30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

wizara ya Habari yaja na Bajeti ya bil 40

Ramadhan Hassan -Dodoma

WIZARA ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, imewasilisha bajeti ya zaidi ya Sh bilioni 40 kwa mwaka 2020/21 huku ikisema inakabiliwa na changamoto  ya kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia na utandawazi inayosababisha upotoshwaji wa mila, desturi na maadili hususani kwa vijana na wasanii.

Akiwasilisha mapato  na  makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/21, Waziri Habaro Dk. Harrison Mwakyembe, alisema wizara yake imeomba zaidi ya Sh bilioni 40 ambapo kwa mwaka 2019/20 iliomba zaidi ya Sh bilioni 30.

Waziri Mwakyembe alisema wanakabiliwa na changamoto ya kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia na utandawazi inayosababisha upotoshwaji wa mila, desturi na maadili hususan kwa vijana na wasanii.

Alisema  katika kukabiliana na changamoto hiyo, wizara imeendelea kutoa elimu na kuhamasisha jamii kwa njia mbalimbali ikiwemo makongamano, semina na warsha kuhusu umuhimu wa kuzingatia maadili, mila na desturi.

Alisema changamoto nyingine ni, kusimamia utekelezaji wa sheria zinazosimamia masuala ya habari, filamu, sanaa, muziki, ulimbwende na kazi zote za ubunifu.

Aidha kwa kuwa suala la maadili ni mtambuka, wazazi wanaaswa kuwalea watoto na vijana kwa kuzingatia dhana ya malezi na makuzi ya asili ya Kitanzania na kuepuka mila na desturi zisizoendana na utamaduni wetu.

Alisema changamoto nyingine ni kuwepo kwa baadhi ya vyombo vya habari vinavyotekeleza majukumu yao bila ya kuzingatia Sheria ya Huduma za Habari Na.12 ya mwaka 2016 na Sheria nyingine.

Vilevile, kumekuwepo na matumizi ya mitandao ya kijamii bila kuzingatia matakwa ya Sheria pamoja na maadili.

“Wizara imeendelea kutoa elimu na miongozo juu ya kuzingatia Sheria na taratibu katika utoaji wa taarifa na matumizi ya mitandao ya kijamii,”alisema.

“Uchakavu na upungufu wa miundombinu katika Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa),”alisema.

Alisema Ili kukabiliana na changamoto hizi, Wizara imetenga fedha za maendeleo katika mwaka 2020/21 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya taasisi.

Alisema katika bajeti ya mwaka 2020/21,    fedha za mishahara ni Sh. bilioni 20.98, matumizi mengineyo ni sh. bilioni 11.45 na miradi ya maendeleo ni Sh. bilioni 7.71.

Akizungumzia makadirio ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2020/21 alisema wizara inatarajia kukusanya Sh. milioni 960 kupitia Idara ya Habari-Maelezo  na Maendeleo ya Michezo.

Aidha, alisema kwa upande wa taasisi saba zilizo chini ya wizara kiasi kinachokadiriwa kukusanywa ni jumla ya zaidi ya Sh. Bilioni 40.17.

Akizungumzia mafaniko yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano, Dk. Mwakyembe alisema mafanikio yaliyopatikana katika wizara hiyo katika kipindi cha utawala huu ni ya kujivunia na yanapaswa kuendelezwa.

Alisema   wizara hiyo inalipa taifa heshima kubwa duniani, na ndio wizara ambayo kupitia sekta zake zote inalipa nguvu na uhai Taifa kwa kufanya vyema zaidi katika nyanja nyingine.

”Kwani bila sekta imara na inayowajibika kitaaluma ya habari, taifa litakosa taarifa na maarifa, na taifa lisilo na taarifa ni sawa na ndege asiye na mbawa, sekta za utamaduni, sanaa na michezo nazo pia ndizo msingi mkubwa wa afya na furaha kwa Watanzania,”alisema.

MAONI YA KAMATI

Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Peter Serukamba, alisema kamati inaendelea kuishauri Serikali kuongeza bajeti ya Baraza la Kiswahili  (Bakita)  ili iweze kujiandaa katika kutoa huduma mbalimbali kama ukalimani na tafsiri mbalimbali.

“Pamoja na  ufundishaji wa Kiswahili katika nchi za SADC na uandaaji wa mitaala ya kufundishia na kujifunza baada ya Kiswahili kuamuliwa kuanza kutumika katika nchi za SADC,”alisema.

Aidha alisema kamati inashauri Serikali itoe fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo  katika bajeti ya mwaka 2020-2021.

“Fedha hizo ambazo asilimia 83.3 ni fedha za mradi wa Uusikuvu wa TBC ni muhimu sana hasa ikizingatiwa changamoto ambazo TBC inakumbana nazo. Kamati inashauri Fedha hizo zitoke  kabla ya mwaka huu wa Fedha 2019/2020 kuisha ili kusaidia TBC kutekeleza malengo ambayo imejiwekea,”alisema Serukamba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles