NA KYALAA SEHEYE-DAR ES SALAAM
MWIGIZAJI na mrembo wa taji la Tanzania mwaka 2006 Wema Sepetu, amedai anapokea vitisho vya kupotezwa kama ataendelea na msimamo wake wa kuitumikia Chadema.
Akizungumza na MTANZANIA jana kwa njia ya simu Wema alisema yeye hatishwi na chochote, ameshaamua na hakuna mtu yeyote atakaebadili mawazo yake kwa kuwa anachohitaji ni amani ya moyo wake na kuwa huru kwani alikokuwa aliona nchi ilikuwa inaenda kubaya.
“Ninatishiwa sana, napigiwa simu na kutumiwa ujumbe mfupi wa maneno kwenye akaunti zangu na kwenye mitandao ya kijamii.
“Mimi siogopi, nimeshaamua na hakuna wa kunizuia kwa hilo, kwani tangu nimeingia katika chama hiki nina amani ya moyo na ninahisi nimetua mzigo mzito niliokuwa nimeubeba,” alisema Wema.
Alifafanua kuwa baadhi ya vitisho anavyopata ni matusi ya nguoni ambapo anaweza kupigiwa simu na kutukanwa, wengine kumtumia ujumbe mfupi wakidai watampoteza lakini anauhakika anayeweza kupoteza maisha yake ni Mungu.
Aliongeza kuwa anajua amepata maadui ila anauhakika ni wachache sana kwani wengi wanamuunga mkono na ukizingatia watu wake wa karibu wote wako naye bega kwa bega hivyo hana sababu za kuogopa na anauhakika yuko kwenye chama makini kinachojua nini maana ya demokrasia.
“Hakuna mtu muhimu kama mzazi wako kama anakupa sapoti ya kutosha basi hakuna mwingine atakayeweza kuzuia hilo, nashukuru wamejua nini ninakihitaji na ninataka kuonyesha nini nilichokuwa nacho ambacho nilikokuwa hawakukiona,” alisema Wema Sepetu.
Kwa sasa Wema yuko katika ziara ya kutambulishwa mikoa yote kwa wanachama na wapenzi wa Chadema na jana ameanzia Arusha kumtia moyo Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, anayekabiliwa na kesi ya uchochezi.