NA RAMADHANI HASSAN,
SERIKALI imesema inafanya majaribio ya kuweka vifaa vya kupimia Ukimwi katika maduka ya kawaida.
Imesema majaribio hayo yakimalizika itaonekana njia gani inayofaa kuruhusu matumizi ya vifaa hivyo kununuliwa katika maduka hayo.
Hayo yalielezwa jana bungeni na Naibu Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Abdallah Kigwangwalla alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi (Chadema).
Mbilinyi alitaka kujua ni lini serikali itaweza kuweka vifaa vya kupima virusi vya ukimwi kila mmoja aweze kupima kwa wakati anaotaka.
“Suala la kupima afya ni jambo zuri na linatakiwa kuungwa mkono.
“Je, ni lini sasa serikali mtaweza kuweka vifaa ambavyo ni (disposable) ili iwe rahisi kupima mwenyewe anapoona a kuna haja ya kupima?” alihoji Mbilinyi.
Katika swali lake la msingi, Mbunge wa Tumbatu, Juma Othman Hija (CUF) alitaka kujua maana halisi ya virusi vya ukimwi na Ukimwi.
“Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa mtu anaweza kuwa na virusi vya UKIMWI lakini hana ugonjwa wa UKIMWI, je, nini maana ya maelezo haya?” alihoji Hija.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Dk. Khamisi Kigwangwalla alisema ugonjwa wa kifua kikuu ni ugonjwa pacha na ugonjwa wa Ukimwi kwa vile ugonjwa huo uonekana kutokana na kushuka kwa kinga mwilini.
Kuhusu vifaa vya Ukimwi kuwekwa katika maduka ya kawaida, Dk.Kigwangwalla alisema serikali kwa sasa ipo katika majaribio kuona kama jambo hilo linafaa na kuona kuwa litakuwa na tija kufanya hivyo na ikimalizika majaribio itaonekana njia gani inafaa.
Kuhusu Ukimwi na Virusi vya Ukimwi, Dk.Kigwangwalla alisema ni kweli kuwa mtu anaweza kuwa na Virusi vya Ukimwi lakini akawa hana ugonjwa wa Ukimwi.