Winfrida Mtoi na Mitandao
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Jonson na Shirikisho la soka nchini humo (FA), wamelaani kitendo cha ubaguzi wa rangi katika mitandao ya kijamii dhidi ya wachezaji wa England Marcus Rashford, Jadon Sancho na Bukayo Saka baada ya fainali ya kombe la Euro 2020.
Wachezaji wote watatu walikosa penalti katika mchezo huo wa fainali uliokitunanisha England dhidi ya Italia waliotwaa ubingwa kwa ushindi wa penalti 3-2 kwenye Uwanja wa Wembley, Uingereza.
“Timu hii ya England inastahili kupongezwa kama mashujaa, sio kubaguliwa kwa msingi wa rangi kwenye mitandao ya kijamii. Wale wanaohusika na unyanyasaji huu mbaya wanapaswa kuona haya,” amesema Boris kwa mujibu wa BBC.
Aidha FA imesema:Imeshangazwa na matusi hayo ya ubaguzi wa rangi. Wachezaji wa England wamekuwa wakipiga magoti katika michuano ya Euro kuangazia vita vyao dhidi ya ubaguzi wa rangi katik timu yao.
“Tutafanya kila tuwezalo kusaidia wachezaji walioathiriwa huku tukisisitiza adhabu kali zaidi kwa kila mtu anayehusika.
“Tutaendelea kufanya kila tuwezalo kumaliza ubaguzi ndani ya michezo, lakini tunasihi serikali ichukue hatua za haraka na kuleta sheria inayofaa ili unyanyasaji huu uwe na adhabu za kudumu kimaisha kwa wahusika.
“Makampuni ya mitandao ya kijamii yanahitaji kuchukua hatua na kuwajibika kwa kuwapiga marufuku wanyanyasaji kutoka kwa majukwaa yao, kukusanya ushahidi ambao unaweza kusababisha kushtakiwa na kusaidia kufanya majukwaa yao kutotumiwa kwa dhuluma hizi,” amesema.