30.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 27, 2024

Contact us: [email protected]

World Vision yaokoa wananchi kufuata huduma za Afya kilometa 15

Na Derick Milton, Simiyu

Wakazi wa Kijiji Cha Ikungulipu Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, wameondokana na adha ya kutembea umbali wa zaidi ya kilometa 15 kufuata huduma za afya katika Zahanati ya Luguru baada ya ujenzi wa Zahanati ya kijiji hicho kukamilika.

Mradi huo umejengwa kwa ufadhili wa Shirika la World Vision Tanzania, kupitia mradi wake wa Maendeleo Ruguru wa miaka 15 ambapo ujenzi wa Zahanati hiyo umegharimu Sh milioni 110.5.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi zahanati hiyo iliyofanyika leo Alhamsi Februari 25, 2020 katika kijiji hicho, Kaimu Meneja wa Shirika hilo kanda ya Nzenga Gilselda Balyagati amesema kuwa ujenzi huo umefanyika kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji hicho.

Balyagati amesema kuwa wananchi wa kijiji hicho walichangia nguvu kazi ambapo ni mawe pamoja na mchanga, ambapo Shirika hilo likichangia gharama za ujenzi kwa kumlipa mkandarasi hadi ujenzi unakamilika na kufikia hatua ya zahanati kuanza kutumika.

“Ujenzi ulianza mwaka 2015 ambapo world vision Tanzania kupitia mradi wa maendeleo Luguru kwa kushirikiana na wananchi wa kijiji cha Ikungulipu tumeshirikiana kujenga mradi na umekamilika, wananchi walichangia mawe, mchanga,maji na kokoto,” amesema Balyagati.

Mbali na ujenzi huo Meneja huyo amesema kuwa World Vison imetoa vifaa mbalimbali vya tiba kwenye zahanati hiyo vyenye thamani ya Sh milioni 5.1 kwa ajili ya huduma kuanza kutolewa kwa wananchi.

Amesema kuwa World Vison iliamua kusaidia ujenzi wa zahanati hiyo ili wananchi wa kijiji hicho na kijiji jirani cha Giriku wapatao 14,634 waweze kupata huduma bora za Afya hasa katika kuwapunguzia umbali wa kufuata huduma kwenye Zahanati ya Luguru.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Luguru, Robert Jongera amelishukuru Shirika hilo kwa kusauidia ujenzi wa Zahanati katika kijiji hicho, ambapo ameeleza awali wananchi waliangaika sana na kutumia muda mrefu kufuata huduma zaidi ya kilometa 15.

“Kijiji hiki kina vitongoji 10 awali wananchi walitembea umbali mrefu kufuata huduma baadhi ya kina mama walijifungulia njiani, mvua ilipokuwa ikinyesha idadi kubwa ya wananchi walishindwa kufika kwenye huduma lakini sasa mambo hayo yamekwisha baada ya kukamilika kwa zahanati hii,” amesema Jongela.

Akipokea Zahanati hiyo kwa niaba ya Serikali Mkuu wa Wilaya hiyo, Benson Kilangi, aliishukuru World Vision kwa msaada huo, huku akiwataka wananchi kuhakikisha wanatunza jengo hilo pamoja na vifaa vilivyotolewa.

Aidha, Kilangi amewahakikishia wananchi kuwa Serikali kupitia halmashauri itakamilisha baadhi ya mahitaji kwenye zahanti hiyo ikiwemo huduma ya umeme, maji pamoja na Nyumba ya mganga mfawidhi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles