Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ameitaka Bodi mpya ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), aliyoizindua Dar es Salaam jana, kushughulikia kwa ukamilifu changamoto ndani ya tume hiyo.
Profesa Ndalichako alisema amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kuhusiana na vyuo wanavyosoma, jambo ambalo anaamini kama likifanyiwa kazi vizuri malalamiko yatakwisha.
“Tunaelewa wanafunzi ni watu wa kulalamika kila wakati, yapo malalamiko ambayo yana tija lazima yatatuliwe.
“Kwa mfano malalamiko yanayohusu uvurugaji wa matokeo au taratibu zinazowakandamiza kutoka kwa walimu wa vyuo vikuu,”alisema.
Akitoa mfano wa taratibu kandamizi katika vyuo hivyo, Profesa Ndalichako alisema mwanafunzi anapopoteza kitabu cha chuo hulipishwa mara tatu ya gharama huku akiwa ni mtoto wa masikini, hali inayosababisha washindwe kuazima vitabu wakihofia kulipishwa gharama kubwa.
Alisema kuna baadhi ya vyuo vimekuwa vikiwataka walimu kutoa taarifa ya kuacha kazi miezi mitano kabla ya kuacha kazi.
Waziri alisema sheria mama inamtaka mwajiriwa kutoa taarifa ya kuacha kazi kwa mwajiri miezi mitatu kabla ya kuacha kazi.
Pia alisema amepokea malalamiko kutoka kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ifakara mkoani Morogoro, Mei mwaka huu juu ya walimu wa chuo hicho kuvuruga matokeo yao.
Aliitaka TCU kufanya utafiti wa wanafunzi walioko vyuoni kubaini wanafunzi wasio na sifa kutokana na baadhi ya vyuo kuingiza wanafunzi kinyemela bila kupitia TCU au Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE).
Bodi hiyo itakayodumu kazi kwa miaka mitatu inaongozwa na Mwenyekiti, Profesa Philip Mtabaji.