26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

HISA ZA VODACOM SOKONI RASMI

Joseph Lino na Patricia Kimeremeta – dar es salaam


BAADA ya Serikali kuzitaka kampuni za simu kujisajili katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE), Kampuni ya Vodacom imekuwa ya kwanza kukidhi vigezo na sasa muda wowote kati ya leo hadi Machi 4, itasajili asilimia 25 ya hisa zake ili watu waanze kuzinunua.

 Hatua hiyo inakuja baada ya Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), kuiidhinishia kampuni hiyo kuendelea na usajili huo na kwamba takribani hisa milioni 560 zenye thamani ya Sh bilioni 467 zitauzwa kila moja kwa Sh 850.

Kwa mujibu wa taarifa za ndani kutoka Vodacom na CMSA, soko hilo linatarajiwa kufunguliwa kwa wiki sita.

Kwamba Aprili 21 litafungwa na siku ya mauziano inatarajiwa kuwa Mei 9 kwa kulinganisha bei ya Sh. 850 na thamani ya ukubwa wa kampuni ya Vodacom kwa upande wa mapato yake.

Kampuni ya Vodacom inamiliki asilimia kubwa ya soko la mawasiliano ikiwa pia kampuni kubwa katika mapato na ulipaji wa kodi. 

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Vodocom ndio kampuni kubwa zaidi katika soko la huduma za mawasiliano kwa simu za kiganjani kati ya kampuni saba, ikiwa na wateja milioni 12.06.

Kampuni za Tigo na Airtel zinamiliki asilimia 29 na 26 ya soko. Tigo ina wateja milioni 11.6, huku Airtel ikiwa na wateja milioni 10.3.

Aidha, Kampuni ya Halotel ambayo ilianza huduma zake mwaka jana, imefikisha wateja milioni 2.7, Zantel inahudumia wateja milioni 1.4, Smart 881,756 na TTCL 304,058.

Vodacom inaingia DSE wakati ambao biashara katika soko hilo imekuwa ikipanda na kushuka kwa siku za karibuni.

Februari 13, mwaka huu DSE ilitangaza mauzo yake ambayo yalikuwa yameshuka kwa asilimia 84 kutoka Sh trilioni 2.5 hadi Sh milioni 406, huku idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa ikipungua kutoka 868,000 hadi 262,000.

Juzi ilitangaza tena mauzo yake, yakaonyesha yameongezeka hadi kufikia Sh bilioni 8.6 sawa na asilimia 3771.

Ilisema kuongezeka kwa mauzo hayo kumechangiwa na kuongezeka kwa idadi ya hisa zilizouzwa na kununuliwa kutoka 257,000 hadi milioni 1.2.

Miongoni mwa kampuni zilizoongoza kwa kuwa na hisa nyingi zilizouzwa na kununuliwa ni TBL kwa asilimia 98.5 ikifuatiwa na Benki ya CRDB.

Meneja Masoko na Mauzo wa DSE, Patrick Mususa, alisema ukubwa wa mtaji wa kampuni zilizoorodheshwa katika soko umepanda kwa takribani Sh bilioni 100, kutoka Sh trilioni 20.0 wiki iliyopita hadi Sh trilioni 20.1 wiki hii ikichangiwa na ongezeko la bei za hisa za Kenya Airways kwa asilimia 18.2, TBL kwa asilimia 12.7 na JHL kwa asilimia 3.8.

“Mtaji wa kampuni za ndani pia umepanda kutoka Sh trilioni 7.1 hadi Sh trilioni 7.4, hii ni kutokana na ongezeko la bei za hisa za TBL kwa asilimia 12.7,” alisema Mususa.

Kwa upande wa viashiria vya soko, kiashiria cha kampuni zilizoorodheshwa katika soko, kimepanda kwa pointi 14 kutoka pointi 2,294 hadi 2,308 kutokana na ongezeko la bei za hisa za kampuni mbalimbali zilizopo sokoni.

Mwaka jana Serikali ilitoa agizo kwa kampuni za simu kuweka hisa katika soko la hisa kupitia sheria iliyopitishwa na Bunge mwezi Juni mwaka jana inayolenga kuwasaidia wananchi kumiliki sehemu ya kampuni zinazokua kwa kasi zaidi barani Afrika.

Mawasiliano ni moja ya sekta zinazofanya vizuri nchini huku inazidi kukua kwa kasi.

 

WASOMI WAZUNGUMZA

Baadhi ya wachumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamepongeza uamuzi huo kwa madai kuwa utawasaidia Watanzania kumiliki makampuni makubwa yakiwamo ya simu ambayo awali yalikuwa yanamilikiwa na wageni, huku faida inayopatikana ikienda nje ya nchi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Dar es Salaam jana, wachumi hao walisema kuwa kampuni za simu zinawekezwa kwa mtaji mkubwa jambo ambalo lilichangia Watanzania kuogopa kuwekeza kwa madai kuwa wanaweza kushindwa kwenye soko.

 “Uamuzi wa Serikali wa kuzitaka kampuni za simu za mkononi kuuza hisa zake ili ziweze kumilikiwa na wazawa, utasaidia kupata faida kutokana na gawio litakalopatikana ambapo fedha zote zitabaki nchini,” alisema Profesa Hajji Semboja.

Aliongeza kuwa pia Watanzania wataweza kupata elimu ya uwekezaji na kujijengea uzoefu wa kushiriki kwenye soko la mitaji mikubwa, ikiwamo ya kumiliki hisa za makampuni makubwa.

Alisema kutokana na hali hiyo, mkakati wa uuzaji hisa wa makampuni hayo unapaswa kwenda na makampuni mengine makubwa yakiwamo ya mafuta na gesi ili Watanzania waweze kupata fursa ya kumiliki hisa zake, jambo ambalo linaweza kukuza uchumi.

Profesa Semboja alisema kuwa jambo la kupongeza kwa Serikali ya awamu ya tano ni pamoja na uamuzi wake wa kuahidi kuuzwa kwa hisa za makampuni hayo na kutekeleza kwa vitendo.

Naye Mhadhiri Mwandamizi wa uchumi kutoka UDSM, Dk. Jehovannes Aikaeli, aliwataka wananchi kujitokeza kununua hisa za kampuni hiyo kwa sababu zitawasaidia kujijengea uwezo wa kumiliki hisa za makampuni makubwa.

“Uuzaji wa hisa za makampuni haya utasaidia Watanzania kumiliki makampuni makubwa ya simu ambayo awali yalikuwa yanamilikiwa na wageni,” alisema Dk. Aikaeli.

Aliongeza kuwa kwa sasa ni lazima kwa makampuni hayo kufanya hivyo kusaidia kukuza uchumi ili kuondoka kwenye umasikini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles