25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga kisasi, Simba ubabe

NA ABDUCADO EMMANUEL, DAR ES SALAAM

HOMA ya pambano la watani wa jadi imezidi kupanda kwa timu zote kuingia mafichoni, lakini kitakachojiri kwenye mchezo huo ni ama Yanga kufuta uteja au Simba kuendeleza ubabe dhidi ya Wanajangwani hao katika Uwanja wa Taifa Jumamosi hii.

Katika kujiandaa na mechi hiyo, timu zote zimekimbilia visiwani Zanzibar, Yanga ikiwa Pemba tokea Jumapili iliyopita na Simba ilirejea juzi Unguja kwenye kambi ya awali kabla ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL).

Tofauti na msimu uliopita, msimu huu timu zote mbili zitaingia dimbani zikiwa na kasi ya ushindi kwenye mechi zote tatu walizocheza, hivyo kila timu itakuwa na morali nzuri ya kumtambia mwenzake.

Msimu uliopita Simba ilipata sare mechi zote tatu za awali kabla ya kuivaa Yanga, huku hasimu wake akishinda mbili na kufungwa moja na mechi baina yao ikaisha kwa suluhu.

Mzunguko wa pili kibao kikaigeukia Yanga, walishindwa kufurukuta kwa kufungwa bao 1-0 lililowekwa kimiani na mshambuliaji kutoka Uganda, Emmanuel Okwi, aliyeuzwa Ulaya kwenda timu ya Sonderjyske ya Denmark.

Ukiwa ni mchezo wa 80 wa Ligi Kuu kwa watani wa jadi tokea ligi hiyo ianze, Yanga mpaka sasa ina ukame wa mechi nne wa kushindwa kuifunga Simba, sawa na dakika 360.

Mara ya mwisho kuwafunga wekundu hao ilikuwa ni Mei 18, mwaka juzi, walipoichapa mabao 2-0 na kutwaa ubingwa wa ligi kwa mara ya 24, wafungaji wakiwa Didier Kavumbagu na Hamis Kiiza, ambaye hivi sasa yupo Simba.

Kinachowauma zaidi Yanga kuelekea kila mchezo dhidi ya Simba ni ile kumbukumbu mbaya waliyokuwa nayo ya kukubali kichapo cha mbwa mwizi cha mabao 5-0, walichopewa Mei 7, 2012 na Simba kutwaa ubingwa wa ligi kwa mara ya mwisho, kwani hadi sasa wanahaha kulisaka kombe bila mafanikio.

Wakati pambano hilo likikaribia, tumeona namna wachezaji wa kigeni walivyong’ara kwa timu zote mbili katika kupachika mabao na huenda ikaamuliwa na nyota hao.

Kiiza, aliyekatwa Yanga msimu uliopita na Kocha Marcio Maximo, ameibukia Simba msimu huu na ndiye kinara wa ufungaji mabao Ligi Kuu, akiwa na mabao matano, ni wazi atakuwa na uchu wa kuwazodoa mabosi wake wa zamani.

Kama ilivyo kwa Kiiza, nyota wa Yanga, Amissi Tambwe, ambaye alikatwa na Simba msimu uliopita, akiwa na mabao matatu mpaka sasa sawa na mshambuliaji mwenzake Donald Ngoma, naye atataka kudhihirisha ubora wake kwa kuiua Simba.

Lakini historia inawabana wachezaji wazawa kwa misimu minne iliyopita kuanzia 2011-12, kwani katika mabao 19 yaliyofungwa kwenye mechi nane zilizopita, wageni wamefunga 12 na wazawa saba.

Mechi yao ya mwisho kuisha kwa wazawa kufunga kwenye ligi ilikuwa ni sare ya 1-1 kwenye mzunguko wa pili 2013/14, Haruna Chanongo akifunga kwa Simba na Simon Msuva akaisawazishia Yanga.

Nyota wapya wa kigeni wa Yanga wanaotarajia kucheza mchezo huo kwa mara ya kwanza ni Ngoma, Thabani Kamusoko na Vincent Bossou, huku wa Simba wakiwa ni Justice Madjavi, Emery Nimubona, Vincent Angban kama watachezeshwa.

Kocha wa Yanga, Hans van Pluijm, ataingia kwenye mchezo wake wa tatu wa ligi dhidi ya Simba, miwili ya awali aliambulia pointi moja, wa kwanza akitoa sare na mwingine akipoteza msimu uliopita, Dylan Kerr wa Simba yeye utakuwa ni mchezo wake wa kwanza wa watani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles