29.9 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

WAZIRI MKUU AWAJIA JUU WATENDAJI MASHIRIKA YA UMMA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amewajia juu baadhi ya watendaji wa mashirika ya umma na kusema wamekuwa chanzo cha mashirika wanayoyaongoza kutofanya vizuri.

Waziri Mkuu aliyafananisha mashirika hayo sawa na boya lililowekwa kwenye chombo baharini na kuzuiwa kisizame ama kutembea huku akitaka mwongozo upatikane wa namna ya uteuzi wa wajumbe wa bodi hizo.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini Dar es Salaama  kwenye mkutano wa watendaji wakuu wa mashirika ya umma wakiwemo wajumbe wa bodi mbalimbali, ambapo alisema baadhi ya watendaji wa mashirika hayo wanachofanya ni kuhakikisha mashirika hayafi lakini kila mwaka yako vilevile.

Mkutano ho ulioandaliwa na taasisi ya uongozi ulilenga kujadili nafasi ya mashirika ya umma katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano (2016/17 – 2020/21).

“Ni sawa tu na kuku aliyeatamia mayai bila kuyatotoa kila mwaka yako vilevile. Matamanio ya serikali ni kuona mayai yanatotolewa ili tupate vifaranga vingi zaidi vitakavyoendeleza uzao wa mama kuku. Tujitathmini sisi wenyewe na kubadilisha utendaji kazi katika mashirika yetu ya umma.

“Mashirika ya umma ya wenzetu yameweza kufungua makampuni tanzu mengi yaliyoweza kuvuka mipaka ya nchi zao, hata sisi tunaweza. Lakini je, tunaweza kuvuka kwa namna tulivyo sasa?,” alihoji Majaliwa.

Alisema urasimu umekithiri katika mashirika mengi na mengine yamekuwa yakiingia mikataba isiyokuwa na tija na kuisababishia hasara serikali.

Pia alisema zana kwamba mashirika ya umma hayawezi kufanya biashara ama yakifanya yanapata hasara ni potofu na kwamba hali ya sasa ni tofauti na miaka ya nyuma.

Kwa mujibu wa Majaliwa, moja ya sababu kubwa ya mashirika mengi kupata hasara na kushindwa kujiendesha katika miaka ya nyuma ilitokana na kutokuwa na menejimenti nzuri na wataalamu wa kuyaendesha.

Alitoa mfano wa Shirika la Ndege la Ethiopia ambalo ni la umma kwamba limekuwa likiendeshwa kwa faida kwa asilimia 100 licha ya hali ngumu kwenye biashara ya usafiri wa anga.

“Fikirieni kama nusu ya mashirika yetu yangefikia nusu ya faida ambayo Ethiopia wanapata. Mkurugenzi wa ATCL tunataka ulipaishe tupate faida kubwa. Uwezo unao, timu unayo, ndege unazo na nyingine tunakuletea.

“Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ambalo lilikuwa linaendeshwa kwa hasara leo hii lina miradi mingi na yenye tija kubwa. TRL lilishakufa halikuwa na matumaini lakini leo hii tumeanza kuona matarajio. Mabadiliko hayakuletwa na mshauri mwelekezi kutoka nje ya nchi bali ubunifu na kutumia wataalamu waliobobea katika fani zao,” alisema.

Waziri Mkuu alisema serikali inamiliki mashirika 264 ambapo kati yake 65 ni ya kibiashara na 187 ni ya huduma wakati 12 ni ya udhibiti.

Alisema kati ya mashirika 65 ya kibiashara, manane yanaendeshwa kwa ruzuku ya serikali na 57 hayategemei ruzuku.

Waziri Mkuu aliagiza mfumo wa kuwapata wajumbe wa bodi za mashirika ya umma uangaliwe upya ili kuwe na tija na ufanisi katika uendeshaji wa mashirika hayo.

“Wananchi wanalalamika je, kuna mwongozo wa kupata wajumbe wa bodi? Kama upo unafuatwa? Kama haupo je, si wakati mwafaka wa kuwa na mwongozo rasmi?

“Tujiulize je, muundo, rasilimali na teknolojia Ofisi ya Msajili wa Hazina ina uwezo wa kutosha wa kusimamia mashirika yetu yote kwa ufanisi? Tunatarajia mkutano huu utakuja na majibu,” alisema Majaliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles