28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI WA JK ATISHWA KWA RISASI

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


ALIYEKUWA Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima, ametishiwa kufyatuliwa risasi na askari polisi.

Hili ni tukio la pili kutokea baada ya aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, kutishiwa bastola hadharani.

Katika video iliyoanza kusambaa kwenye mitandao ya kijamii jana, linaonekana gari aina ya Land Cruiser lenye namba T 296 ATW, ambalo liliegeshwa pembeni kisha wakashuka askari wawili – mmoja wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) na mwingine polisi wa kawaida.

Askari huyo wa FFU baada ya kushuka kwenye gari hilo, alinyanyua bunduki na kufyatua risasi hewani kabla mwenzake kumfwata na kumshika kifuani na kutaka kumrudisha katika gari.

Kisha alimfuata Malima na kuzungumza naye na wakati wakiendelea, yule askari aliyefyatua risasi naye alikuja na kumsukuma mara mbili waziri huyo wa zamani, kisha akanyanyua bunduki juu.

Askari huyo alisikika akitamka: “Kwanini hamuheshimu, kwanini hamuheshimu Serikali nyie, mzee heshimu Serikali, mimi nimewekwa kuitumikia Serikali, siwezi kudharaulika.”

Mtu mwingine wa pembeni ambaye hakuonekana katika video hiyo, alisikika akisema: “Huna mamlaka, huna mamlaka ya kutishia.”

Wakati wote huo, Malima alionekana akiwa ameweka mikono mfukoni mwa suruali yake.

Baada ya majibizano, mmoja wa askari alionekana akimsihi mwenzake waende katika gari, huku akitamka “Poti, Poti, Poti ee.” 

 

CHANZO CHA TUKIO

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea katika eneo la Masaki jijini Dar es Salaam jirani na Hoteli ya Double Tree, ambako dereva wa Malima aliegesha gari vibaya.

Hatua hiyo ilisababisha kutokea kwa majibizano kati ya maofisa wa Kampuni ya Udalali ya Majembe kabla polisi kuingilia kati na kufyatua risasi juu.

Inaelezwa kuwa Malima alifika akiwa kwenye gari jingine na kukuta mzozo unaendelea.

 

KAULI YA POLISI

Akizungumza na MTANZANIA, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Suzan Kaganda, alisema ufafanuzi kuhusu tukio hilo utatolewa leo.

Pia alisema wanaendelea kumhoji Malima katika Kituo cha Polisi Oysterbay.

“Polisi walikuwa wanafanya ukamataji, lakini tukio litatolewa ufafanuzi kesho (leo)… kuna mambo mawili, kuna kumshikilia na kumhoji, sisi tunamuhoji,” alisema Kaganda.

 

WAZIRI MWIGULU

MTANZANIA lilipomtafuta kwa simu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba kuzungumzia tukio hilo, aliomba atumiwe ujumbe mfupi na hata alipotumiwa hakujibu.

 

LEMA AONYA

Akizungumza na MTANZANIA, Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Godbless Lema, alisema roho za visasi zinaendelea kujengwa kati ya raia na polisi na hivyo taifa linakoelekea ni kubaya kwani litapoteza dira na amani.

“Nimesikitika na nampa pole Malima, matukio ya aina hii yako mengi. Kama imefika mahali tunatoleana SMG hadharani, hakuna mtu ambaye yuko salama katika nchi hii,” alisema.

Lema alikwenda mbali na kugusia matukio yaliyowahi kutokea, likiwamo lile la aliyekuwa Waziri wa Habari, Nape na kusema kuwa hata aliyemtishia bastola hajakamatwa.

“Kama kusipokuwa na udhibiti watu watauana hadharani, tukio la kubishania parking (maegesho) si la kurushiana risasi, ni suala la maelewano tu,” alisema.

 

TUKIO LA NAPE

Machi 23, mwaka huu, Nape alitishiwa bastola akiwa nje ya Hoteli ya Protea jijini Dar es Salaam, alipotaka kuzungumza na waandishi wa habari.

Tukio hilo lilitokea saa chache baada ya Rais Dk. John Magufuli kumvua uwaziri.

[embedyt] https://www.youtube.com/watch?v=oEdovxg2Fn0[/embedyt]

Nape alipanga kuzungumza na vyombo vya habari, lakini harakati zake zilitiwa dosari, ikiwamo kuzuiwa kufanya mkutano ndani ya Hoteli ya Protea na kuamua kuzungumza nje ya hoteli hiyo.

Hata hivyo, kabla ya kushuka katika gari kuzungumza na vyombo vya habari, alifuatwa na watu wawili waliodaiwa kuwa ni askari na kutaka kumzuia asishuke.

Mmoja wa watu hao alichomoa bastola na kumtishia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles