24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI NAPE: NI RUKSA KUIKOSOA SERIKALI

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amevitaka vyombo vya habari kutoogopa kuikosoa Serikali kwa sababu imebeba dhamana kubwa ya kuliongoza taifa.

Amesema Serikali ina ajenda kadhaa za kutekeleza, ikiwamo uchumi wa viwanda, hivyo ni lazima vyombo vya habari vishiriki kikamilifu kwani bila kufanya hivyo Watanzania wengi wataachwa nyuma.

Akizungumza katika mkutano na wahariri na wamiliki wa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, alisema vyombo vya habari vinatakiwa kuwaleta pamoja Watanzania katika uchumi wa viwanda ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2025.

“Serikali ni rahisi sana kujisahau, ama inaweza ikaziba masikio, hivyo ni lazima pawepo na ‘very strong media’ zitakazofanya kazi ya kuiambia Serikali kwa namna fulani ya heshima, lakini ujumbe unafika.

“Najua kuna hofu na lazima tuchukue hatua tuiondoe, kwa sababu ikiendelea kuwepo watu watabaki na mafundofundo na si vizuri katika nchi. Hivyo muwe huru, Serikali si adui, nguvu yenu ni kubwa na msiposhiriki kikamilifu tutawaacha Watanzania wengi nyuma,” alisema Nape.

Katika kuthibitisha kwamba kuna hofu ya kuukosoa utawala wa Rais Dk. John Magufuli, Mhariri wa ITV, Steven Chuwa, alimweleza Nape kuwa katika siku za hivi karibuni, imekuwa ni shida kuwapata washiriki kwenye vipindi vyao mbalimbali.

 “Hivi sasa kupata washiriki kwenye vipindi ni shida, kuna urasimu mkubwa, waziri tusaidie kusafisha hali ya hewa kwa sababu kuna woga wa hali ya juu serikalini,” alisema Chuwa.

 

WAMILIKI, WAHARIRI

Awali wakizungumza katika mkutano huo, wamiliki na wahariri walilalamikia kuwapo kwa urasimu katika utoaji wa matangazo na watendaji wa Serikali kuficha habari na kutahadharisha kuwa kama hali hiyo itaendelea, vyombo vya habari vitashindwa kujiendesha.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, wachapishaji wa gazeti hili, RAI, Bingwa na Dimba, Erasto Matasia, alisema vyombo vya habari na Serikali vinategemeana na kushauri kuwe na chombo kitakachounganisha sekta zote.

“Vyombo vya habari vinaweza vikaanzisha mchakato, lakini ukazimwa kwa nguvu ya kisiasa, ukosoaji lengo lake si kuua, lakini kwanini kuwe na matamshi mengi wakati lengo letu ni moja na tunataka tufike mahali?” alihoji Matasia.

Naye Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jamhuri, Deodatus Balile, alishauri kupitiwa upya kwa mfumo wa ulipaji kodi kwa madai kuwa utakwamisha mpango wa Serikali wa uchumi wa viwanda.

“Kuna shida ambayo itatufanya tushindwe kushiriki kikamilifu, tukiomba matangazo tunaambiwa yanatolewa Daily News, Habari Leo na Uhuru. Kodi zipitiwe upya, ziwe zinalipika, kwa hali ilivyo sasa itabidi mtu ukope asilimia 23 ya mtaji halafu uilipe Serikali kodi zake,” alisema Balile.

Naye Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Theophil Makunga, alisema ushirikiano kati ya Serikali na vyombo vya habari ni muhimu ili viweze kushiriki vizuri katika mikakati mbalimbali ya maendeleo ya nchi.

“Asilimia 60 ya operesheni kwenye vyombo vya habari zinategemea matangazo na asilimia 40 mauzo ya nakala za magazeti. Hivyo, yakichukuliwa maamuzi ambayo yatasababisha vyombo vya habari vishindwe kujiendesha, tutarudi nyuma kama nchi,” alisema Makunga.

Katika hilo, Nape aliitaka Idara ya Habari – Maelezo kuwa wazi na kutenda haki katika utoaji wa matangazo ili vyombo vya habari viendelee kuwa salama.

“Nataka niwaahidi, kama nitaendelea kuwa waziri, uwazi utakuwepo na nitasimamia mwenyewe kuhakikisha kuna haki katika ugawaji wa matangazo. Iko hofu baadhi ya watu kutumia mwanya huu kwa sababu zao za kisiasa… kelele ni kubwa na tusiporekebisha hali hii ‘media’ zitakufa,” alisema.

Kwa upande wake, Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Dk. Jim Yonaz, alishauri vyombo vya habari vihamasishwe viwe na utashi wa kushiriki katika kuchochoea uchumi wa viwanda.

“Sisi tuna kalamu na tuna uelewa, sisi ni jeshi jingine pia ambalo tunalinda na kuendeleza nchi, hivyo badala ya kuambiwa kasemeni, tuwe washiriki katika ajenda hii ya uchumi wa viwanda,” alisema Dk. Yonaz.

Naye Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji wa Clouds Media, Ruge Mutahaba, alipendekeza kabla ya kufanywa uamuzi wowote, ni vyema zikaangaliwa athari za kiuchumi na kisiasa.

“Mfano shisha iko kwenye bajeti kama chanzo cha mapato, lakini leo hii tumepiga marufuku. Kumekuwa na maamuzi ya kisiasa bila kujali athari za kiuchumi, Tanzania ya viwanda haiwezi kujengwa na maamuzi na misimamo ya kisiasa,” alisema Mutahaba.

 

MKURUGENZI MAELEZO

Akijibu hoja kuhusu kuwapo kwa urasimu katika utoaji matangazo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari – Maelezo, Dk. Hassan Abbas, alisema matangazo yatatolewa kwa kuangalia vyombo vya habari vitakavyofanya vizuri.  

“Mfano kwenye ‘print’ kuna magazeti 470, hivyo sitaki niahidi kama kila mtu atapata, tutaangalia vyombo vya habari vitakavyofanya vizuri. Hivyo ‘perform’ yako kwenye soko ndiyo itakayokusaidia, tutaangalia na content (maudhui) ya habari zako kama zinavutia wasomaji,” alisema Dk. Abbas.

Kuhusu watendaji wanaoficha habari, alisema wanatarajia kuanzisha mfumo wa kuwafuatilia na kuwapima maofisa habari na wale watakaoshindwa kufikia malengo watachukuliwa hatua.

“Wakati mwingine inaniwia vigumu, naulizwa vitu vingi sana, mfano naweza kuulizwa suala la taasisi fulani wakati kuna msemaji na analipwa mshahara… kama wote hawa ni majipu, itafika mahali tutatafuta namna ya kuyatumbua,” alisema.

Wizara hiyo imeanzisha mchakato wa kukutana na tasnia mbalimbali zilizoko chini yake kila siku ya Jumanne na programu hiyo itakuwa ni ya mwaka mzima.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles