Na WINFRIDA MTOI-DAR ES SALAAMÂ Â Â Â Â Â |Â Â Â Â Â
WAWAKILISHI pekee kwenye michuano ya kimataifa, timu ya Yanga, leo inatupa karata yake nyingine katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kumenyana na Gor Mahia ya Kenya katika mchezo wa hatua ya makundi ya Shirikisho barani Afrika.
Timu hizo zinakutana katika mchezo wa marudiano baada ya ule wa awali uliofanyika nchini Kenya, Julai 18, mwaka huu na Yanga kufungwa mabao 4-0.
Mchezo huo utakuwa wa nne kwa Yanga  katika hatua hiyo ya makundi, awali ilicheza na USM Alger, Mei 7 na kufungwa mabao 4-0, nchini Algeria, mchezo wa pili Mei 16, mwaka huu, ilitoka suluhu na Rayon Sports ya Rwanda, katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika michuano hiyo, Yanga wapo kundi D linaloongozwa na USM Alger yenye pointi saba, wakifuatiwa na Gor Mahia walio na pointi tano, Rayon Sports wakiwa na pointi mbili na Yanga ikiwa na pointi moja.
Kutokana msimamo huo, pamoja na matokeo ya Yanga ya michezo iliyopita, timu hiyo itakuwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha kinarudisha imani kwa mashabiki wake kwa kuibuka na ushindi dhidi ya Gor Mahia.
Ikumbukwe katika michezo iliyopita, Yanga imecheza ikiwa haina kikosi cha kueleweka kwa sababu wachezaji wengi walikuwa wamemaliza mikataba na baadhi yao walikuwa hawaendi mazoezini.
Uongozi wa Yanga ulishindwa kuwaongezea mikataba wachezaji wake mapema kwa sababu ya hali ya ukata na mvutano uliokuwepo kwenye klabu hiyo.
Hata hivyo, hali ya utulivu imerejea klabuni hapo na wamefanikiwa kuwaongezea mikataba wachezaji wake muhimu pamoja na kusajili wapya kuimarisha kikosi hicho.
Wachezaji walioongezewa mikataba ni Kelvin Yondani, Vincent Andrew ‘Dante’, Juma Abdul, Said Juma Makapu na Benno Kakolanya.
Pia Yanga imewasajili wazawa, Mrisho Ngassa, Deus Kaseke, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Mohammed Issa ‘Mo Banka’ Klaus Kindoki Nkizi na Heritier Makambo kutoka DR Congo.
Kurejea kwa Kelvin Yondani ni faraja kwa wapenzi wa Yanga, kwani  pengo lake lilionekana kwenye mchezo uliopita  na Gor Mahia.
Hivyo kuna uwezekano mkubwa wa kikosi cha Yanga kuwa na mabadiliko makubwa katika mchezo wa leo, hali inayoweza kuleta matokeo chanya tofauti na mechi zilizopita.
Tofauti na Yondani, wachezaji wanaotarajiwa kuongezeka kwenye kikosi hicho ni Kaseke na Matheo Athony ambao awali majina yao yalikuwa hayajatumwa kwenda Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Kingine kinachotoa matumaini kwa Yanga ni kocha mkuu Mwinyi Zahera, ambaye alikuwa anakaa jukwaani kwa kukosa vibali, leo atakuwepo kwenye benchi baada ya suala hilo kukamilika.
Kupatikana kwa kibali cha kocha huyo, kulithibishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa klabu hiyo, Hussein Nyika, juzi wakati wa kutangaza majina ya kikosi cha msimu ujao.
Kwa upande wake, kocha Zahera ameweka bayana kuwa kuna mabadiliko katika mchezo huo na mashabiki wa Yanga watarajie matokeo mazuri kwa kuwa alifanyia marekebisho makosa aliyoyaona kwenye mchezo uliopita.
Alisema katika mchezo uliopita, tatizo lilikuwa safu ya ushambuliaji, washambuliaji walishindwa kufunga mabao licha ya kupata nafasi.
Alisema kingine alichokifanyia kazi ni jinsi ya kutulia na mpira pamoja na kuimarisha safu ya ulinzi kwa kuwa wachezaji walikuwa wanashindwa kukaa na mpira wanapoupata.
Gor Mahia itawavaa Yanga ikiwa na morali wa kutoka kushinda katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Kenya kwa kuifunga wapinzani wao AFC Leopads mabao 2-1.