MWANDISHI WETU-MTWARA
WAKALA wa Vipimo Tanzania (WMA) imeendelea kufanya uhakiki na ukaguzi wa kushtukiza katika vituo vya kununulia korosho kwenye mikoa mitano inayolima zao hilo.
Mikoa hiyo ni pamoja na Mtwara, Lindi, Ruvuma, na Pwani ambapo jumla ya wilaya 20 katika mikoa yote zilifikiwa.
Ukaguzi wa kushtukiza ulifanyika kati ya Novemba na Desemba mwaka jana baada ya kukamilika uhakiki wa mizani zote zinazotumika kununulia korosho ambalo hufanyika kabla ya kufunguliwa kwa msimu.
Akizungumza mwishoni mwa wiki, Meneja wa WMA Mkoa wa Mtwara, David Makungu alisema jumla ya vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) 919 vilikaguliwa kwa mtindo wa kushtukiza.
Alisema katika ukaguzi huo mizani ya vyama vya msingi 1,296 na mizani 20 ya maghala makuu ilikaguliwa.
“Katika ukaguzi huo mizani 23 ilibainika kuwa na makosa mbalimbali ikiwa ni pamoja kutokupima kwa usahihi, mawe ya mizani kuongezewa uzito na baadhi ya mizani kutumiwa bila kuhakikiwa.
“Katika ukaguzi huo kuna mizani 23 ilibainika kuwa na makosa na wamiliki wa mizani hiyo walikubali makosa yao na kutozwa faini ambayo inaanzia Sh 100,000 hadi milioni 20 kwa kila kosa,”alisema meneja huyo.
Aidha Makungu aliongeza kuwa katika ukaguzi huo, watu wanne kati ya waliokamatwa walikana makosa yao hivyo kesi zao zipo mahakamani.
Endapo watuhumiwa hao watakutwa na hatia kwa kosa la kwanza watatozwa faini isiyopungua Sh 300,000 na isiyozidi millioni 50, kifungo cha miaka miwili au vyote kwa pamoja kwa mujibu wa sheria ya vipimo sura na. 340 na mapitio yake ya mwaka 2002.
Pia, endapo mtuhumiwa atakamatwa na kosa kwa mara ya pili na kuendelea na akipelekwa Mahakamani akakutwa na hatia adhabu ni faini isiyopungua Sh 500,000 na isiyozidi milioni 100 au kifungo kisichozidi miaka mitano (5) au vyote kwa pamoja.
Baadhi ya wakulima wa korosho katika wilaya ya Newala wameipongeza Serikali kwa kununua korosho zao pamoja na WMA kwa kusimamia usahihi wa mizani.