27.2 C
Dar es Salaam
Thursday, June 13, 2024

Contact us: [email protected]

Wizara ya Afya yawezesha Wanawake kiuchumi miaka 60 ya Uhuru

Na Ranadhan Hassan, Dodoma

KATIKA kipindi cha miaka 60 ya Uhuru Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imewezesha Wanawake kiuchumi, imeimarisha mifumo ya kupambana na kuzuia vitendo vya ukatili kwa wanawake na Watoto na uwepo wa Sera, Sheria, Miongozo na mifumo ya kushughulikia masuala ya watoto.  

Hayo yameelezwa leo Novemba 8,2021 jijini Dodoma na Waziri wa Afya, Dk. Doroth Gwajima wakati akieleza mafanikio ya Wizara hiyo kwa miaka 60 ya uhuru, ambapo amesema Serikali katika kipindi cha miaka 60 imewezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika uchumi.

“Ikiwemo kuwezesha nyenzo mbalimbali ikijumuisha kutoa mikopo isiyo na riba inayotokana na kutengwa kwa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Mamlaka za serikali za Mitaa, Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake, Dirisha la mikopo kwa wanawake kupitia Benki ya Wanawake na sasa Benki ya Posta, VICOBA, SACCOS,” amesema Dk. Gwajima.

Pia amesema Serikali imeimarisha mifumo ya kupambana na kuzuia vitendo vya ukatili wa wanawake na Watoto kwa kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto yaani MTAKUWWA (2017/18 2021/22).

“Jitihada hizi zimewezesha kamati 18,186 mpaka sasa kuanzia ngazi ya Kijiji/Mtaa hadi Taifa. Aidha, yameanzishwa Madawati ya Jinsia na Watoto 420 katika vituo vya Polisi, Madawati ya Jinsia 153 katika Jeshi la Magereza na Dawati katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa ajili ya kupambana na vitendo vya rushwa ya ngono kupitia Kampeni ya ‘Vunja Ukimya’,”amesema Dk. Gwajima.

Amesema baada ya Uhuru serikali imejielekeza kwenye kuimarisha ustawi wa watoto ambapo, katika miaka ya mwanzo ya 1970 wizara ilikuwa inaratibu na kusimamia upatikanaji wa haki na ulinzi wa mtoto kwa kutumia Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977.

“Ili kuimarisha upatikanaji wa haki, maendeleo na ustawi wa mtoto, Serikali imeongeza wigo wa kutekeleza masuala ya watoto kwa  kuridhia na kusaini mikataba ya kikanda na kimataifa,”amesema.

Vilevile, amesema baada ya uhuru, serikali imepanua wigo wa majukwaa ya watoto katika kujadili masuala yanayowahusu ambapo, katika kipindi cha mwanzo cha Uhuru wa Tanzania Bara, jukwaa pekee la watoto la kujadili masuala yanayowahusu na kufikisha ujumbe ilikuwa ni kupitia shule ikijumuisha majukwaa kama chipukizi.

Amesema mfumo huo ulijumuisha watoto wale tu waliopo shule na kuwaacha watoto wasiokuwa shule na hivyo kutokutoa fursa sawa ya kushirikisha watoto wote.

Waziri Gwajima amesema mara baada ya Uhuru, serikali ilihakikisha uwepo wa Sera, Sheria, miongozo na mifumo ya kushughulikia masuala ya watoto ili kuimarisha mifumo ya kusimamia haki, ulinzi na ustawi wa watoto na kuwakinga dhidi ya ukatili wa aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na ukatili wa kimwili, kingono na kisaikolojia.

“Sera ya kwanza ya Maendeleo ya Mtoto iliandaliwa  mwaka 1996 na kurejewa 2008 ambayo imeainisha haki tano za msingi kwa watoto; haki ya kuishi, kuendelezwa, kulindwa, kushiriki na haki ya kutobaguliwa,”amesema.

Vilevile,amesema  Serikali imesajili jumla ya vituo 2,133 vya kulelea watoto wadogo mchana kwa ajili ya kutoa huduma za malezi na uchangamshi wa awali.

Aidha, ili kukabiliana na changamoto za afya na Maendeleo kwa Vijana Balehe Wizara iliratibu uandaaji na inasimamia utekelezaji wa Ajenda ya Kitaifa ya kuwekeza katika Afya na Maendeleo kwa Vijana Balehe (2021/22 – 2024/25).

“Lengo likiwa kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana balehe wenye umri wa 10-19 katika ya maeneo ya VVU/UKIMWI, mimba za utotoni, ukatili, lishe bora, kuendelea kuwa shuleni na kujengewa ujuzi ili kupata fursa za kiuchumi,” amesema Dk. Gwajima.

Aidha, katika kukabiliana na changamoto ya makao ya watoto, Serikali inaratibu na kusimamia jumla ya makao ya watoto 239 ikilinganishwa na makao moja yaliyokuwepo mwaka 1960.

Amesema, Serikali kwa kushirikiana na shirika la ABBOT FUND imejenga Makao ya Watoto katika Eneo la Kikombo Mkoani Dodoma ambayo yalizinduliwa na Mhe. Philip Isdor Mpango, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Ameongeza kuwa ushiriki wa wazee katika masuala mbalimbali ya kijamii na kimaendeleo umeimarika baada ya serikali kuweka utaratibu wa kuwa na Mabaraza ya Wazee katika ngazi zote, ambayo yameanzishwa kupitia Sera ya Taifa ya Wazee ya mwaka 2003.

Amesema Mabaraza 26 yameundwa katika mikoa yote ya Tanzania Bara na kufanya Mabaraza kufikia 20,748.

Aidha, amebainisha kuwa katika kipindi cha miaka 60 ya uhuru, Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa mashirika Yasiyokuwa ya Kiserikali  kwa kutunga Sheria Na. 24 ya mwaka 2002 ambayo ndiyo ilianza kuweka Taratibu za uratibu na usajili wa Mashirika hayo.

Aidha, katika kuimarisha utoaji wa huduma za usajili na uratibu Serikaliimefanikiwa kutengeneza Mfumo wa Kieletroniki wa Usajili na Uratibu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NIS) kwa lengo la kuboresha mazingira ya utendaji kazi ili kuleta ufanisi na tija katika uratibu wa Mashirika hayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles