SEOUL, KOREA KUSINI
RAIS Moon Jae-in wa Korea Kusini, amemfukuza kazi Waziri wa Fedha, Kim Dong-yeon na msimamizi mkuu wa sera, Jang Ha-sung, wakati ambapo taifa hilo likikabiliana na kasi ndogo ya ukuaji uchumi na ongezeko la ukosefu wa ajira.
Msemaji wa Ikulu ya Korea Kusini, Yoon Young-chan, amesema jana kuwa nafasi hizo tayari zimeshajazwa. Imeelezwa kuwa maofisa hao wamekuwa wakipingana katika kulishughulikia suala la uchumi.
Serikali ya Moon imeongeza kima cha mshahara pamoja na kupunguza muda wa kufanya kazi.
Wakosoaji wanasema hatua hiyo imewaathiri zaidi wanaopata kiwango cha chini cha mshahara na kampuni ndogo zimepunguza wafanyakazi, huku kampuni kubwa zikipunguza kuwekeza kutokana na sheria ngumu za uwezekaji.
Mwezi uliopita Benki Kuu ya Korea Kusini, ilipunguza makadirio ya ukuaji wa uchumi wake kwa mwaka huu hadi asilimia 2.7, ikiwa ni chini ya asilimia 3.1 zilizofikiwa mwaka uliopita.