Na MWANDISHI WETU-PWANI
WAZIRI wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, amepongeza jitihada zinazofanywa na mwekezaji wa Kampuni ya TwyFord Tanzania Cereramics kwa ujenzi wa kiwanda cha kutengeneza vigae katika Kijiji cha Pingo, Chalinze mkoani Pwani.
Akizungumza juzi baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya awali ya eneo litakalojengwa kiwanda hicho cha kutengeneza vigae ‘tiles’, alisema pindi kitakapokamilika kitatoa ajira kwa Watanzania zaidi ya 2,000 katika mfumo rasmi, 4,000 zisizo rasmi.
“Bidhaa hizi za vigae zitauzwa katika nchi majirani kama Zambia, Malawi, DRC, Rwanda, Burundi, Uganda na Jamhuri ya Watu wa Afrika Kati na kusafirishwa nje ya Bara la Afrika,” alisema Mwijage.
Kwa upande wake Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM), alisema ujenzi wa kiwanda hicho kipo katika hatua ya mwanzo na unatarajiwa kukamilika kati ya Julai na Agosti, mwaka huu.
Alisema kiwanda hicho kitasaidia kufungua mji wa Chalinze na kufanya mji wa viwanda na biashara na hivyo kufungua fursa za kiuchumi na kupanua mji huo katika sekta ya viwanda inayosimamia vyema na Serikali ya Awamu ya Tano.
“Ujenzi wa kiwanda hiki ni alama chanya ya jinsi Serikali ya Awamu ya Tano ilivyojizatiti kufungua fursa za viwanda katika nchi yetu. Wananchi wa Chalinze na Pwani wameaswa kuendelea kujipanga kwa viwanda na fursa nyingi zaidi,” alisema Ridhiwani.