KAMPALA, UGANDAÂ
POLISI nchini Uganda wana haki ya kuua kwa kupiga risasi ikiwa kiwango fulani cha ghasia kitafikiwa, Waziri wa Usalama Elly Tumwine amesema.
Makabiliano kati ya polisi na waandamanaji yalisababishwa na hatua ya kukamatwa kwa mgombea urais wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine yalisababisha vifo vya watu 37 tangu Jumatano wiki hii.
Alishtakiwa kwa kukiuka kanuni za afya za kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona katika mkutano wa kampeni.
Makundi ya kutetea haki za binadamu yanasema hatua ya kukamatwa na kushitakiwa kwa Bobi wine ni kisingizio cha kukandamiza upinzani kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi Januari.
Mwanamuziki huyo ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, ni miongoni mwa wagombea 11 wanaopinga rais Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani tango mwaka 1986.
Bobi Wine aliachiwa kwa dhamana siku ya Ijumaa baada ya kufikishwa mahakamani.
Kukamatwa kwake kulizua maandamano ya vurugu miongoni mwa wafuasi wake.
Kundi la vijana lilifunga barabara na kuchoma tairi za magari katika ya mji mkuu wa Kampala, na miji mingine nchini Uganda.
Vikosi vya usalama vilijibu kwa kurusha vitoa machozi na kutumia risasi halisi kuwatawanya watu.
Akiashiria kuwa maofisa 11 wa usalama walijeruhiwa Tumwine aliwaambia wanahabari kuwa “polisi wana haki ya kukupiga risasi na kukuua ukifikia kiwango fulani cha ghasia”.
“Wataka nirudie? Polisi wana haki ya kukupiga risasi na kukuua na utakufa bure…. usiseme hukuambiwa .”
Katika taarifa yake, polisi ilisema ni watu 28 waliofariki katika maandamano ya siku ya Jumatano na Alhamisi, lakini shirika la habari AP limemnukuu mchunguzi wa maiti wa polisi na mkuu wa huduma za afya za polisi kwamba walihesabu miili 37 Alhamisi asubuhi.
Mnamo mwezi Juni Bobi Wine aliapa kukiuka marufuku ya mikutano ya kampeni wakati wa janga la corona. Alimshtumu Rais Museveni kwa “kuogopa watu”.
Msemaji wa serikali ya Uganda Don Wanyama ameiambia BBC kuwa maofisa “hawengeweza kutualia na kuangalia ghasia zikifanyika “.
Pia amesema Rais Museveni “ametii marufuku iliyowekwa na Tume ya Uchaguzi na Wizara ya Afya”.
Human Rights Watch linasema ni wazi kwamba mamlaka za Uganda zinatumia mwongozo wa kuzuia Covid-19 kukandamiza upinzani na kuongeza kuwa chama tawala kimefanya kampeni kubwa.
Hizi ni vurugu mbaya kuwahi kutokea mitaani nchini Uganda tangu Bobi Wine alipochaguliwa kuwa mgombea wa nafasi ya urais.
Alhamisi asubuhi, BBC ilishuhudia maofisa wa usalama wakiingia kwenye maduka makubwa katikati ya jiji la Kampala na kuwatoa watu nje, au kufyatua mabomu ya machozi ili kuwafurumusha nje.
Wafanyabiashara na wateja wao walikuwa wakitoka nje wakiwa wamenyoosha mikono juu.
Vurugu nyingi zinarekodiwa na Waganda wa kawaida na kuchapishwa kwenye mitandao ya kijamii.
Waganda wameelezea hasira na mshtuko kwa kiwango cha nguvu inayotumiwa na polisi – na kwa maisha yaliyopotea.
Upinzani unasema utekelezaji wa vizuizi vya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona unatumika kwa kubagua.
Rais wa sasa Yoweri Museveni ameendelea kufanya kampeni bila kukatizwa – wakati hajahutubia umati, wafuasi wake wamekuwa wakikusanyika kumkaribisha katika miji mbalimbali.
Bobi Wine anayemtikisa ni nyota wa muziki wa mtindo wa Afrobeats aliingia katika taaluma ya muziki katika miaka ya 2000.
Anaelezea kipaji chake kuwa ni cha kuelimisha na kuburudisha. Mojawapo ya vibao vyake vya awali Kadingo, inahusu usafi wa mwili.
Jina lake rasmi Wine, ni Robert Kyagulanyi Ssentamu, alichaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi mdogo baada ya kusimama kama mgombea huru mwaka jana wilayani Kyadondo mashariki, Uganda ya kati.
Aliwashinda wagombea kutoka chama tawala National Resistance Movement (NRM) na chama kikuu cha upinzani Democratic Change (FDC).
Baada ya kutangazwa mshindi, aliahidi kuangazia zaidi kuwaunganisha raia.
“Jambo langu la kwanza ninalotaka kufanya ni kufanikisha maridhiano kati ya viongozi wa Kyadondo Mashariki…Ninataka siasa zitulete pamoja… jinsi muziki ufanyavyo.”