26.2 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

Wosia wa Aboud Jumbe kwa Watanzania

Marehemu Aboud Jumbe Mwinyi
Marehemu Aboud Jumbe Mwinyi

NA YUSSUF KAJENJE

JUMAMOSI ya Mei 18, 2002, majira ya alasiri nikiwa katika chumba cha habari mwandishi mmoja maarufu hapa nchini alipiga simu, akiuliza iwapo kama tulimaliza kukamilisha gazeti na kulipeleka kiwandani tayari kwa kuchapishwa.

Nilipomjibu kuwa gazeti bado halijaenda mtamboni, akasema kuwa hiyo ni bahati kwetu kama gazeti kwani tungekuwa na habari kubwa kuhusu Mzee Aboud Jumbe siku iliyofuata.

Mtoa taarifa huyo alisema kuwa Mzee Aboud Jumbe alikuwa mahututi na kwa jinsi alivyomuona kule uwanja wa ndege wa Mwalimu Nyerere ilionekana kana kwamba tayari alikuwa amekata kauli.

Nilimshukuru kwa ‘tip’ ile na nikaamua kuifanyia kazi ili kupata taarifa zaidi juu ya suala hilo. Nikaamua kupiga simu nyumbani kwa Mzee Jumbe kule Mji Mwema, Kigamboni.

Lahaula! Sauti iliyojibu simu upande wa pili ilikuwa sauti niliyoifahamu na kuzoea kuisikia. Aliyepokea simu hakuwa mwingine bali Mzee Jumbe mwenyewe! Sikumweleza sababu zilizofanya nipige simu nyumbani kwake, badala yake nikamwomba ya kukutana naye ili tufanye mahojiano juu ya masuala mbalimbali.

Akakubali, akanialika niende kuzungumza naye siku ya pili yake. Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano yetu ambayo yaliwahi kuchapishwa katika gazeti la Mtanzania Jumapili, Mei 26, 2002.

“Siku hizi sisikii vizuri na pia sioni sawasawa. Hivyo niwie radhi kwa mapungufu yatakayojitokeza wakati wa mazungumzo yetu,” alianza kusema Aboud Jumbe wakati akikaa vizuri katika moja ya masofa yaliyokuwa sebuleni baada ya kutoka mahali ambako bila shaka alikuwa amejipumzisha.

Katika umri wake wa zaidi ya miaka 80 wakati huo, Aboud Jumbe alionekana wazi kuwa umri ulikuwa umeanza kumtupa mkono.  Alikuwa amezeeka. Hata hivyo, mbali  na uzee huo bado alikuwa na uwezo mkubwa kufuatilia mambo yanayotokea duniani na alionekana kukumbuka mengi aliyokutana nayo za utoto wake.

“Tangu nilipotoka serikalini mwaka 1984, nimekuwa nikifanya shughuli mbalimbali za kujipatia riziki, na kutafuta mwisho mwema kwa Mwenyezi Mungu,” alisema Aboud Jumbe.

Alisema alikuwa akijishughulisha na kazi za uvuvi na ufugaji wa kuku, ng’ombe na mbuzi. Pia alifungua kiwanda cha kuzalisha barafu kwa ajili ya wavuvi.

Licha ya umri wake mkubwa, yeye mwenyewe ndiye aliyekuwa anasimamia miradi yote hiyo.

Akizungumzia juu ya maisha yake tangu utotoni, Aboud Jumbe ambaye alizaliwa Zanzibar Juni 14, 1920, alisema kwamba mambo mengi yalimtokea kwa namna tofauti na jinsi alivyotarajia.

“Utastaajabu kwamba katika maisha yangu yote sikuwahi kuwa na mpango. Na kama ulikuwapo, basi haukufanikiwa.

“Kwanza nikiwa na miaka 10 nilipelekwa kusoma madrasa, lakini nikatolewa kwa nguvu na askari waliokuwa wakipita kuwakamata watoto wenye umri mkubwa wa kwenda shule. Nilipenda sana kuendelea na madrasa, lakini haikuwezekana.

“Ingawa nilipenda madrasa, sikutoroka katika shule ya Mnazi Mmoja (sasa inaitwa Ben Bella) ambako nilikuwa nimepelekwa kusoma. Nilifanikiwa kumaliza darasa la nane katika shule hiyo,” alisema Aboud Jumbe.

Alisema kwamba siku moja asubuhi akiwa anafua nguo, alifahamishwa na mkuu wa shule hiyo ambaye alikuwa mzungu kwamba alikuwa amefaulu mtihani, hivyo alitakiwa kuendelea na masomo ya sekondari katika shule hiyo.

Alipofika kidato cha pili mwaka 1943, rafiki zake wengi wakawa wanaondoka kwenda nje kupigana katika Vita Kuu ya Dunia. “Nami sikutaka tena kuendelea na masomo, nikaamua kujiandikisha ili niende vitani.”

“Hata hivyo, siku nilipokwenda kujiandikisha nilimkuta Mkuu wa shule katika ofisi za kujiandikishia. Alinizuia kwa kuniambia kwamba vita ikiisha, sitanufaika na mshahara waliokuwa wakilipwa wanajeshi, hivyo ni vema nikaendelea na masomo kwani baadaye ningeweza kupata ajira yenye mshahara mzuri.”

Aboud Jumbe alikubali ule ushauri wa mwalimu wake kwa shingo upande, kwani mpango aliokuwa amepanga ulikuwa umevurugika. Alipohitimu masomo ya sekondari, alifanikiwa kupata nafasi ya kwenda Chuo Kikuu Makerere, Uganda.

“Nilitaka nikasomee uhandisi au udaktari, lakini yote hayo nilikataliwa isipokuwa ualimu,” alisema Aboud Jumbe, na kuongeza: “Kwa mara nyingine mpango wangu ukawa umevurugika.”

Alisema akiwa Makerere ndiko alikopata fursa ya kukutana kwa mara ya kwanza na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. “Wote tulikuwa tunasomea ualimu, na tulielewana sana.”

Aboud Jumbe alisema kwamba mara baada ya kuhitimu Makerere, alifundisha kwa miaka 15. “Mwaka 1958, kiongozi wa chama cha ASP, Sheikh Thabit Kombo, alinijia akaniomba nisaidie harakati za chini kwa chini za kupambana na utawala wa kisultani.”

“Nilishauriana na mke wangu, mama, pamoja na dada yangu kuhusu uamuzi wa kuacha kazi ya ualimu iliyokuwa ikinipa mshahara wa Sh 1,500. Walikubali, nami nikaingia katika harakati za chini kwa chini ambazo hazikuwa na mshahara mkubwa.”

Aboud Jumbe alisema kwamba mapinduzi yalipofanyika mwaka 1964, alipata wadhifa wa kuwa Katibu wa Mipango mpaka mwaka 1972 wakati alipochaguliwa kuwa Rais wa SMZ. “Kwa mara nyingine hilo halikuwa katika matarajio yangu.”

Akizungumzia juu ya maisha yake ya ndoa, Aboud Jumbe alisema kwamba alioa mke wa kwanza mwaka 1948, miaka mitatu tangu alipoanza kazi ya ualimu. Miaka minne baadaye, 1952, alijaliwa kupata mtoto wa kwanza. Mkewe huyo wa kwanza ambaye alifariki mwaka 2000, alizaa watoto wanane, wawili wa kike, na sita wa kiume.

Aboud Jumbe alisema kwamba baada ya mapinduzi ya mwaka 1964, alioa tena mke mwingine ambaye alizaa watoto watano wa kiume. “Baadaye tuliachana, kisha nikaoa mke mwingine wa kutoka Pemba ambaye ndiye ninayeishi naye sasa (wakati wa mahojiano), na amezaa watoto wawili, wa kike na wa kiume.”

Mbali na wake zake hao watatu, Aboud Jumbe alioa mwanamke mwingine ambaye kwa kauli yake ndiye aliyekuwa akisafiri naye mara kwa mara katika safari za kikazi. Alizaa naye watoto watatu. Kwa ujumla alioa wake wanne, na hadi mwaka 2002 alikuwa amejaaliwa kupata jumla ya watoto 18.

Akizungumzia jinsi alivyofanya Mji Mwema kuwa makazi yake, Aboud Jumbe alisema kwamba alianza kujenga huko akiwa bado kiongozi serikalini.

“Hapa palikuwa msitu mnene. Siku moja katika miaka ya katikati ya 1970, nikiwa katika ziara ya kikazi katika Mkoa wa Dar es Salaam, nilifika Mji Mwema. Ilikuwa ziara ya kiserikali ya kuwahamsisha wananchi wahamie katika vijiji vya ujamaa.

“Nilikuwa na kawaida ya kulala popote; usiku uliponikuta, na siku hiyo nilipangiwa kulala katika nyumba ya serikali iliyokuwa karibu na eneo hili la Mji Mwema.”

Aboud Jumbe alisema kwamba enzi hizo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alikuwa Joseph Rwegasira. “Siku hiyo niliyokuwa nimepangiwa kulala hapa, usiku walikuja wavuvi waliokuwa wameweka kambi zao za uvuvi hapa.

“Nilizungumza nao kwa muda mrefu, kiasi kwamba baadaye Rwegasira aliniuliza iwapo nilikuwa nafahamiana na wale watu. Nami nilimwambia Rwegasira kwamba wale wavuvi walikuwa ndugu zangu wa upande wa baba.”

Jumbe alisema kuanzia siku hiyo akawa ameipenda sehemu hiyo ya Mji Mwema, hivyo akafanya mpango wa kuanza kujenga nyumba yake binafsi.

Anasema kwamba baada ya kuanza ujenzi, wenyeji wengine waliokuwa wakiishi maeneo ya mbali, walianza kusogea karibu na mahali alipo.

Jumbe alisema kwa kuwa alipata eneo kubwa, aliamua kupanda miembe, minazi pamoja na mazao mengine. “Nilijenga bila kujua kuwa baadaye ningekuja kuishi katika nyumba hii.”

Akizungumzia juu ya kujiuzulu kwake mwaka 1984, Aboud Jumbe alisema kuwa kulitokana na baadhi ya viongozi aliokuwa nao serikalini Zanzibar kumfitini kuwa anataka kuiuza nchi.

Alisema viongozi hao wafitini (anamtaja Maalim Seif) walieneza uvumi kwamba kulikuwa na mpango wa kutaka kuipindua serikali ili kuua Muungano. “Hata hivyo, viongozi hao baadaye walipata matatizo, nao wakatoka serikalini kwa kufukuzwa.”

“Siku moja kabla ya sherehe za mapinduzi ambazo zilikuwa zimepangwa kufanyika Pemba, walikuja wajumbe wawili wa Baraza la Mapinduzi wakaniambia kuwa kule Pemba hali haikuwa nzuri, na kwamba kungetokea maasi.

“Nilimpa taarifa hizo Mwalimu Nyerere, naye akaja Zanzibar kama ilivyokuwa imepangwa bila kujali taarifa nilizokuwa nimempelekea.

Aboud Jumbe alisema kuwa katika kikao maalumu cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kilichofanyika Dodoma mwaka 1984 kujadili hali ya machafuko ya kisiasa Zanzibar, hakuna aliyejua kwamba angechukua uamuzi wa kujiuzulu. “Hata Mwalimu Nyerere hakujua.”

“Nilichukua uamuzi wa kujiuzulu kwa sababu masharti yangu matatu ya kufanya kazi popote pale yalikuwa yamevunjwa.”

Alisema kuwa sharti lake la kwanza kufanya kazi ni lazima isiwepo hali ya kutia shaka, na pawepo uwazi na ukweli.

“Sharti la pili ni kuwa na uwezo kimwili na kiakili, na si kuendeshwa na kufanywa kama sanamu.” Alitaja sharti la tatu ni kuwa “ni lazima wote tukubaliane kufanya kazi pamoja.”  Aboud Jumbe alisema kuwa masharti hayo yote yalivunjwa, na ndiyo maana aliamua kujiuzulu.

Alipojiuzulu alitaka kurudi kwao Zanzibar, lakini kwa maelezo yake Mwalimu Nyerere alimzuia. “Nyerere alinishauri nisirudi Zanzibar wakati huo kwa sababu hali haikuwa nzuri.  Alisema nisubiri mambo yatulie kwanza.”

Baada ya kujiuzulu, mbali na mambo mengine ambayo alikuwa akiyafanya ni pamoja na kuandika vitabu. “Nimekuwa nikijishughulisha na kazi ya uandishi wa vitabu. Mpaka sasa (wakati wa mahojiano) nimekwishaandika vitabu vinne; cha kwanza ni ‘Safarini’ ambacho maudhui yake ni kwamba binadamu wote katika maisha tuko safarini.”

Aboud Jumbe alisema aliamua kuandika kitabu hicho kwa lengo la kuikumbusha nafsi yake pamoja na binadamu wengine mambo ya kufanya ili kupata mwisho mwema kwa wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu.

Alitaja kitabu kingine alichotunga kuwa kinaitwa “Partnership”, neno la Kiingereza lenye maana ya “ubia” au “upamoja” wenye lengo la kufanya jambo kwa pamoja. Katika kitabu hicho, hakutaka kutumbukia katiak mambo ya siasa. “Maudhui yake yamelenga kueleza hali halisi ya mambo tulikotika, tulipo na jinsi hali itakavyokuwa huko tuendako.”

Jumbe alisema kuwa vitabu vingine alivyotunga vinahusu mambo ya dini ya Kiislamu. Navyo ni pamoja na kilie kiitwacho “Mjue Mtume Wako” ambacho kina matoleo 15. Mpaka wakati huo alikuwa amekwisha kuchapisha mfululizo wa matokeo matatu tu, hali ambayo ilikuwa imechangiwa na kupungua kwa uwezo wake wa kuona vizuri, hivyo kulazimika kuandika vitabu kwa kumsomea mtu mwingine ambaye alikuwa akinakiri yale anayotamka.

Aliwahi kuandika kitabu kingine kiitwacho “Tuko Wapi Dunia Hii?” “Hata hivyo bado sijakimaliza kwa sababu ya afya yangu kutokuwa nzuri,” alitamka Jumbe wakati wa mahojiano yetu.

Akizungumzia juu ya kuongezeka na kupanuka kwa vyombo vya habari, Aboud Jumbe alisema kuwa ni jambo zuri, lakini vingi vina mapungufu katika utendaji kazi wake.

“Redio nyingi zimeanzishwa, lakini kutwa nzima ni muziki tu. Mimi sisikilizi redio kwa sababu hiyo, na inapotokea, nikasikiliza basi ni kwa vipindi vya taarifa ya habari tu,” alisema Aboud Jumbe.

Mwisho wa mahojiano yetu, Aboud Jumbe alitoa ushauri ambao yeye binafsi aliuita kuwa wosia wake kwa Watanzania. Aliwataka wasibweteke na amani iliyopo nchini.

Alisema kwamba nchi nyingi duniani, zikiwamo zile tunazopakana nazo, zina mgogoro. “Karibu nusu ya idadi ya nchi tunazopakana nazo kuna machafuko. Mamia ya watu wanapoteza maisha yao.

“Nadhani kuna haja kwa serikali, vyama vya siasa na wananchi wenyewe, kwenda kwa undani na kuangalia sababu ambazo zimesababisha matatizo katika nchi hizo hadi kufikia hatua ya kupigana.

“Lazima wote tuangalie sababu zote; za msingi na hata zile zinazojitokeza kwa muda mfupi ambazo zimezifikisha nchi jirani zetu na nyingine duniani kuwa katika hali hiyo ya machafuko.

“Ni jukumu la kila mtu kuangalia kwa makini juu ya mwenendo wa nchi yetu na kuchukua hatua ambazo zinaweza kulinusuru taifa lisitumbukie katika machafuko tunayosikia katika nchi nyingine,” alisema Aboud Jumbe.

Alihitimisha mazungumzo yetu kwa kusema kuwa ni wakati wa kuchukua tahadhari. “Ukiona kwa mwenzako kunaungua, basi nawe ondoa makuti kwenye banda lako ili nako kusiungue.”

Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles