Na MWANDISHI WETU-DODOMA
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameziagiza mamlaka ya serikali za mitaa, wizara na taasisi zote zitoe taarifa za ajira zinazozalishwa kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo kila robo mwaka.
Ametoa agizo hilo juzi bungeni, mjini Dodoma, wakati akitoa maelezo ya kuhitimisha majadiliano ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2017/2018.
Waziri Mkuu alikuwa akijibu hoja ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, ambaye aliitaka Serikali itoe maagizo kwa wakurugenzi wote wa halmashauri kutengeneza ajira angalau 20,000 kila mwaka katika miradi mbalimbali inayotekelezwa katika halmashauri zao, na taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo iwe inatolewa kila mwaka kwenye Bunge la Bajeti.
“Napenda, kumtaarifu Mheshimiwa Mbunge kuwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2015, Ibara ya 59 inazielekeza Mamlaka za Serikali za Mitaa zote nchini kuzingatia viashiria vya ukuzaji ajira katika mipango ya maendeleo ya ngazi husika pamoja na kutoa taarifa za mwenendo wa ajira kila robo mwaka,” alisema.
Waziri Mkuu alisema maelekezo hayo yanazingatiwa katika mwongozo wa kuandaa Bajeti ya Serikali unaotolewa na Hazina kila mwaka, ambao unazitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa, wizara na taasisi zote zibainishe fursa za ajira zinazotarajiwa kupatikana kila mwaka kutokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Vilevile mwongozo huo unazitaka taasisi hizo kutoa taarifa za ajira zinazozalishwa kutokana na utekelezaji wa miradi hiyo kila robo mwaka. Ninatoa agizo, Mamlaka ya Serikali za Mitaa, Wizara na taasisi zote ziendelee kuzingatia maelekezo haya,” alisema.
Akizungumzia kuhusu ujenzi wa viwanda, Waziri Mkuu alisema ndani ya mwaka mmoja, jumla ya viwanda 2,169 vimesajiliwa, vikiwamo viwanda vya mbolea, saruji, chuma na vya usindikaji wa mazao.
“Serikali pia inaendelea kuhamasisha ujenzi wa viwanda na kuvutia uwekezaji nchini. Uhamasishaji wa ujenzi wa viwanda nchini ni dhahiri na tayari tumeanza kuona matokeo. Kwa mfano, Mkoa wa Pwani peke yake una viwanda vikubwa 83 na vingine vidogo vidogo zaidi ya 200.
Huu ndio mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Tano,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, alisema Programu ya Miundombinu ya Masoko, Uongezaji Thamani na Huduma za Fedha Vijijini (MIVARF) ilipanga kukarabati barabara zenye jumla ya kilomita 148.5, kujenga masoko manne na kukarabati kituo kimoja cha mafunzo ya utunzaji mazao baada ya kuvuna.
Akijibu hoja za utekelezaji wa programu hiyo kwa upande wa Pemba na Unguja, Waziri Mhagama alisema miradi ya ujenzi na ukarabati wa barabara ilianza Agosti na Novemba 2014 na kazi hiyo kwa Pemba ilikamilika Desemba 2015, wakati kwa upande wa Unguja ilikamilika Januari 2016.
“Kazi za ujenzi wa masoko ya Kinyasini na Mombasa (Unguja) pamoja na Konde na Tibirinzi (Pemba) zilianza Desemba 2016 na zinatarajiwa kukamilika Julai 2017. Wakandarasi wamehimizwa kuhakikisha wanakamilisha kazi hizo katika muda uliopangwa ili kuendana na ratiba iliyopangwa,” alisema Jenista.