29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI UMMY AWASHUKIA MA-DC, RC WANAOWEKA NDANI MADAKTARI

Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA


WAZIRI wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, amegeuka mbogo kwa wakuu wa mikoa na wilaya wanaowaweka ndani madaktari, akisema hayupo tayari kuona jambo hilo likiendelea.

Hivi karibuni, Chama cha Madaktari (MAT) kiliwataka viongozi wa Serikali, hasa wakuu wa mikoa na wilaya, kuacha kuwadhalilisha watumishi wa umma na kumtangaza Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Christopher Ngubiagai, kuwa adui namba moja wa afya.

MAT pia ilimtaka mkuu huyo wa wilaya kuomba radhi madaktari kutokana na kitendo chake cha kumweka ndani Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Dk. Vitalis Katalyeba, baada ya kumwona mkutanoni wakati aliagiza asimamishwe kazi kwa kutuhumiwa kuchelewesha gari la kumpeleka mgonjwa hospitali na kusababisha kifo chake.

Chama hicho pia kiliwanyooshea kidole wateule wengine wawili wa rais, ambao ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo na Dk. Rehema Nchimbi wa Mkoa wa Singida kwa kuwatia ndani waganga wa wilaya zao.

Jana akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanayofanyika leo, Waziri Ummy alisema kwa sasa imekuwa kama fasheni kwa wakuu wa mikoa na wilaya kuwatia ndani madaktari na wauguzi kwa kisingizio cha kuwawajibisha.

Alisema jambo hilo hakubaliani nalo kwani kuna Baraza la Wauguzi na Wakunga na Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) ambayo ndiyo yenye haki ya kufanya kazi hiyo.

“Unapomtia ndani husaidii kumwajibisha, kama ni kosa la kitaaluma tuletee sisi tumpeleke kwenye Baraza la Wauguzi na Madaktari ambapo hapo atakuwa amefutiwa leseni na maana yake ni kuwa hawezi kufanya kazi mahala popote.

“Nitaendelea kuongea, hamtusaidii kumrekebisha huyu daktari au muuguzi kwa mbwembwe za kumweka ndani halafu mbele ya vyombo ya habari. Hapana, tuna Baraza la Madaktari, tuna Baraza la Wauguzi na Wakunga ambao wanatakiwa kufanya kazi hiyo.

“Mimi nipo kufuta cheti na leseni ya muuguzi yoyote, yaani nipo tayari pale ambapo imethibitika, tuleteeni hizi kesi, kuna makosa ya kinidhamu na makosa ya kitaaluma, hivyo watofautishe lipi la kumuweka ndani na lipi la kutokuweka ndani,” alisema.

Pia aliwataka madaktari na wauguzi kufanya kazi kwa kufuata taratibu na kanuni kwani kabla ya kuanza walipita katika kiapo.

Kuhusu wauguzi wanaotoa lugha za matusi kwa wagonjwa, Waziri Ummy alisema yupo tayari kufuta leseni zao ili watafute kazi nyingine za kufanya.

“Kama amekosea mwite DMO (Mganga Mkuu wa Wilaya) au RMO (Mganga Mkuu wa Mkoa) muelekeze, lete kwetu, baraza na mimi tutamshughulikia, nimeishalielekeza baraza kesi inapokuja ndani ya siku 14 nataka matokeo, kama mnamsimamisha na  tukikusimamisha kazi hata mshahara hapati,” alisema.

Pia alizitaka halmashauri kutenga fedha kwa afya ya mama na mtoto kwa kuhakikisha wanajenga vituo vya afya kwa kina mama kuweza kupata huduma hizo.

Kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mwanamke Duniani, Waziri Ummy aliwataka waajiri wote nchini kuacha mara moja utaratibu wa kuwaachisha kazi wanawake pindi wanapoenda kujifungua.

“Namtafuta mwajiri mmoja nitalala nae mbele, pia natoa onyo kwa waajiri, hasa katika sekta binafsi kuacha utaratibu wa kuwaachisha kazi wanawake, hasa wanapoenda kujifungua,” alisema.

Alisema umefika wakati wa mwanamke kufanya kazi kwa bidii na kuacha utegemezi kutoka kwa mwanaume, huku akiwataka wazazi na walezi kumsaidia mtoto wa kike aweze kupata elimu.

“Serikali inatambua kuwa ukatili dhidi ya mwanamke ni tatizo kubwa ambalo linaathiri ushiriki wa mwanamke katika shughuli za kiuchumi, hivyo nitoe rai kwa jamii kumsaidia mtoto wa kike ili aweze kufanikiwa katika njia anazopita,” alisema.

Wakati huo huo, wizara hiyo imetoa tamko kuhusu mwenendo wa ugonjwa wa kipindupindu kwa mwezi Februari mwaka huu, ambapo jumla ya watu 198 wamegundulika kuugua ugonjwa huo, huku wawili wakiripotiwa kufariki.

Waziri Ummy alisema hii ni tofauti na Januari ambapo kulikuwa na wagonjwa 823 na vifo 14.

“Kuna jumla ya mikoa saba ambayo ndiyo imeripoti kupatikana kwa ugonjwa huo kwa mwezi Februari ambayo ni Dar es Salaam wagonjwa 44 na kifo kimoja, Pwani wagonjwa 16, Mara (50), Dodoma (16), Morogoro (35), Kigoma (26, kifo kimoja) na Rukwa wagonjwa wawili.

“Ugonjwa wa kipindupindu bado upo kaika jamii, niisihi mikoa ambayo imekuwa ikificha taarifa kuwa hilo linaweza kuwa kosa la jinai kwani wamekuwa wakiogopa kutumbuliwa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles