MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga juzi walikula bata ndefu kwa kujirusha usiku kucha wakisherehekea mjini Kigali, Rwanda baada ya kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya APR katika mchezo wa Klabu Bingwa Afrika uliopigwa Uwanja wa Amahoro.
Wachezaji wa Yanga wakiongozwa na mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Donald Ngoma, usiku wa juzi walikuwa wakijirusha katika klabu ya usiku ya Class iliyopo jirani na hoteli waliyofikia ya The Mirror yenye hadhi ya nyota tano.
Wakiwa ndani ya klabu hiyo, wachezaji wa Yanga walionekana kufurahia ushindi waliopata dhidi ya wenyeji wao APR huku wengine wakieleza kuwa wamepania kuifikisha mbali timu hiyo msimu huu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na kuweka rekodi wakiwa na kikosi cha Wanajangwani hao.
Akizungumza na MTANZANIA mjini Kigali, Ngoma alisema wamepania kufanya kweli wakiwa Yanga kwani wamejiwekea malengo ya kufika mbali pamoja na kutumia michuano ya Klabu Bingwa Afrika kujitangaza kimataifa.
“Tumepania kufanya vizuri mwaka huu, nia na malengo yetu ni kujitangaza zaidi ili kuonekana kwa nchi nyingne kupitia michuano hii kama walivyofanya wachezaji wengine waliotumia fursa ya michuano ya kimataifa kupata timu katika mataifa ya Ulaya,” alisema.
Ngoma alisema huu ni mwaka wa kihistoria kwa Yanga baada ya Wanajangwani hao kukosa mafanikio katika michuano ya Afrika kwa miaka mingi, hivyo wamejipanga kuhakikisha wanafanya kweli na kuifikisha mbali timu hiyo mwaka huu.