23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu asisitiza ulinzi kwa Watoto wote

*Asema wasiojali malezi ya watoto, wachukuliwe hatua

*Achagiza kauli ya “Mtoto wa mwenzio ni wako”

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kusimamia ulinzi wa watoto na kupinga ukatili dhidi yao huku akisisitiza kwamba ni lazima kila mtoto wa Kitanzania alindwe na atunzwe.

“Lazima mtoto wa Kitanzania alindwe, atunzwe. Mtoto wa mwenzio ni wako. Kama kuna Mtanzania yoyote anatenda ukatili na hamtunzi mtoto, lazima achukuliwe hatua za kisheria. Kwenda shule ni lazima kwa mtoto wa Kitanzania. Asipoenda shule, ukamtuma kuuza maandazi stendi, tukimkamata tutakushtaki wewe mzazi au mlezi,” amesisitiza.

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha picha ya Rais Samia Suluhu Hassan iliyochorwa  na mtoto Rashidi Mahabad katika Maadhimisho ya Miaka 75 ya Shirika la Kuwahudumia Watoto la Umopja wa Mataifa (UNICEF) kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Desemba 4, 2021. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu).

Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Desemba 4, 2021) wakati akizungumza na wadau mbalimbali walioshiriki maadhimisho ya miaka 75 ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Watoto (UNICEF) kwenye ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo, amesema wiki iliyopita wakati akizindua maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia alisisitiza haja ya kila mtoto kupewa haki zake anazostahili. “Nilisema, lazima kila mtoto wa Kitanzania apate haki zake, asome hadi ukomo ili naye aweze kuwalea wengine kama alivyolelewa.”

Akizungumzia hoja zilizoibuliwa na watoto na vijana balehe kwenye mjadala uliokuwa mubashara katika mkutano huo, Waziri Mkuu amewapongeza vijana hao watano kutoka mikoa ya Dodoma, Mwanza, Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar kwa kuwasilisha kwa uwazi na ujasiri hoja hizo.

Hoja walizowasilisha ni kutaka Serikali iongeze bajeti kwenye ajira za walimu ili kukabiliana na upungufu uliopo; kuboresha miundombinu ya shule ikiwemo maji; kuboresha mitaala ya elimu ili iendane na soko la ajira; kuondolewa kwa adhabu ya viboko, kupatiwa taarifa sahihi za elimu ya afya na kupewa fursa ya kuonesha vipaji vyao na kutambuliwa.

Akifafanua hoja hizo, Waziri Mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imeshaanza kutekeleza baadhi ya mambo kama vile kuajiri walimu 6,900 (hadi Juni, 2021), kujenga maabara, kujenga mabweni ili watoto wanaokaa mbali na shule wasipate shida, kutoa sh. bilioni 20.5 kila mwezi za elimu msingi bila ada ili kuwawezesha vijana wasome bila usumbufu wa michango kwa wazazi na kuboresha miundombinu ya kujifunzia na ya kufundishia.

Kuhusu suala la kupata taarifa na huduma rafiki za afya ya uzazi kwa vijana, Waziri Mkuu amesisitiza wizara husika zihakikishe kuwa elimu sahihi yenye kuzingatia umri wa mtoto, mila na tamaduni zetu inatolewa katika ngazi zote.

Kuhusu suala la adhabu ya viboko shuleni na athari zake kwa watoto, Waziri Mkuu amesema jambo hilo linahitaji mjadala mpana utakaohusisha wadau wote kwa sababu lina changamoto  nyingi zikiwemo za mfumo wa malezi, maadili na tamaduni za makabila tofauti.

Kuhusu uibuaji na uendelezaji wa vipaji vya vijana, Waziri Mkuu amesema Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeanza kukusanya maoni kutoka kwa wadau ili kubaini ni aina gani ya elimu inatakiwa kwa kijana wa Kitanzania.

“Tumepanga tutoe stadi za ujuzi mbalimbali ili mwanafunzi akihitimu awe anaweza kujiari au kuajiri wenzake kulingana na yale aliyojifunza na asikae kusubiri ajira ya ofisini. Pia tumejenga VETA katika kila mkoa, bado tunakamilisha mikoa miwili mipya ya Simiyu na Songwe na sasa tutaenda kuwa na vyuo vya stadi katika kila wilaya.

“Huko watajifunza, upishi, uashi, ufundi makenika, ushonaji … nia yetu wapate umahiri katika ufundi stadi na Serikali itaongea na taasisi za fedha ili watoe mitaji kwa walio tayari kujiajiri,” amesema Majaliwa.

Mtoto mwenye kipaji cha kuimba Abby Chams akiimba katika Maadhimisho ya Miaka 75 ya Shirika la Kuwahudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete jijini Dodoma, Desemba 4, 2021. (Picha na ofisi ya Waziri Mkuu)

Mapema, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako alisema wizara yake imeshirikiana na UNICEF katika miradi mbalimbali ikiwemo Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Watoto Walioikosa (MEMKWA), Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK), Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana Walio nje ya Shule (IPOSA) na kuandaa Mwongozo wa Malezi, Unasihi na Ulinzi wa Watoto Mashuleni.

“MEMKWA imewanuifaisha vijana 4,372 waliopitia mpango huu na wengine wamefika hadi elimu ya juu. Mradi wa IPOSA unaotoa fursa mbadala kwa vijana balehe unatekelezwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Mbeya, Njombe, Tabora Songwe, Kigoma na Dodoma ambako vijana 9,930 wamepata mafunzo.

Naye Mwakilishi Mkazi wa UNICEF hapa nchini, Shalini Bahuguna alisema miaka 75 iliyopita, isingetarajiwa kwamba watoto wanaweza kukaa jukwaa moja na viongozi wakuu wa nchi na kutoa maoni lakini kwa sasa jambo hilo linawezekana.

Ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuwa miongoni mwa nchi za mwanzo kusaini Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Mtoto na akaomba viongozi waliopo madarakani wawasikilize watoto na kufanyia kazi maoni wanayoyatoa ili kuboresha maisha ya watoto na Tanzania kwa ujumla.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles