26.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, January 18, 2022

WALICHOPANDA NDICHO WALICHOVUNA VPL 2016/17

Na ZAINAB IDDY, DAR ES SALAAM

LIGI Kuu Tanzania Bara msimu wa 2016/17 unatia nanga Jumamosi ijayo kwa mechi mbalimbali kuchezwa kwenye viwanja nane tofauti hapa nchini.

Msimu huu jumla ya timu 16 zilipata nafasi ya kushiriki ligi hiyo, huku kila mmoja ikionekana kutoa changamoto kwa nyingine.

Ushindani ulioonyeshwa msimu huu kwenye ligi umetokana na maandalizi yaliofanywa na kila timu, kulingana na nafasi na fedha walizonazo.

Vigumu kutabiri bingwa ninani kutokana na timu zinazowania taji hilo kupishana kwa pointi ndogo, lakini kwa upande wa zile zinazoshuka daraja tayari JKT Ruvu imejiondoa, baada ya pointi walizonazo pamoja na michezo waliyobakisha kushindwa kuwabakiza.

SPOTIKIKI wiki hii inakuletea walichopanda na kuvuna timu zote 16 zilizoshiriki ligi msimu huu, ikiwa ni kabla ya mechi za mwisho wa wiki iliyopita.

Simba SC

Huu ni msimu wenye mafanikio kwa Simba  kutokana na ubora wa kikosi chao, benchi la ufundi pamoja na umoja uliooneshwa na wanachama kwa ujumla wao.

Msimu huu Simba ilionekana kufanya usajili makini kwa kuwapa nafasi wanandinga wenye damu changa, jambo lililosababisha kuwa na kikosi imara kila idara na hivyo kutoa upinzani mkubwa kwa Yanga, wanaoonekana ndio wapinzani wao katika mbio  za ubingwa msimu huu.

Mbali na taji la ligi msimu huu,  Simba ilionekana kuchanga karata zake vizuri pia kwenye kombe la FA, baada ya kupigana na kufanikiwa kuingia hatua ya fainali  ya kuwania taji hilo litakalowapa nafasi ya kushiriki mashindano ya kombe la Shirikisho Barani Afrika mwakani iwapo kama watakosa lile la Ligi Kuu.

Mbeya City

Wagonga nyundo hao wa mkoa wa Mbeya msimu huu si wale walioonekana kwenye  misimu miwili iliyopita, kwani licha ya kuwa na  wachezaji mahiri kama Kenny Ally na wakongwe wa ligi,  Zahoro Pazi pamoja na Mrisho Ngassa,  bado wameshindwa kupata matokeo ya kuridhisha kwa asilimia 100.

Mbeya City chini ya kocha wake Kinnah Phiri,imeonyesha ushujaa kwa Yanga tu wakiwa nyumbani, baada ya kuwafunga mabao 2-1 lakini kwenye mechi nyingine wamekuwa si jambo la ajabu kuona wakinyukwa mabao zaidi ya matatu na kuendelea, jambo lililohatarisha mipango yao ya kuwa ndani ya tano bora kwenye msimamo wa ligi, pia kuhatarisha pia kibarua cha kocha Phiri.

Kagera Sugar

Moja ya timu ambazo hazikuwa na mwanzo mzuri kwenye ligi na hii ni baada  ya kubadilishwa kwa benchi lake la ufundi na kukabidhiwa Mecky Mexime, ambaye alipigana hadi sasa kikosi hicho kuwa miongoni mwa vikosi vinavyowania nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi.

Jambo kubwa lililoleta uzima ndani ya Kagera ni mabadiliko ya dirisha dogo la usajili, baada ya kusajiliwa kipa Juma Kasejana  mshambuliaji Ame Ally.  huku Mbaraka Yusuph akionekana kuimarika zaidi katika suala la kucheka na nyavu, hivyo kuipa matokeo mazuri timu yao ambayo kabla ya mechi za mwisho wa wiki ilikuwa ikishika nafasi ya nne ikiwa na pointi 47 nyuma ya Azam wenye alama 49.

Mwadui FC

Haina mabadiliko makubwa katika misimu yake miwili ya ligi tangu ilipopanda daraja chini ya kocha Jamhuri Kihwelo 'Julio', kwani matokeo ya kufungwa na kushinda ni jambo la kawaida kwao.

Mwanzoni mwa msimu huu, mambo yameonekana kuwa tofauti baada ya Julio kuamua kuachia ngazi na sababu kubwa akilalamikia timu yake kunyongwa na waamuzi, huku wahusika Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) wakiwa kimya, jambo ambalo kiuhalisia ni kawaida lakini pia kikosi chake hakikuwa cha ushindani.

Kuondoka kwa Julio kulitoa nafasi kwa kocha msaidizi Khalid Adam kuvaa viatu, vyake kabla ya kuja kukabidhiwa mikoba Ally Bushir, lakini hakuna mabadiliko yalioonekana kwani hadi michezo 28 imekujana pointi 35, ikiwa nafasi ya sita.

Tanzania Prisons

Kikosi hiki cha maafande wa Magereza msimu huu wa ligi umeonekana kutokuwa rafiki kwao, baada kutoonyesha cheche walizokuwa nazo msimu uliopita wakinolewa na Salum Mayanga aliyetimkia Mtibwa Sugar, kabla ya kupata dili la kufundisha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Katika msimu huu wakiwa na kocha Abdallah Mohammed ‘Bares’, Prisons wamejikuta wakipoteza michezo 11, sare 10 huku wakishinda mechi saba pekee, hadi sasa wakiwa na pointi 31 wakishika nafasi ya 11, kitu ambacho hakikuonekana kwenye ligi iliyopita na hiyo imetokana na kushindwa kujipanga kuanzia katika hatua ya usajili.

Yanga SC

Kosa kubwa wanaloweza kujilaumu Yanga msimu huu ni kufanya mabadiliko katika benchi lake la ufundi kwa kumtoa Mholanzi Hans Van der Pluijm na kumpa majukumu mengine kama Mkurugezi wa ufundi kabla ya kuvunja mkataba wake na nafasi yake ya ukocha kuchukuliwa na Mzambia George Lwandamina, aliyeanza kazi katika duru la pili.

Mabadiliko hayo yakichangiwa na migomo ya mara kwa mara kwa wachezaji kutokana na kudai fedha zao za mishahara, kumewafanya wachezaji kutocheza kwa hali na kujikuta wakipoteza mechi hata kwa timu ambazo hazikutegemewa.

Licha ya kuwa na nafasi kubwa ya kutetea taji lao la ligi kimahesabu, lakini wanaweza kujikuta wakilipoteza iwapo kama wataruhusu kufungwa kwenye mechi zao zilizobaki kwani hadi sasa wanapointi 62 wakiwa wamecheza michezo 27 na kubaki mitatu mkononi mbele ya Simba, wenye alama sawa lakini wakiwazidi kwa idadi ya mabao ya kufunga kabla ya mechi za mwisho wa juma lililopita.

Majimaji FC

Imekuwa ni kawaida kwa Wanalizombe kuponea tundu la sindano kushuka daraja, kwani kwa mwaka wa pili sasa wanahaha kujinusuru kushuka daraja.

Majimaji  ilianza kuonyesha dalili za kutouweza ushindani wa ligi, baada ya kufanya usajili usiokidhi viwango, kukosa fedha za kuwalipa mishahara wachezaji lakini hata baada ya kumrejesha kocha wao Kali Ongola aliyeinusuru msimu uliopita, bado hali tete inaonekana kuwaandama kwani kwenye msimamo wa ligi kabla ya michezo ya mwisho wa juma ilikuwa nafasi ya 15 ikiwa imecheza mechi 28 na kuwa na pointi 29 mbele ya JKT Ruvu iliyokwisha kuyaaga mashindano hayo.

Azam FC

Yaliowakuta msimu huu, hakuna aliyetarajia na hiyo inatokana na upinzani waliokuwa wakiuonyesha kwa miaka ya hivi karibuni, kwani wamezoeleka kuonekana kwenye mbio za kuwania taji la ligi na lile la FA, lakini mwaka huu wameshindwa licha ya kufanya usajili wa gharama kuanzia katika benchi la ufundi na hata wanandinga wa kigeni.

Msimu huu Azam walianza ligi, wakiwa na benchi jipya la ufundi lililoongozwa na Wahispani  lakini matokeo ya kusuasua katika mzunguko wa kwanza wa yalisababisha Wanalambalamba hao kuvunja mkataba nao na mikoba ikikabidhiwa kwa Aristica Ciaoba, anayeinoa timu tangu kuanza kwa mechi za mzunguko wa pili, akisadiana na mzawa Idd  Nassoro 'Cheche.'

Licha ya kubadili benchi la ufundi, Azam imeshindwa kuyafikia mafanikio ya kuliwania taji la ligi pamoja na lile la FA, hivyo kujikuta mwakani wakikosa nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa yale ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Stand United

Ni timu iliyoanza vizuri msimu huu, kiasi cha kuwaaminisha wadau wa soka  kuwa uenda ikawa ndani ya timu mbili bora kwenye msimamo, lakini mgogoro wa viongozi umeweza kuchangia kuivuruga Stand iliyokuwa na kocha Patrick Liewig, kabla ya kukabidhiwa kwa Athumani Bilali ‘Bilo’ na kisha Hemed Morocco.

Liewig aliamua kuvunja ndoa na Stand kwa kile alichokidai kuwa ni vuta nikuvute ya malipo ya mshahara wake, baada ya wadhamini wao wakuu kampuni ya madini ya Acacia kujiondoa, sababu kubwa ikiwa ni kuzuka kwa makundi mawili yanayokidhana ya Stand United na Stand Kampuni.

Tangu kuondoka kwa Liewig aliyefanya usajili wa timu hiyo msimu huu, wachezaji walianza kupoteza  morari ya kucheza ikichagizwa na makundi yaliojitokeza na hivyo Stand kujikuta ikishuka kutoka nafasi ya pili iliyoshika hadi kuja kuwania nafasi ya tano, hivi sasa ikiwa na pointi 37 michezo 28 nyuma ya Mtibwa Sugar.

Toto Africans

Msimu uliopita Toto ilionekana kuwa tishio, lakini mgogoro wa wenyewe kwa wenyewe ndani ya timu umeonekana kuwamaliza.

Toto ilianza ligi msimu huu ikiwa na Rogatian Kaijage kabla ya kujiuzulu kwa kile alichodai uongozi kushindwa kutimiza mahitaji ya timu, huku kijiti chake  kikichukuliwa na Halfan Ngasa kisha majukumu kubaki kwa Flugence Novatus, lakini bado matokeo mabovu yaliochangiwa na ukata, migogoro ya mara kwa mara kwa wachezaji imewafanya kuwa katika hati hati ya kushuka baada ya kukusanya pointi 29 katika michezo 27 iliyocheza.

Ndanda FC

Imekuwa na bahati ya kufundishwa na wazee wawili Hamimu Mawazo na Meja Mstaafu Abdull Mingange, wanaobadilishana vijiti, lakini msimu huu timu hii imeonekana kuwa kwenye hali mbaya kiuchumi iliyoleta pia matokeo yasiyoridhisha uwanjani.

Msimu huu wameonekana wakifanya usajili wa funika bovu kiasi cha kujikuta miongoni mwa timu zinazoweza kushuka daraja, kwani kwenye mechi 28 walizocheza wamepata pointi 30 ambazo kama wanaowafuata wataweza kushinda mechi zao zilizosalia nao kupoteza msimu ujao hawatokuwepo katika ligi.

JKT Ruvu

Licha ya msimu huu kufundishwa na makocha watatu katika vipindi tofauti, lakini imekuwa ya kwanza kuaga Ligi Kuu Tanzania Bara na hivyo msimu ujao wataonekana Ligi Daraja la Kwanza.

JKT Ruvu ambayo imefia mikononi mwa kocha, Abdallah Kibaden, kabla ya hapo ilishafundishwa na Bakari Shime aliyepokea mikoba ya Felix Minziro, lakini  msimu huu walianza kuonyesha hali ya kutokuwa vizuri mwanzoni mwa ligi, baada ya kukubali vipigo vinne mfululizo kiasi cha kocha wake Minziro kuamua kujiudhuri.

Kabla ya mechi za mwisho wa wiki iliyopita, JKT Ruvu walikuwa wakishika nafasi ya mwisho wakiwa na pointi 23, huku wakibakiwa na michezo miwili ambayo hata kama watashinda watafikisha alama 29 ambazo haziwatoshi kubaki kwenye ligi hiyo.

Mtibwa Sugar

Ni timu iliyoweza kutoa changamoto kubwa msimu huu, baada ya ujio wa kocha Salum Mayanga, lakini tangu kuondoka kwake imejikuta ikipokea vipigo vya aibu ikiwemo kile cha 5-0 walichokipata kwa Mbao FC, mzunguko wa pili lakini jambo baya kwao wameshindwa kulinda heshima yao ya kutofungwa na Yanga, wakiwa uwanja wao wa nyumbani.

Hadi mzunguko wa kwanza wa ligi unamalizika, Mtibwa chini ya Mayanga walikuwa ndani ya tano bora za juu baada ya kushinda mechi sita, sare tano na kupoteza michezo mitatu, nafasi ambazo wanaipigania hadi sasa wakiwa sambamba na Stand United  na Mwadui wanaopishana nao kwa alama mbili pekee, wakati wao wakiwa na pointi 37.
 

Ruvu Shooting

Ilibahatika kurejea tena kwenye ligi msimu huu, baada ya kushuka na kujikuta wakishiriki Ligi Daraja la Kwanza  msimu uliopita.

Baada ya kupanda  kikosi hicho kilichonolewa na makocha wawili hadi sasa, kimeweza kuonyesha wazi kuwa kushuka kwao daraja haikuwa na maana hawana uwezo,  baada ya kutoa changamoto kubwa kwa baadhi ya timu za Ligi Kuu ingawa wameshindwa kuvua uteja wao mbele ya Yanga.

Hadi sasa Ruvu Shooting inasiliami 100 ya kusalia kwenye ligi msimu ujao, baada ya kucheza mechi 28 na kukusanya pointi 33 ambazo zinawabakisha na hii inatokana na kuanza vizuri kwenye mechi zake msimu huu.

African Lyon

Imepata nafasi ya kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, ikiwa ni baada ya kuikosa kwa misimu miwili iliyopita, lakini ujio wao haukuweza kuleta changamoto iliyotarajiwa na wengi kutokana na historia waliyowai kujiwekea katika ligi.

Walianza ligi na Mreno Bernado Taveres, kabla ya ujio wa Mkenya Charles Otieno, lakini wameonekana kushindwa kutoa changamoto kiasi cha kujikuta mguu ndani, mguu nje kushuka daraja  na hadi sasa wapo nafasi ya 10 wakiwa na alama 31 ambazo wanapishana kwa alama  moja na timu zinazomfuata nyuma, ukiitoa JKT Ruvu iliyokwisha kushuka daraja.

Mbao FC

Wakati ikiteuliwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF) kucheza Ligi Kuu, mashabiki wengi wa soka walitegemea kuwa  ingekuwa si tu ‘jamvi la wageni’, lakini pia ingekuwa timu ya kwanza kushuka daraja msimu huu  na hiyo ni kutokana na kuonekana iliteuliwa ghafla, baada ya kufutwa kwa matokeo ya timu za Geita Gold, Polisi Tabora, JKT Oljoro na JKT Kanembo zilizokubwa na mkasa wa upangaji matokeo katika mechi za mwisho za Ligi Daraja la Kwanza, hivyo Mbao  kupandishwa kutokana na kuongoza kwenye kundi C.

Kupata nafasi ya kushiriki ligi msimu huu, Mbao imeonyesha wazi kuwa haijaja kibahati kama inavyodhaniwa, baada ya kuonyesha usumbufu mkubwa kwa timu zinazoshiriki ligi hiyo ikiwemo Yanga na Azam kiasi cha kuitishia pia Simba.

Ikiwa na kocha wake Mrundi, Etienne Ndairagije, Mbao imeweza kuzifunga Azam na Yanga katika mechi za Ligi lakini pia kuwatoa Wanajangwani kwenye kutetea taji lao la FA, hivyo kutinga fainali watakayokipiga na Simba Mei 28 mwaka huu Uwanja wa Jamhuri Dodoma.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
174,926FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles