NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Harrison Mwakyembe, ameibuka na kusema hajawahi kumshambulia kwenye mitandao Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kuhusu sakata la Richmond.
Kauli hiyo ya Dk. Mwakyembe imekuja siku chache baada ya kusambazwa kwa waraka unaodaiwa kuandikwa naye, ukimuhusisha na tuhuma za kumshambulia Lowassa, jambo ambalo amelifananisha kuwa ni sawa na siasa za kitoto.
Akizungumza jana katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na kituo cha redio Clouds FM, alisema kutokana na kusambazwa kwa waraka ambao umeandikwa nyadhifa zake za ubunge na uwaziri, hivi sasa ameshaanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya watu waliokuwa wakiusambaza.
Waziri Mwakyembe ambaye kitaaluma ni mwanasheria na mwanahabari, alisema anapata shaka hata na baadhi ya vyombo vya habari pamoja na mitandao hiyo na kudai kuwa anamshambulia Lowassa.
“Ninashangazwa sana na hii mitandao ya kijamii na baadhi ya vyombo vya habari (magazeti), vimekuwa vikiandika vitu vibaya ikiwa ni pamoja na kumshambulia Lowassa wakati hata siku moja sijazungumza nao.
“Kitendo cha baadhi ya watu wa aina hii kuwaandika vibaya wanasiasa katika mitandao ya kijamii kwa kutumia majina ya watu wengine ni ishara ya woga wa kisiasa na kushindwa kujiamini katika misimamo yao.
“…Kinachonikera kupindukia ni kuwa taarifa hizo sijawai kuziandika ila kuna mtu ama kundi maalumu la watu limeziandika na kuweka jina langu na nafasi zangu za uongozi kama mbunge na waziri, huu si uungwana na wala si siasa kwa kuchezea majina ya watu. Kama siasa zimefika huku basi ni za hatari,” alisema.
Dk. Mwakyembe ambaye pia ni Mbunge wa Kyela mkoani Mbeya, alisema katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, watu wanapaswa kuacha woga na kutojiamini.
“Kitendo cha kutumia majina ya watu na kuelezea hisia zao ni kukosa ujasiri na hata yanayosambazwa kwenye mitandao hayaendani na hadhi yangu kiongozi, sina tabia ya woga na uongo,” alisema.
Alisema baada ya kupata taarifa zilizopo mitandaoni alilazimika kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi Kitengo cha Makosa ya Mtandaoni pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili kulalalimikia mchezo huo mchafu.
Dk. Mwakyembe alisema vyombo hivyo vimeshaanza uchunguzi mkali ili kuwabaini watu walioandika na kutuma taarifa hizo.
“Hizo porojo zilianza tu polepole, zilienda mitandao ya kijamii na magazeti kuwa nimesema Lowassa hana sifa ya kuwa rais, wengine walisema niliwaambia nitapambana kufa na kupona Lowassa asiingie Ikulu wakati sijaongea nao na sijawahi kusema, huu ni mchezo wa kitoto uliopitiliza, lakini una madhara makubwa,” alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema kutokana na hali hiyo, amedhamiria na kuhakikisha kesi ya kwanza ya matumizi mabaya ya mitandao inaanzia kwake kwa kuwa hana utamaduni wa woga, na watu wanapaswa kuwa wazi endapo wanakuwa na vitu na si kutumia majina ya watu.
Dk. Mwakyembe alisema anashangazwa na watu kutumia jina lake kumchafua kwa kuwa hana tatizo na mtu yeyote na kama chanzo ni suala la Richmond, ilikuwa ni kazi aliyopewa na Bunge.
Alisisitiza kuwa alifanya kazi hiyo vizuri kwa kumuweka Mungu mbele, lakini si kuongea uongo jambo ambalo si utamaduni wake.
“Wananchi wanapaswa kutambua kuwa nchi inaendeshwa kisheria na ninaamini wahusika wote waliofanya tukio hilo watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema.
MTANZANIA ilimpomtafuta Meneja Mawasiliano wa TCRA, Innocent Mungy kupata ufafanuzi wa suala hilo, alisema kwa sasa jambo hilo linashughulikiwa na vyombo husika likiwemo jeshi la Polisi.