Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
KIKOSI cha Yanga kinatarajia kurejea kambini jioni ya leo kuendelea kujifua, licha ya baadhi ya nyota wake wakijiunga na timu zao za Taifa kwa michezo ya kufuzu Kombe la Dunia.
Wachezaji wa Kimataifa wa Yanga walioitwa katika timu zao ni kipa Djigui Diarra (Mali), Khalid Aucho(Uganda) na Yacouba Songne (Burkina Faso).
Upande wa wazawa waliojiunga na kikosi cha timu ya Taifa Tanzania ambayo inatarajia kucheza na DR Congo na Madagascar, ni Ramadhan Kabwili, Shomari Kibwana, Bakari Mwamnyeto, Zawadi Mauya, Feisal Salum ‘’Fei Toto’ na Dickson Job.
Kocha Msaidizi wa Yanga, Cedrick Kaze, amesema siku 15 za mampunziko ya kupisha timu za taifa, watazitumia kuimarisha zaidi kikosi hicho.
“Tumecheza mechi tano, ushindi mara tano, tutakuwa na mapumziko ya siku 15 za kupisha timu za Taifa, tunakwenda kuzitumia kujiimarisha, tunajua tutafanya vizuri zaidi, Mechi inayofuata tunacheza na Namungu mkoani Lindi,” amesema Kaze.