26 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

YANGA REKODI, SIMBA THAMANI ACHA TUONE

Na ABDUL MKEYENGE

UBISHI unaoweza kukutoa machozi, jasho na damu kuhusu pambano la watani wa jadi nchini, Simba na Yanga, unatarajiwa kumalizika leo jioni kwa wababe hao kukutana Uwanja wa Uhuru, jijini hapa.

Ubishi wa timu gani imara umekuwa mkubwa nchi nzima na kila shabiki anavutia upande wake kwa kuisifu iko vizuri tayari kwa mchezo huo unaosubiriwa kuisimamisha nchi kwa dakika 90, zitakazosimamiwa vyema na mwamuzi bora wa msimu uliopita, Herry Sasii.

Sassi aliyechezesha pambano la ufunguzi wa Ligi Kuu Bara msimu huu lililokutanisha wababe hao na Simba kupata ushindi wa penalti 5-4, ndiye aliyekabidhiwa rungu la kuamua nani mkali kati ya vigogo hao wa soka la Tanzania.
Mchezo huo unaotarajiwa kuwa na presha nje na ndani ya uwanja, matokeo yake huenda yakatoa timu kinara itakayoongoza ligi kutokana na timu hizo zinaenda kukutana zikiwa zimefungana pointi, lakini Simba wakiwa kileleni kwa kuwa na wastani mzuri wa mabao ya kufunga. Zina pointi 15 kila moja.

Yanga wataingia uwanjani wakitambia rekodi yao nzuri ya kuifunga Simba mara 32, Simba ikishinda michezo 25 katika michezo 91 waliyokutana katika wastani.
Rekodi hii inawafanya Yanga waingie uwanjani wakiwa na heshima hiyo ya kuwafunga wapinzani wao mara nyingi katika michezo waliyokutana.

Mabingwa hao watetezi wana jumla ya mabao 99, wakichukuwa ubingwa mara 27. Hizi ni rekodi zinazowafanya waingie uwanjani kifua kikiwa mbele.

Nyota wao Ibrahim Ajib, Obrey Chirwa ni watu wa kuchungwa na walinzi wa Simba kutokana na nyota hao kuwa katika kilele cha ubora wao hivi sasa.

Katika mabao 10 waliyofunga Yanga mpaka sasa kwenye michezo saba, kwa pamoja washambuliaji hao wameshirikiana kufunga mabao saba.

Ajib amefunga mabao matano, Chirwa amefunga mabao mawili. Muunganiko wao umeonekana kuwa na maelewano mazuri kwenye safu ya ushambuliaji pamoja na kiungo Pius Buswita.

Yanga wana hatihati ya kuwatumia nyota wao muhimu kwa miaka ya hivi karibuni Donald Ngoma, Thaban Kamusoko na Ammis Tambwe ambao wana majeraha.

Wachezaji hao wenye majeraha tofauti wamekuwa roho ndani ya kikosi cha Yanga na majeraha yao yamepunguza kikosi cha makali ya Yanga msimu huu, licha ya Ajib, Buswita na Chirwa kuibeba timu.

Lakini zimetoka taarifa kuwa majeruhi hao wamerudi na leo jioni watakuwa sehemu ya kikosi kitakachoshuka uwanjani kupambana na Simba.

Kama nyota hao watakuwa sehemu ya kikosi, itakuwa faraja kwa Wanayanga ambao wataamini kikosi chao kimekamilika na kiko tayari kuifunga timu yoyote ile.

Yanga waliowakosa wachezaji wao Juma Abdul, Kelvin Yondani na Raphael Alpha kwenye mchezo wao uliopita dhidi ya Stand United kutokana na nyota hao kuwa na kadi mbili za njano kila mmoja, leo wachezaji hao wanatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza.

Benchi la ufundi liliamua kutokuwachezesha nyota hao kwa kuhofu mmoja wao akipata kadi moja ya njano ataukosa mchezo wa Simba kwa mujibu wa kanuni ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).

Hivyo katika mcheo huo wa Yanga dhidi ya Stand United, iliwatumia wachezaji wengine Pato Ngonyani, Hassan Ramadhan na nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ili kuziba mapengo ya nyota hao ambao waliwekwa nje kwa kazi maalumu.

Licha ya hivyo hofu kubwa kwa mashabiki wa Yanga ni jina la mshambuliaji wa Simba, Emmanuel Okwi aliyeko kwenye kiwango bora wakati huu.

Okwi ambaye ndiye kinara wa ufungaji mabao wa Ligi Kuu Bara akifunga mabao nane mpaka sasa, ana rekodi nzuri ya kukutana na Yanga na kufanya mambo makubwa.

Uwepo wake katika mchezo huo ni moja ya sehemu inayowafanya Yanga wawe makini na nyota huyo, mwanzo wa mchezo mpaka mwisho wa mchezo.

Hata Simba wenyewe licha ya kuwa na kikosi chenye thamani inayokadiriwa kufikia bil. 1.3, lakini wana matarajio makubwa na Okwi aliyejiunga nao akitokea Sports Club Villa ya kwao Uganda katika pambano hilo.

Mtu mwingine wa kuchungwa na walinzi wa Yanga ni kiungo mshambuliaji, Shiza Kichuya. Nyota huyo aliyesajiliwa na Simba akitokea Mtibwa Sugar amekuwa na bahati ya kuwatungua Yanga mara kwa mara.

Msimu uliopita Kichuya alifunga mara zote mbili walizokutana na Yanga. Uwepo wake kikosini pamoja na Okwi na John Bocco kwenye safu ya ushambuliaji, Simba ni hatari kwa walinzi wa Yanga.

Uimara mwingine wa Simba uko kwenye safu ya kiungo ambako kuna James Kotei, Jonas Mkude, Mzamir Yassin, Said Ndemla na Haruna Niyonzima.

Viungo hao wote wako tayari kwa mchezo, ni jukumu la kocha wa Simba, Joseph Omog na msaidizi wake Djuma Masoud Irambona, kuchagua watu wa kuwalisha mipira wakina Okwi.

Majeraha ya mlinzi wa kati, Salum Mbonde moja kwa moja yanamrudisha kikosi cha kwanza mlinzi Juuko Mursheed ambaye alikuwa benchi muda mrefu wa michezo hiyo saba iliyochezwa mpaka sasa.

Ulinzi wa kati Simba unaweza kuundwa na Mursheed na nahodha wa kikosi Method Mwanjale, huku Mohamed Hussein ‘Zimbwe JR’ na mkongwe Erasto Nyoni wakitarajiwa kuwa walinzi wa pembeni na langoni akisimama Aishi Manula.
Mursheed ambaye pia ni mlinzi tegemezi wa timu ya taifa Uganda (The Craenes), inatajwa amepewa kazi maalumu ya kumlinda Ajib asilete madhara langoni mwa Simba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles