Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA
MAJANGILI 1,726 wa kesi za uhujumu uchumi  wamekamatwa na kikosi kazi maalumu kilichoundwa   mwaka mmoja uliopita katika hifadhi mbalimbali za taifa.
Pia kesi 2,625 zimesikilizwa katika mahakama mbalimbali na kutolewa hukumu na watuhumiwa kuhukumiwa kwenda jela.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema hayo ni miongoni mwa mafanikio makubwa ndani ya mwaka mmoja yaliyofanywa na wizara yake  baada ya kuunda kikosi kazi maalumu cha kudhibiti ujangili.
Alisema katika kesi hizo, watuhumiwa wengi   wamefungwa kati ya miaka 10 hadi 30, ikiwamo kulipa faini  za Sh milioni 452.
Alisema mbali na majangili hao kukamatwa ndani ya hifadhi za taifa na mapori ya akiba, kuna vitendea kazi vyao walivyokamatwa navyo.
Alivitaja kuwa ni bunduki, risasi, magunia ya mkaa, mbao, magogo, baiskeli, pikipiki, magari, mitumbwi na ng’ombe 88,435 ambao walikutwa ndani ya hifadhi kinyume cha sheria.
Alisema baadhi ya vitu hivyo  vimerejeshwa kwa wananchi kutokana na kutokuwa na kesi wakati vinavyohusika vinaendelea kushikiliwa.
Waziri alisema ndani ya kipindi hicho, mafanikio makubwa yamepatikana kutokana na vifo vya tembo  kupungua hadi kufikia asilimia 45, tofauti na ilivyokuwa mwaka  jana.
“Kwa kweli tuna haki ya kujivunia hili, vifo vya tembo 84 ambavyo vilitokea kwa sababu mbalimbali sasa  vimepungua,” alisema Maghembe.
Akizungumzia biashara ya utalii, alisema mwaka 2015/16 kulikuwa na   watalii 1,137,182 na mwaka 2016 wameongezeka hadi kufikia 1,284,279.
Alisema ndani ya kipindi hicho, mapato ya jumla yaliyopatikana ni Sh bilion 101.1 jambo ambalo ni mafanikio makubwa ndani ya wizara hiyo.