YANGA YAKUBALI YAISHE KWA NIYONZIMA

0
528

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM

UONGOZI wa klabu ya Yanga umempa mkono wa kwaheri aliyekuwa mchezaji wao wa kimataifa raia wa Rwanda, Haruna Niyonzima, baada ya kushindwa kufikia mwafaka wa kuendelea naye katika kuelekea kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara 2017/18.

Niyonzima ambaye aliichezea Yanga kwa mafanikio makubwa kwa misimu sita mfululizo, mkataba wake unatarajia kuisha Julai mwaka huu.

Mchezaji huyo alishindwa kusaini mkataba mpya kwa waajiriwa wake hao, baada ya kushindwa kuafikiana kwa kile kinachodaiwa kuwa walimwahidi dau dogo, tofauti na wapinzani wao wa jadi Simba, ambao inasemekana kuwa wamempatia ofa kubwa na kukubali kumwaga wino kwenye klabu hiyo.

Klabu ya Simba inadaiwa kumpatia Niyonzima Dola 70,000 za Marekani (sawa na Sh milioni 156 za Tanzania), huku Yanga wakitaka kumpa kiasi cha Sh milioni 80.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa klabu hiyo, Boniface Mkwasa, alisema walikuwa na nia ya kuwa na Niyonzima kwa msimu ujao, lakini wameshindwa kutokana na kutoafikiana katika mazungumzo yao.

“Tulifanya jitihada za juu ili kuhakikisha tunakuwa na Niyonzima kwa msimu ujao, lakini hatukuweza kufikia mwafaka katika mazungumzo yetu na yeye, hivyo sisi kama klabu tunamtakia kila la kheri katika maisha yake mapya ya soka kwa ujumla,” alisema.

Alisema kwa masilahi ya klabu wameona ni bora wamruhusu ili aweze kuendelea na sehemu nyingine, ambayo itaweza kumpatia masilahi makubwa kwa faida yake pamoja na familia kwa ujumla.

Mkwasa alieeleza kwa sasa wanaendelea vizuri na usajili kwa wachezaji wengine, ambao wanawahitaji kwa msimu ujao wa ligi kuu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here