Asha Bani, Dar es Salaam
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, amesema wawekezaji zaidi wanahitajika kwenye mashamba ya miwa na michikichi ili kukabiliana na upungufu wa sukari na mafuta ya kula nchini.
Hasunga amesema hayo leo Jumatatu Februari 11, jijini Dar es salaam wakati akizungumza na wataalamu wa kilimo na watafiti waliokutana kwa ajili ya kuweka mikakati ya kukuza kilimo kitakachosaidia kuingia katika uchumi wa kati kuelekea uchumi wa viwanda nchini.
Amesema tani 670,000 zinahitajika kukidhi mahitaji ya Watanzania lakini uwezo wa uzalishaji ni tani 300,000 hivyo kuna upungufu wa tani 370,000 ambazo zinaagizwa kutoka nje.
“Wawekezaji wakijikita zaidi katika kulima miwa tatizo hilo litakuwa historia na hata sukari itakuwepo ya matumizi na biashara pia,” amesema.
Akizungumzia uhitaji wa mafuta ya kula, amesema yanazalishwa asilimia 36 na asilimia 64 yanaagizwa nje ya nchi na kufanya nchi kutumia mabilioni ya fedha.
“Hapa ni lazima tushirikiane kwa pamoja watafiti wasomi wetu na wakulima kuhakikisha inawekwa mikakati kamambe kuwavutia wawekezaji waweze kulima mashamba makubwa ya miwa na michikichi ili kupata mazao hayo ambayo licha kuwa chakula pia ni biashara,” amesema Hasunga.