Derick Milton, Itilima
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amewataka wazazi kuacha tabia ya kuwageuza watoto wao hasa wanafunzi wa kike kuwa mitaji ya kipato chao ikiwemo kuwaozesha, na badala yake wawasaidie katika kupata elimu ili wawe msaada mkubwa wa baadaye.
Amewataka wazazi wawekeze zaidi elimu kwa watoto wao wakiwemo wakiume ambao wamekuwa wakiwakataza kwenda shule na badala yake wachunge mifugo ambapo aliwaeleza uwekezaji wa elimu ndiyo msingi bora zaidi kwa maisha ya kesho.
Ole Nasha ameyasema hayo leo alipokuwa katika ziara ya kikazi wilayani Itilima mkoani Simiyu baada ya kukagua ujenzi wa mabweni ya wasichana shule ya sekondari Nkoma, ofisi ya wathibiti ubora na jengo la veta linaloendelea kujengwa katika kijiji cha Kanadi wilayani humo.
Amewataka wazazi kuwekeza zaidi kwenye elimu ili kuwa na mtaji mzuri baadae huku akisisitiza kuwa mtoto wa kike ana haki sawa ya kupata elimu sawa na mtoto wa kiume ambapo katika jamii nyingi bado hazijawapa kipaumbele cha kupata elimu.
‘’Kuna baadhi ya wazazi bado wanashawishi watoto wao kufanya vibaya katika mitihani yao ya mwisho ili wasiendelee na masomo, niwaombe msishawishi watoto wa kike na kuwatilia vikwazo vya kukatisha masomo mtoto wa kike ana nafasi ya kupata elimu sawa na mtoto wa kiume na pia mtoto wa kike ni wa serikali, hivyo mnaowakatisha masomo mtakiona cha moto’’ amesema Naibu Waziri Ole Nasha.