27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WIZARA ARDHI NA UANZISHAJI KUTOA HUDUMA KIDIGITALI 

 

NA CHRISTINA GAULUHANGA-DAR ES SALAAM


KUKITHIRI kwa migogoro ya ardhi hapa nchini kulisababishwa na ugawaji ardhi na uuzaji  wake kiholela hali hiyo ilisababisha kila kukicha wananchi kugombania eneo moja kwa kuwa na wamiliki zaidi ya watu wawili pamoja na mipaka isiyo dhibitiwa.

Sasa Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imekuja na ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la kuondoa Migogoro ya ardhi iliyokuwa ikiendelea kutokana na changamoto ya usalama wa taarifa za ardhi ambao pia umekuwa ukisababisha hata kughushiwa kwa nyaraka hizo.

Pia ugumu wa kupata taarifa kwa wakati au  kwa usahihi, kuwepo kwa mianya ya rushwa na kutokuwepo kwa ufanisi katika utoaji wa huduma za ardhi nako ilikuwa ni changamoto zilizosababisha kuibuka kwa migogoro kila kukicha ndani ya jamii hasa kwa wafugaji na wakulima.

Mfumo Unganishi wa Taarifa za Ardhi (Integrated Land management Information System (ILMIS) umeanzishwa na Serikali ikiwa ni jitahada za kuunganisha mifumo mingi mbalimbali inayotumika hivi sasa Wizarani katika kutoa huduma za ardhi kwa wananchi kwa ubora zaidi.

Mfumo huo utarahisisha utaratibu wa upatikanaji wa hatimiliki za ardhi kwa kipindi kifupi zaidi kwa kusogeza huduma za upangaji, upimaji na usimamizi wa ardhi karibu na wananchi kuliko ilivyokuwa awali.

Mfumo huu mpya ambao ujenzi wa jengo lake umeshakamilika, utakuwa na mifumo midogo midogo sita ambayo itaunganishwa pamoja ili iweze kuonana na kuwasiliana. Mifumo hiyo inahusisha;

Mipango miji na upimaji ambao utahifadhi ramani za mipango miji (Town Planning Drawings) pamoja na ramani za upimaji wa ardhi, Utawala wa Ardhi na Usajili (kupitia  mfumo huo utawezesha kazi za idara husika ili ziweze kufanyika kwa njia ya Kielektroniki.

Mfumo huo utatunza nyaraka zote za waombaji na wamiliki wa ardhi kutoka idara zote za Ardhi, Fedha itasimamia malipo yote ya huduma ya ardhi kama vile kodi ya pango la Ardhi, ada na tozo mbalimbali za ardhi.

Pia kupitia mfumo huo utaweza kutoa taarifa za ardhi kwa wananchi na kwenye taasisi za Serikali na Mabenki nchini; na Huduma za TEHAMA ambao utawezesha usimamizi, ufuatiliaji na usalama wa mfumo wa ILMIS na pia kutoa huduma za kiufundi za TEHAMA.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano; Dk. Shaban Pazi anasema, Taarifa za masuala ya ardhi zitapatikana kwa kupitia mfumo unganishi wa taarifa za ardhi, katika ofisi za halmashauri, kanda na Wizarani pindi mwananchi atapofika katika ofisi husika.

“Taarifa zote za ardhi kuanzia upangaji wa ardhi, Upimaji, Usimamizi wa ardhi, uthamini na usajili zitakuwa zinapatikana katika mfumo huo, ’’anasema Pazi.

Anasema faida za mfumo huo,  kuwa ni kupunguza migogoro kwa kiasi kikubwa kwa sababu kumbukumbu zote za ardhi zitapatikana katika mfumo.

‘’ Kwa mfano ramani za mipango miji ambazo zinatumika katika kupanga matumizi ya ardhi zitatunzwa kidijitali katika mfumo, kwahiyo itaweza kugundulika kama mtu kajenga au kapatiwa kiwanja katika eneo ambao si la makazi. Pia kwa kuwa ramani za upimaji zitakuwa katika mfumo huo itabidhiti  kiwanja kimoja kutopimwa mara mbili au watu wawili kumilikishwa kiwanja kimoja,’’ anasema Pazi.

Inadaiwa mpaka sasa changamoto ambazo zimejitokeza katika maandalizi ya kuuwezesha mfumo kukamilika ni pamoja na; Uchakavu wa ramani au ramani kuchanika kwahiyo imebidi mtaalam wa mkandarasi IGN kutoka Ufaransa aje nchini kuzifanyia marekebisho ili ziweze kubadilishwa kwenda kwenye mfumo wa kidijitali.

Mfumo huo unategemewa kuanza kutumika rasmi mapema mwakani kwa kuanzia Manispaa ya Kinondoni na Ubungo kabla haujaendelezwa nchi nzima.

Anasema katika awamu ya pili mfumo utasimikwa katika halmashauri zote nchini, hivyo wananchi wote hata wale wa vijijini watapelekewa huduma za upangaji, upimaji na umilikishwaji wa ardhi karibu na wanapoishi.

“Serikali ya Tanzania ndio inayojenga mfumo huu kupitia mkopo kutoka Benki ya Dunia(WB), ambapo imeingia mkataba na mkandarasi kutoka nchini Ufaransa ili aweze kujenga mfumo katika kipindi cha miaka miwili cha awamu ya kwanza ,”anasema  Pazi.

Anasema mfumo utaweka huduma zote zinazohusu sekta ya ardhi kuwa wazi kwa kila mwananchi kujua ni nini wajibu wake na anatakiwa afanye nini ili kupata haki yake ya msingi.

Naye, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ; William Lukuvi anasema mfumo huo, utawezesha uhakika wa kuwa na usalama wa nyaraka za mmiliki.

’’Itakuwa vigumu kughushi nyaraka au kupoteza faili la mtu kwa makusudi ili mwananchi mwingine aweze kumilikishwa au hatimiliki itumike kukopea mkopo benki.  Pia kwa kuwa kutakuwa kuna ramani za msingi zijulikanazo kama  basemaps ambazo zitahuishwa na mipaka yote ya kiwanja husika itaonekana vizuri na hivyo kuweza kubaini kama kiwanja hicho kimeingiliana na kiwanja kingine au kimeingilia sehemu ya hifadhi ya serikali kama vile barabara,  ‘’ anasema Lukuvi..

Naye, Ofisa Mwandamizi wa Idara ya Tekinolojia ya Habari na Mawasiliano, Hamida John anataja faida hizo ni pamoja na mwananchi kuweza kupata taarifa za ardhi kwa gharama nafuu, haraka, uwazi, usahihi na mahali popote nchini.

Anasema mojawapo ya suluhu kuu ambayo Mfumo huo utafanya kwa wananchi, ni kwamba utawezesha utatuzi wa baadhi ya migogoro ya ardhi inayowakabili wananchi ambapo tatizo hilo limekuwa kubwa.

“Kumbukumbu za mwananchi zitahifadhiwa mahala salama na penye uhakika; kwani kila mmiliki ataweza kupata hatimiliki na miamala mingine ya ardhi kwa kipindi kifupi ukilinganisha na sasa; Mwananchi ataweza kupata huduma za ardhi kwa urahisi; pamoja na hatimilki ya ardhi ya mwananchi itahifadhiwa kwa usalama,”anasema Hamida..

Anasema usalama wa mfumo upo kwa kiwango bora, ambapo milango yote ya kuingilia katika mfumo itafungwa, na pia taarifa za ardhi zitakuwa vigumu kwa wahalifu wa mtandao kuweza kuchukua.

Hamida anasema njia ya kufuatilia utendaji kazi wa kila muhusika, kwahiyo mtumishi yeyote wa Wizara, Ofisi ya kanda na halmashauri atakayejaribu kufanya vitendo vya uhalifu katika mfumo ataweza kujulikana.

Mfumo huu pia utawezesha kuondoa urasimu uliokuwepo awali katika sekta ya ardhi na kuleta maendeleo haraka kwani itasaidia kila mwananchi kujinufaisha na ardhi yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles