27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

TRA yasisitiza wananchi kuwa wazalendo

KOKU DAVID-DAR ES SALAAM



MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA), imekuwa ikisisitiza wananchi kuwa wazalendo wa kulipa kodi kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.
Kutokana na kodi, Serikali itaweza kutekeleza majukumu yake mbalimbali ya maendeleo kwa wananchi wake.

Kwa mujibu wa sheria za kodi kila mwenye mapato anatakiwa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi.

Sambamba na kuhamasisha wananchi kulipa kodi, mamlaka hiyo imekuwa ikitoa elimu kwa walipa kodi hasa wafanyabiashara, wamiliki wa makampuni pamoja na taasisi za Serikali ili kuwawezesha kuwa na uelewa wa kodi na kuwajengea utayari wa kulipa kwa hiari.

Pia imekuwa ikiweka mazingira mazuri ya kuhakikisha wafanyabiashara wanafanya biashara zao bila usumbufu ikiwa ni pamoja na kulipa kodi bila kusumbuliwa.

Aidha, imekuwa ikiandaa walipakodi wa baadaye ambao ni wanafunzi kutoka shule mbalimbali za sekondari ambao TRA inaamini kuwa watakuwa mabalozi wazuri wa kodi.

Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere, anasema kuwa ujenzi na maendeleo ya nchi yanatokana na kodi hivyo wananchi wanatakiwa kuwa na utamaduni wa kudai risiti za mashine za kielektroniki (EFD) ili kuchangia mapato yatakayotumika kuboresha miundombinu mbalimbali, ujenzi wa shule pamoja na shughuli mbalimbali za jamii.

Anasema matunda ya kodi zinazopatikana pia hutumika kuboresha huduma mbalimbali za jamii kama ujenzi wa hospitali, barabara, ununuzi wa vitabu kwa ajili ya maktaba, utoaji wa mikopo ya elimu ya juu, ujenzi wa madarasa, mabweni, nyumba za walimu na ununuzi wa vifaa vya maabara na kufundishia.

Anasema kutokana na hali hiyo, TRA inatoa wito kwa wananchi hasa wafanyabiashara kuwa wazalendo kulipa kodi ikiwa ni pamoja na wale ambao wameshapata elimu ya kodi kuwafundisha na wengine umuhimu wa kulipa kodi.

Kichere anasema kodi ni muhimu kutokana na kuwa ni chanzo kikuu cha mapato ya Serikali, hivyo mamlaka hiyo imeamua kusambaza elimu ya kodi kuanzia shule ili kuandaa walipakodi wazuri wa baadaye na mabalozi wa mafanikio katika ulipaji wa kodi kwa hiari.

Anasema utoaji wa elimu ya kodi kuanzia mashuleni kutasaidia kuwa na taifa la watu wazalendo watakaopenda kuchangia maendeleo ya nchi yao kupitia kodi watakazokuwa wakilipa.

Anasema mamlaka hiyo ambayo imejipanga kuhakikisha inakusanya mapato hadi kuvuka lengo la Serikali, imekuwa ikitumia mfumo wa kisasa wa uondoshaji mizigo bandarini pamoja na ukadiriaji wa kodi (TANCIS) ambao utamwezesha mlipakodi kujua kodi stahiki anayotakiwa kulipa pamoja na kujua mzigo wake ulipo.

Anasema sambamba na kutumia mifumo ya kisasa katika kusaidia kuongeza mapato ya Serikali, pia wamejipanga kuhakikisha wanatanua wigo wa walipakodi kwa kuongeza walipakodi wapya.

Anaongeza kuwa hivi sasa wapo katika maandalizi ya kuanzisha kampuni itakayotengeneza mashine za EFD ili kuwawezesha wafanyabiashara kuzipata kwa bei nafuu.

Anasema matumizi ya mashine za EFD yatasaidia kutunza kumbukumbu za mauzo ya wafanyabiashara, lakini pia kuwezesha mapato ya Serikali kwa mujibu wa sheria.

Anasema TRA inaendelea kuwasisitizia wananchi kuendelea kuwa wazalendo kwa nchi yao ili kuiwezesha Serikali kutimiza lengo lake la kuwa na Serikali ya viwanda itakayotoa ajira kwa wanachi wake pamoja na kukusanya kodi ya kutosha hadi kuvuka lengo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles