24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga SC yakamilika mpango wa kutwaa sportpesa

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

KIKOSI cha Yanga leo kinashuka dimbani kuumana na Kariobangi Shark ya Kenya, katika mchezo wa ufunguzi wa michuano ya SportPesa, utakaochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Pambano kati ya timu hizo linatarajia kuanza saa 10 jioni, lakini litatangulia na lile la mapema kati ya Singida United na Bandari ya Mombasa litakalopigwa kuanzia saa 8 mchana.

Yanga itakutana na Kariobangi ikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mchezo wake uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara ilipochapwa bao 1-0 na Stand United, Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Kipigo hicho kilikuwa cha kwanza kwa Yanga msimu huu, baada ya kucheza michezo 19 na kushinda 17 na kutoka sare miwili.

Vijana hao wa Jangwani waliondoshwa hatua ya awali katika michuano iliyopita ya Sportpesa ilipokubali kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa Kakamega Home Boys ya nchini Kenya.

Yanga itashuka dimbani ikiwa imeimarika zaidi, baada ya baadhi ya wachezaji wake waliokuwa majeruhi, kipa Ramadhani Kabwili, Papy Tshishimbi, Thabani Kamusoko kupona majeraha yaliyokuwa yanawasumbua.

Kwa sasa kikosi cha Yanga ndicho kinachoongoza katika msimamo wa Ligi Kuu kikiwa na pointi 53, ni wazi hii itaifanya timu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1935, kujiamini kiasi cha kutosha itakapowavaa Wakenya hao.

Akizungumzia maandalizi ya kikosi chake, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera, alisema mipango yao ni kufika fainali na kutwaa taji hilo.

“Hii itakuwa ni mara yangu ya kwanza kuiongoza Yanga katika michuano hii ya Sportpesa, nimekiandaa kikosi changu kiushindani zaidi ili tuweze kutwaa ubingwa,” alisema.

Kwa upande wa kocha msaidizi wa Kariobangi, Collins Omondi, alisema hawakuja Tanzania kushiriki bali kushindana na kulipeleka kombe la michuano hiyo Kenya.

“Nafahamu timu ya Yanga ni kubwa na ina wachezaji wazuri, ikiwa ni pamoja na mashabiki wengi, hata hivyo wachezaji 11 kila upande ndio watashindana na atakayeonyesha uwezo mzuri ndio atapata matokeo,” alisema.

Bingwa mtetezi wa michuano ya Sportpesa ni timu ya Gor Mahia ya  Kenya iliyotwaa mwaka jana ilipofanyika Nakuru nchini humo.

Timu bingwa wa michuano hiyo hupata fursa ya kuivaa timu ya Everton inayoshiriki Ligi Kuu ya nchini England.

Timu nyingine zinazoshiriki michuano hiyo ni Simba, Mbao za Tanzania, AFC Leopard na Gor Mahia za nchini Kenya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles