24.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

Wizara yaipa maelekezo TFS, TAWA uanzishaji bustani za miti nchini

Na Clara Matimo, Mwanza

ILI kuendana na mahitaji, mwamko mkubwa wa wananchi kupanda miti nchini, Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa maelekezo kwa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na Mfuko wa Misitu (TAWA) kuharakisha uanzishwaji wa bustani huku wakitakiwa kuanzisha bustani nyingine ndogo kuanzia ngazi ya kata na tarafa kisha  kubaini, kutenga maeneo sahihi ya kupandwa miti pia kuainisha aina ya miti itakayofaa kulingana na eneo husika.

MWANAMKE NA MTI: Mkazi wa Kijiji cha Sagani Kata ya Sandawe, wlayani Magu mkoani Mwanza, akipanda mti katika kilele cha maadhimisho ya siku ya upandaji miti na misitu kitaifa yaliyofanyika wilayani humo. Picha na Clara Matimo.

Maelekezo hayo yametolewa leo Machi 21, 2022 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Marry Masanja,  katika kilele cha maadhimisho ya siku ya upandaji miti na misitu kitaifa yaliyofanyika uwanja wa Sabasaba wilayani Magu Mkoa wa Mwanza.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa wizara hiyo,Dk. Damas Ndumbaro,  mbele ya wananchi waliojitokeza kwenye maadhimisho hayo, Marry amesema wananchi wamekuwa na mwamko wa kupanda miti katika maeneo yao hivyo kuna umuhimu wa kuhakikisha miche bora inapatikana wakati wote kwa urahisi na kutoa elimu ya ugani kwa wananchi kuhusu upandaji miti.

“Ili kuwe na upatikanaji wa miti kwa wingi na kwa urahisi nawaelekeza TFS  kwa kushirikiana na Tawa hakikisheni bustani mnayotaka kuianzisha inanza mara moja, miche ya aina zote kulingana na mahitaji ya wananchi ipatikane ikiwemo ya mbao, matunda, kivuli, mapambo, kuboresha ardhi na malisho ya mifugo,” amesema Marry na kuongeza:

“Pia anzisheni bustani nyingine ndogondogo katika ngazi ya kata na tarafa ili wananchi waishio vijijini waweze kuipata kwa urahisi, shirikianeni na ofisi za wakurugenzi wa halmashauri kufanya upembuzi yakinifu kubaini na kutenga maeneo sahihi pa kuanzisha bustani hizo, maeneo ya kupandwa miti na kuainisha aina ya miti itakayofaa kupandwa katika eneo husika  ili kuwe na upandaji miti wenye tija.

“Ili tuwe na mipango halisia ya upandaji miti katika maeneo yetu ardhi na malisho ya mifugo ibainishwe  kwa kufanya hivyo tutakuwa na  makisio halisia ya mahitaji ya miche kwa msimu husika vingenevyo tutakuwa tukibahatisha tu, watendaji hususan wizara yetu toeni  elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa upandaji miti na uhifadhi ili wajue na watambue faida za rasilimali misitu,” amesema.

BALOZI: Balozi wa Mazingira chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Winfrida Shonde, akimwagia maji mti baada ya kuupanda katika kilele cha maadhimisho ya siku ya upandaji miti na misitu kitaifa yaliyofanyika Wilaya ya Magu mkoani Mwanza. Picha na Clara Matimo.

Naibu huyo amesema katika maadhimisho hayo jumla ya miti 6,000 ilipandwa shule ya msingi Sagani wilayani Magu huku akiitaka halmashauri hiyo kuhakikisha miti  iliyopandwa inatunzwa vyema kwa kuimwagilia maji ili ikue bila kubugudhiwa na mifugo pamoja na uchomaji moto ambapo miti itakayoshindwa kukua uwekwe utaratibu wa kurudishia mingine mapema.

Amesema  Wilaya ya Magu ni miongoni mwa wilaya chache zinazonyemelewa na ukame hapa nchini pia zipo dalili za hatari ikiwemo ukosefu wa mvua za kutosha na  zisizotabirika,  kuanza kukauka kwa baadhi ya vyanzo vya maji hivyo serikali imeona  maadhimisho hayo yatakuwa chachu kwa wananchi kupanda miti mingi zaidi katika maeneo wanayoishi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, amesema tangu Desemba 9 mwaka jana hadi Februari mwaka huu mkoa huo umepanda jumla ya miti 3,237,871 huku akiwataka wananchi, taasisi za serikali, binafsi na  wadau  wa misitu  mkoani humo waendelee  na juhudi za upandaji miti, uhifadhi wa misitu  ili kuiwezesha jamii kunufaika na bidhaa pamoja na hudama za misitu endelevu.

Kamishna wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, amesema  wamepokea  maelekezo ya waziri huyo na watahakikisha wanayatekeleza  kwa ufanisi huku akibainisha kwamba wameishaanza mkakati wa kuzijengea uwezo shule za  msingi na sekondari  ili zianzishe bustani zao na kuziendesha ili kuwa na misitu inayoweza kuzalisha  mahitaji mbalimbali ya binadamu ikiwemo kuni na ikabaki bila kuathirika.

Naye  Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Mwanza, Antony Diallo, aliyewakilishwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa chama hicho(UWT) mkoani humo, Ellen Bogohe, aliishauri serikali kurejesha utaratibu uliokuwepo miaka ya nyuma  kila mwanafunzi kupanda mti na kuutunza hadi atakapohitimu ili kuendelea kutunza mazingira.

Mmoja wa wakazi wa wilaya ya Magu,  Max Yombo, ambaye ana kitalu cha kuzalisha  miche mbalimbali amemkabidhi waziri huyo miche 1000 ikiwemo ya matunda na mbao ili wizara hiyo iipande maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni kuunga mkono jitihada za serikali katika kutunza na kuhifadhi mazingira.

Maadhimisho ya siku ya misitu duniani yanatokana na Azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la mwaka 2012 ambapo liliagiza nchi wanachama kuadhimisha siku ya misitu duniani Machi 21 kila mwaka malengo yakiwa ni kupaza sauti kwa ajili ya uhifadhi wa misituya aina zote na kuhifadhi mitiyote ambayo kwa namna moja au nyingine haipo maeneo ya hifadhi ya misitu kutokana na kutambua umuhimu wa misitu katika uhifadhi wa mazingira na maendeleo ya watu ambapo kauli mbiu ni uhifadhi wa mazingira na matumnizi endelevu.

 Tanzania imeadhimisha siku ya misitu duniani kwa mara ya kwanza mwaka huu huku  maadhimisho hayo yakiongozwa na Kauli mbiu isemayo ‘mti wangu, taifa langu, mazingira yangu, kazi iendelee’.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles