29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mwakyembe alipuliwa ununuzi wa mabehewa TRL

mwakyembe jpgElias Msuya, Dodoma

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe jana alilazimika kukanusha madai ya kutumia Sh bilioni 238 kununua mabehewa mabovu kwa Shirika la Reli Tanzania (TRL) alipokuwa Waziri wa Uchukuzi wakati wa utawala wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Dk. Mwakyembe alilazimika kukanusha madai hayo baada ya Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Jesca Kishoa kutaka ripoti ya ununuzi wa mabehewa mabovu kwa TRL.

Madai hayo yalimfanya Waziri Mwakyembe kuomba kutoa taarifa kwa kutumia Kanuni ya 63(3) akisema yuko tayari kujiuzulu hata ubunge kama itathibitika kweli kuwa alinunua mabehewa kwa fedha hizo.
Dk. Mwakyembe alisema Serikali haikutumia zaidi ya Sh bilioni 60 kwa ununuzi wa mabehewa hayo.

“Serikali haijawahi kutumia zaidi ya Sh bilioni 60 kununua mabehewa, mheshimiwa mbunge alete ushahidi, mimi niko tayari kujiuzulu hata ubunge kama itathibitika zimetumika fedha hizo. Msilifanye Bunge kuwa kijiwe cha siasa,” alisema Dk. Mwakyembe.

Hata hivyo, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee naye aliomba mwongozo akisema kanuni ya 63(3) aliyotumia Waziri Mwakyembe haikuwa sahihi bali atumie 63(4) inayomtaka atoe kwanza ushahidi wa kukanusha kwake.

“Waziri Mwakyembe angetumia kanuni ya 63(4) inayomtaka kwanza athibitishe anapokanusha jambo lolote ili aliyetoa madai naye atoe uthibitisho,” alisema Mdee.

Kauli ya Mdee ilimwinua tena Waziri Mwakyembe akimtaka Kishoa kutoa uthibitisho wa madai yake.
Naye Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu wa Bunge, Vijana na Ajira ambaye pia ni Mnadhimu mkuu wa wabunge wa CCM, Jenister Mhagama, alimtetea Waziri Mwakyembe akisema kuwa ameshathibitisha taarifa yake.

Hata hivyo, Mdee na Kishoa waliendelea kumtaka waziri Mwakyembe awasilishe taarifa ya ununuzi wa mabehewa hayo kwa ukamilifu badala ya taarifa ya mdomo.

Mwenyekiti wa Bunge, Dk. Mary Mwanjelwa alimpa siku tatu Kishoa kuwasilisha ushahidi wa madai yake.
Akitoa maoni ya kambi rasmi ya upinzani kuhusu mapendekezo ya mpango wa taifa unaokusudiwa kutekelezwa na serikali pamoja na mwongozo wa kuandaa mpango wa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/2017, Mbunge wa Momba, David Silinde alisema serikali imekuwa na mipango mingi na vipaumbele vingi ambavyo mwisho wake italeta changamoto katika utekelezaji.

“Hoja ya Kambi Rasmi ya Upinzani ilitokana na msingi kuwa tayari kulikuwa na mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini (MKUKUTA).

“Katika hali kushangaza baadaye serikali hiyo hiyo kabla ya miaka mitano kumalizika mwaka 3013 ikaja na mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN),” alisema Silinde.

Akizungumzia uchaguzi wa Zanzibar, alisema kufutwa kwa uchaguzi kumekiuka mchakato wa demokrasia.
“Yale yanayoendelea kwa upande wa pili wa Muungano (Zanzibar) ni ushahidi ulio wazi kuwa demokrasia ya haki ambayo ni kichocheo cha maendeleo kwa nchi, bado kwa nchi yetu ni kitendawili, na pia haki ya wananchi kutoa na kupata habari kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 18(b) na (c) ),” alisema Silinde.

Kuhusu mwenendo wa Bunge, Silinde alisema Bunge limeingia katika taharuki kwa polisi ambao hawakuvalia nguo rasmi za kuwa ndani ya ukumbi wakiingia na kufanya fujo na hilo ni kulidhalilisha Bunge katika sura ya kimataifa.

“Kwa wale wote ambao ni wabunge wapya na hawaelewi haki za “minority” katika Bunge ni kuwa na haki ya kuzuia hoja ili kufikiwa kwa uamuzi wenye mwafaka wa pamoja kwa hoja za Serikali na jambo hili kwa mila na tamaduni za bunge halitafsiriki kama fujo,” alisema Silinde.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles