KHARTOUM, Sudan
WAZIRI Abdullah Hamduk, ambaye aliteuliwa juzi kushika wadhifa wa Waziri wa Fedha katika Serikali mpya ya nchi hii, anaripotiwa kukataa uteuzi huo.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la nchi hii, SUNA,  Hamduk ambaye ni Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa katika Idara inayoshughulikia masuala ya uchumi kwa Afrika, alikataa uteuzi huo juzi na hivyo kumlazimu Rais  Omar al-Bashir kukabidhi jukumu hilo kwa Waziri wake Mkuu, Moataz Moussa Abdullah, kusimamia masuala hayo ya fedha.
Rais Bashir alitangaza bara hilo la mawaziri mapema wiki iliyopita na huku akisema kwamba ameamua kulipunguza ili kubana matumizi ya Serikali na kukabiliana na mfumuko wa bei na kupunguza pia uhaba wa fedha.
Kwa muda mrefu Serikali ya Khartoum imekuwa ikijaribu kupunguza matumizi kama njia ya kukabiliana na mfumuko wa bei ambao umekuwa ukipanda kwa asilimia 64 kila mwaka na Julai mwaka huu ikajikuta inakumbwa na uhaba wa  fedha ambao umesababisha ugumu katika upatikanaji wa  mafuta na mkate.
Mwezi uliopita Chama tawala cha Rais Bashir kilisema kina mpango wa kuchagua utawala wa muda mrefu katika uchaguzi wa 2020 hatua ambayo itahitaji mabadiliko ya katiba.