JOSEPH HIZA Na Mashirika
HAWA si wanandoa ambao unaweza kuwahesabu kuwa mwanamume au mwanamke mnene kuliko wote duniani wala China. Bali kwa pamoja wawili hawa ndio wenzi wanene zaidi kuliko wote nchini China.
Wenzi hao vijana wamesafiri zaidi ya maili 1,700 kutoka Sichuan, kusini magharibi mwa China, kwenda Jilin, kaskazini mashariki mwa China, kupata tiba ya kupunguza unene wao.
Wenzi ambao kwa pamoja wana uzito wa 62 stone sawa na pauni 870 sawa na kilo 395.
Hilo linasababisha ugumu wa kupata mtoto ukizingatia changamoto ya kushiriki tendo la ndoa kwa unene walio nao.
Kwa kupunguza uzito, wanaamini itawasaidia kutimiza ndoto yao ya kupata mtoto mwenye afya njema.
Kwa sasa wako katika matibabu katika hospitali iliyopo Changchun, Jilin.
Lin Yue na mkewe Deng Yang kwa sasa wanaelekea katika umri miaka ya 30.
Ijapokuwa uzito wao umekuwa tatizo kwa muda mrefu – walilazimika kupata mavazi maalumu wakati wa ndoa yao– na sasa wameamua kwamba huu ni wakati wa kuchukua uamuzi kwa vitendo kupanua familia.
Kwa unene wao huo imekuwa ngumu kwao kushiriki tendo la ndoa, kwani hawakuwahi kufanya hivyo tangu waoane mwaka 2010.
Kwa sasa, Lin ambaye anafanya kazi kiwandani ana urefu wa futi tano na inchi nne lakini ana kiuno cha inchi 63.
Mkewe, ambaye amefanya kazi kama muuguzi ana urefu wa futi tano na inchi tatu na kiuno cha inchi 67.
Kulinganisha na wastani wa uzito wa pauni 150 sawa na kilo 68 kwa wanaume na pauni 126 sawa na kilo 57 kwa wanawake nchini China, Lin na Deng kwa pamoja wana uzito wa mara tatu wa ule wa wastani wa wenzi wa kawaida.
Uzito wao umewasababishia matatizo mengi hadharani nchini China, ambako unene unabezwa au kudhihakiwa.
Lin na Deng wamejaribu kubakia nyumbani kwa kadiri inavyowezekana kuepuka dhihaka na waliagiza sehemu kubwa vyakula na nguo zao kupitia mtandao.
Hata hivyo, wenzi hao kwa sasa wanataka kupata mtoto na wanahisi kupunguza uzito kutawasaidia kuweza kushiriki tendo la ndoa na kupata mimba.
Katika hospitali moja huko Changchun, walichukuliwa vipimo vyao na kuwekwa katika ratiba ya mazoezi pamoja na mlo maalumu.
Haijaweza kufahamika iwapo wenzi hao watasaidiwa tatizo lao hilo kwa njia ya upasuaji.
Lakini Deng ana matumaini yeye na mumewe watakuwa na picha mpya za ndoa zao mwishoni mwa matibabu hayo.
Jaribio lao la kujaribu kupunguza uzito linakuja mwezi mmoja baada ya mwanamke mnene kuliko wote nchini China kupunguza uzito na kupata mpenzi.
Qian Qian, kutoka Changchun, alikuwa na uzito wa robo tani wa kilo 244 wakati alipofanyiwa upasuaji.
Deng anasema kwamba ndoto ya kuwa mzazi pekee ilitosha kuwafanya wajaribu kupunguza uzito.
Lakini pia wanasema walitiwa moyo kuchukua hatua hiyo baada ya mafanikio ya Qian kuweza kupunguza uzito.