CHRISTCHURCH, NEW ZEALAND
TAKRIBANI watu 10,000 nchini New Zealand, juzi waliungana na waziri mkuu wa nchi hiyo, Jacinta Aredern katika sala ya maombolezo ya wahanga wa shambulizi la kigaidi katika misikiti lililotokea jijini Christchurch nchini humo.
Maelfu ya waumini wa dini ya Kiislamu na wale wasiokuwa waumini wa dini hiyo walikusanyika katika swala ya pamoja iliyofanyika viwanja vya Hagley vilivyopo karibu na Msikiti wa Al Noor ambapo waumini waliuawa katika shambulizi la kigaidi lililotekelezwa wiki iliyopita na Brenton Harrison Tarrant lilisababisha vifo vya watu 50 na wengine zaidi ya 42 walijeruhiwa vibaya pamoja na kusababisha vilio vya 100 ambao hawakuwa na uwezo wa kujitetea.
Jeshi la Polisi nchini New Zealand lilimtaja aliyehusika na shambulizi hilo kuwa Brenton Tarrant mwenye umri wa miaka 28 mzaliwa eneo la Grafton nchini Australia, ambaye anaonekana kwenye video iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa alitumia dakika 17 wakati gaidi huyo akifanya shambulizi na kuonesha moja kwa moja kupitia akaunti yake ya mtandao wa Facebook.
Waziri mkuu wa New Zealand, Jacinda Ardern akiwa amevalia hijabu yenye rangi nyeusi kuonesha mshikamano na wananchi wake wenye imani ya Kiisalamu, alizungumza kwa hisia kali katika hotuba yake aliyotoa kwa wananchi hao.
“New Zealand imejeruhiwa, tumeonesha mshikamano katika jambo hili kuwa sisi ni wamoja,” alisema Jacinta.
Imam Gamal Fouda aliongoza swala hiyo viwanjani hapo, ikiwa ni ishara ya kuwaombea wahanga 50 waliouawa katika shambulizi hilo.
Zaed Moustafa, ambaye amempoteza baba na kaka yake katika tukio hilo la ugaidi, alikuwa miongoni mwa watu waliojitokeza kwenye maombolezo hayo, sambamba na bondia wa Australia ambaye amejiunga na imani ya Kiislamu, Anthony Mundine.
Katika mahubiri yake Imam Gamal Fouda alisema, “Wiki iliyopita tuliona chuki na hasira machoni mwa gaidi ambaye aliwaua ndugu zetu 50 na kuwajeruhi wengine 42, ameumiza mioyo ya mamilioni ya watu. Leo (juzi) katika eneo lilelile, tunaliangalia kwa upendo, hisia na imani machoni mwetu, na kuona huzuni ya maelfu ya wananchi waliojeruhiwa na tukio hilo mioyoni na hisia zao, wanaonesha uungwana na ubinadamu wao. Wapendwa wetu wametuachia huzuni, wamekufa kifo cha maumivu. Damu zao ziwe mbegu ya matumaini na upendo miongoni mwetu,”
Katika swala hiyo viongozi mbalimbali wa serikali na bunge walihudhuria, wakiwemo waziri mkuu, spika wa bunge, pamoja na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama na dini akiwamo Mustafa Faouk wa Umoja wa Waislamu wa New Zealand.
Maombolezo hayo yalifanyika baada ya awali kuwakutanisha watu 15,000 waliokusanyika kwenye uwanja wa mchezo wa Rugby katika eneo la Dunedin nchini humo kwa nia ya kuwaombea wahanga wa tukio la ugaidi.
Kamishna wa Jeshi la Polisi, Mike Bush amesema wahanga wa tukio hilo wametambuliwa, pamoja na takribani miili 25 ya watu wamezikwa katika Makaburi ya Makumbusho.