Na MWANDISHI WETU-ZANZIBAR
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, zimekutana kujadili suala la kufunga kamera maalumu za kudhibiti na kuzuia uhalifu.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alisema Serikali inatambua umuhimu wa ulinzi na usalama kwa raia wake na iko katika mpango wa kufunga kamera hizo katika miji yote mikuu nchini.
Alisema lengo la kufunga kamera hizo ni kuiwezesha serikali kupambana na matukio ya uhalifu ya utekaji, makosa ya barabarani, uporaji wa fedha katika taasisi za fedha.
“Tumekuja kuchukua uzoefu kwa wenzetu wa Zanzibar ambao tayari wameshafunga kamera hizi katika maeneo mbalimbali na nimeona jinsi zinavyofanya kazi za kubaini wahalifu.
“Teknokolojia haiepukiki katika kudhibiti, Serikali tumejipanga na hivi karibuni tutaanza kufunga kamera za CCTV katika miji mikuu na maeneo ya mikoa iliyoko mipakani kudhibiti wahalifu kutoka nje ya Tanzania,” alisema Masauni
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Radhiya Rashid Haroub alisema tayari washafunga kamera hizo ambazo zilizinduliwa Oktoba 3, mwaka huu.
Alisema uzinduzi wa kamera hizo ulifanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein.