoto, Jonas Mkude, Hamis Kiiza, Ibrahim Ajib na Haji Ugando.

Katika mechi nyingine za ligi hiyo, Kagera Sugar watakuwa wenyeji wa Majimaji FC katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora, wakati maafande wa JKT Ruvu wakiwakaribisha Mbeya City katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.

Pia katika Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, African Sports watakuwa wenyeji wa Mwadui FC kutoka Shinyanga, huku Mtibwa Sugar wakiialika Toto African kwa mara ya kwanza katika Uwanja wa Manungu, Morogoro tangu ipande.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles