HUSSEIN OMAR-MBEYA
YANGA imezidi kuchochea kasi, baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Tanzania Prisons, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.
Mabao ya Yanga katika mchezo huo yalifungwa na Ibrahim Ajib dakika ya 76 na Amissi Tambwe, dakika za 85 na 90, wakati lile la Prisons liliwekwa wavuni na Jeremiah Juma, dakika ya 45.
Ushindi huo uliifanya Yanga kufikisha pointi 38 na kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu, baada ya kushuka dimbani mara 14, ikishinda michezo 12 na kutoka sare miwili.
Dakika ya tatu, kiki ya Ajib, aliyepokea pasi makini ya Ngassa ilitoka nje ya lango la Prisons.
Dakika ya tisa, Makambo akiwa katika nafasi nzuri baada ya kupokea pande la Ngassa, alipiga kiki dhaifu iliyodakwa kiurahisi na kipa wa Prisons, Aron Kalambo.
Timu zote ziliendelea kufanya mashambulizi kwa zamu, ingawa hali ya Uwanja wa Sokoine iliyoathiriwa na mvua kubwa iliyonyesha jijini Mbeya jana, ilionekana kikwazo kwa wachezaji katika kumiliki mpira sawa sawa.
Dakika ya 45, Jumanne Fadhil, aliiandikia Prisons bao la kuongoza kwa mkwaju wa penalti, iliyotokana na kitendo cha beki wa Yanga, Vincent Andrew ‘Dante’, kumwangusha ndani ya eneo la hatari mshambuliaji, Kelvin Friday.
Kabla pambano hilo kusimama kupisha mapumziko, mwamuzi wa mchezo huo, Meshack Sudi, aliwalima kadi nyekundu, Mrisho Ngassa wa Yanga na Laurian Mpalile wa Prisons, baada ya wachezaji hao kupigana.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kwa wenyeji kutoka kifua mbele wakiongoza kwa bao 1-0, kipindi cha pili, Yanga ilionekana kuongeza kasi ya mashambulizi kwa lengo la kugomboa bao na pengine kuongeza.
Dakika ya 52, Jumanne Elfadhil, alilimwa kadi ya njano, baada ya kumfanyia madhambi, Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Dakika ya 70, Kalambo alifanya kazi nzuri kuokoa mpira wa kichwa uliopigwa na Anthony Matheo, aliyeunganisha kona iliyochongwa na Juma Abdul.
Dakika 76, Ajib aliifungia Yanga bao la kusawazisha kwa mkwaju wa penalti, baada ya beki wa Prisons kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari.
Bao hilo liliiongezea nguvu Yanga ambayo ilizidisha mashambulizi kwenye lango la Prisons.
Dakika ya 85, Tambwe, aliifungia Yanga bao la pili kwa mkwaju wa mguu wa kushoto, baada ya kutumia vizuri pande la Matheo Antony.
Mambo yalizidi kuwa magumu kwa wenyeji, kwani Tambwe alihamsha shangwe tena za mashabiki wa Yanga, baada ya kuifungia bao la tatu timu yake dakika ya tisini, baada ya kupokea pasi ndefu ya Kamusoko.
Hadi kipenga cha kuashiria kumalizika kwa pambano hilo kinasikika, Yanga ilichomoza na ushindi mnono wa mabao 3-1.
Katika mchezo mwingine wa ligi hiyo, Mwadui ilitoka sare ya bao 1-1 na KMC katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Mwadui Complex, Shinyanga huku Lipuli wakiwa Uwanja wa Samora mkoani Iringa ilipata ushindi wa 2-1 dhidi Biashara United.
Kikosi cha Prisons
Aron Kalambo, Salum Kimenya, Lauriani Mpalile, Nurdin Chona, James Mwasote, Jumanne Elfadhili, Benjamin Asukile, Cleophace Mkandala, Kelvin Friday, Hassan Kapalata, Jeremiah Juma/Hamis Maigo(dk83)
Kikosi Yanga
Ramadhan Kabwili, Juma Abdul/Amis Tambwe(dk 72), Mwinyi Haji, Andrew Vicent ‘Dante’, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Maka Edward/ Matheo Antony (45), Mrisho Ngassa, Feisal Salum/Thabit Kamusoko, Heritier Makambo, Ibrahim Ajib, Raphael Daudi