VERONICA ROMWALD NA RAMADHAN HASSAN – DODOMA
KIKAO cha Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu na wakazi wa Kijiji cha Humweka, jana kiligeuka kuwa ‘kaa la moto’ kwa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Charles Kiologwe na Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Dk Asteria Mpoto.
Katika kikao hicho, Waziri alipokea malalamiko kutoka kwa wakazi wa kijiji hicho hususan wazee ambao walidai kutopatiwa kadi za matibabu bure tangu serikali ilipotangaza hatua hiyo hadi sasa.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Salome Nesilwa alisema wanashangaa pia licha ya kupigwa picha na kukamilisha taratibu zote zilizotakiwa bado hawajapatiwa kadi za bima ya afya tangu Januari hadi sasa.
“Tulipigwa picha tukajiandikisha lakini kila tulipouliza tuliambiwa picha zetu hazionekani na majina yetu hayasomi hivyo hadi leo hatujui hatima ya kadi zetu za matibabu,” alimueleza Waziri Ummy.
Waziri Ummy alimtaka Dk. Kiologwe kujibu hoja hizo, naye alimmtaka Dk. Mpoto kujibu badala yake.
Akitoa majibu ya suala hilo, Dk. Mpoto alisema tayari wamewatambua wazee 950 wa kijiji hicho ambao wanastahili kupatiwa kadi za matibabu bure na wanakusudia kuwapatia kadi hizo wakati wowote kuanzia sasa kwa awamu ya kwanza ambayo wanakusudia kuwapatia wazee 1000.
Waziri Ummy alionekana kutoridhika na majibu hayo na kuwaagiza, Dk. Kiologwe na Dk. Mpoto kuhakikisha wanalitekeleza jambo hilo ndani ya miezi miwili kuanzia sasa.
“Asilimia 18 ya wananchi naona wapo tayari kukata bima ya CHF, Dk. Kiologwe mlikuwa mnafanya vizuri mmekwama wapi? Nataka ndani ya miezi miwili kazi hiyo iwe imefanyika, wazee wawe wamepewa kadi za matibabu bure.
“Nataka muwafikie asilimia 60 ya wananchi wawe wamepata kadi za CHF, kuna malalamiko pia nimeelezwa hapa kwamba licha ya wananchi kuwa na kadi za CHF kuna watumishi wa afya wanalipisha fedha wanapoenda kupata matibabu.