26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 17, 2024

Contact us: [email protected]

WIZARA YA KILIMO YATAKIWA KUFANYA UTAFITI WA UDONGO

Na Masanja Mabula-Pemba


WIZARA ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, imeshauriwa kufanya utafiti wa udongo katika mabonde ya Likoni na Kichangani, ili kuwapa maelekezo ya kitaalamu wakulima juu ya udongo na mbolea ambazo zinaendana na kuwafanya wakulima waweze kuzalisha chakula cha kutosha kujikimu.

Katibu Tawala Wilaya ndogo Kojani, Makame Khamis Makame, amelazimika kutoa ushauri huo baada ya kutembelea bonde ya Likoni na Kichangani ambapo wakulima wamedai kuwa ni mabadiliko ya tabianchi baada ya mazao yao kutostawi vyema.

Alisema pamoja na mabadiliko ya tabianchi, lakini iko haja kwa Wizara ya Kilimo kufanya utafiti wa udongo katika bonde hilo ili wakulima waweze kujua aina ya mbolea ambazo zinafaa kutumika katika mashamba yao.

Makame alisema kwamba, wakulima wa kunde katika mabonde hayo wameitikia wito wa Serikali kulima kwa wakati pamoja na kuzitumia mvua za vuli ambazo zimenyesha, lakini bado wanakabiliwa na changamoto ya kutojua aina ya mbolea inayofaaa kutumiwa.

“Tutaikumbusha Wizara ya Kilimo kufanya utafiti wa udongo katika bonde hili, kwani wakulima bado wanabahatisha kutumia mbolea wakati mwingine haziendani na udongo uliopo,” alieleza Makame.

Nao wakulima wa kunde katika bonde hilo, wamesema kwamba mbali na changamoto  hiyo pia wanakabiliwa na tatizo la aina ya wadudu mafuta (Aphids)  wanaoharibu mazao yao.

Kiula Juma Hija, amesema kwamba wadudu hao wanakuwa ni kero kubwa kwa wakulima wa kunde ambapo hata utaalamu wa kunyunyiza dawa wanaufanya kwa njia ya kienyeji.

Alisema njia ambazo wanazitumia ni kuchanganya dawa kwenye ndoo na kuanza kunyunyiza kwa kutumia vitambaa na baada ya hapo chombo ambacho kimetumika hurejea na kutumika kwa mahitaji mengine ya nyumbani.

Akizungumzia changamoto hiyo, Ofisa Maendeleo wa Kilimo Wilaya ya Wete, Makame Hamad Said, alisema kwamba, wanajipanga kuwapatia mabomba ya kunyunyiza dawa kwa kila kanda bomba moja ili kulinda usalama wa afya zao.

Alisema njia ambazo wanatumia wakulima hao zinahatarisha usalama wa maisha yao kwani dawa ni sumu na wanatakiwa vyombo wanavyovitumia visitumike kwa shughuli nyingine majumbani.

 

“Hii ni hatari sana kwa usalama wa maisha yao, tunajipanga kuwapatia bomba moja kila kanda kwa kuanzia ili kuwafanya watekeleze majukumu yao kwa ufanisi zaidi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles