24 C
Dar es Salaam
Sunday, May 19, 2024

Contact us: [email protected]

Waziri Mkuu amekumbuka: Utawala wa sheria nguzo ya utawala bora

majaliwatulia1

KATIKA kuendesha nchi hasa katika nchi ya kidemokrasia, utawala wa sheria ni moja ya nguzo muhimu.Utawala wa sheria huwezesha Serikali kutimiza malengo yake ya kuleta maendeleo ya nchi kwa raia wa nchi husika. Katiba ndio  sheria kuu inayotoa mwongozo na maelekezo kwa watawala ikifuatiwa na sheria zinazotungwa kwa mujibu wa Katiba.

Pamoja na Katiba kuna misingi ya haki  ya asili ambayo huendana na jinsi sheria zinavyopaswa kutekelezwa.

Nchi yetu ina Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  ya mwaka 1977 na Katiba  hii pamoja na kuwa ina upungufu kadhaa ndio Katiba iliyopo na ndiyo inayopaswa kufuatwa. Zipo sheria nyingi mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na kila mmoja wetu hapa nchini.  Kuna wakati watu hukiuka sheria na kufanya matendo ambayo husemekana kuwa ni kujichukulia sheria mkononi. Lakini pia pamekuwapo na utaratibu wa viongozi mbalimbali nchini nao kuchukua sheria mkononi kwa maana ya kutenda au kutoa amri ambazo hazipo kwa mujibu wa sheria au hazizingatii sheria na haki walizonazo raia wa nchi hii.

Niliposikia kauli ya Waziri Mkuu aliyoitoa alipokuwa anazungumza na Wafanyakazi wa Chama Cha Wafanyakazi  Tanzania nilitafakari  kuhusu suala  zima la Utawala wa Sheria na Utawala bora. Utawala wa Sheria ni ule unaofuata sheria zilizopo na Utawala Bora ni ule unaozingatia sheria zilizopo pamoja na misingi ya haki za binadamu na haki za asili.

Waziri Mku alitahadharisha viongozi wenzake kwenye suala la kutumbua tumbua majipu yaani kuwaachisha kazi watu au kuwawajibisha wafanyakazi bila kufuata sheria zilizopo. Kauli hii niliifananisha na kauli aliyoitoa Makamu wa Rais,  Samia Suluhu Hassan naye alipotoa tahadhari ya aina hiyo hiyo. Kauli hizi hazikutolewa tu ni  kwa vile  kumekuwa na tabia ya viongozi mbalimbali kuchukua  sheria mkononi na kuwafukuza au kuwaadhibu watendaji walio chini yao bila utaratibu unaokubalika kisheria.

Wengi wetu  tutakumbuka suala la Mwalimu aiyelazimishwa kupiga deki kwa vile mkuu wa wilaya husika alikuta shule ikiwa chafu, Wapo watendaji kadhaa  wa Serikali ambao  wamewekwa ndani bila kufuata utaratibu unaostahiki kwa amri ya ama mkuu wa wilaya au mkuu wa mkoa. Wapo wengi waliosimamishwa na viongozi ambao si waajri wao na wasio na mamlaka ya kufanya hivyo.

Kila  mamlaka ina mipaka yake. Pale ambapo mtumishi wa umma amekosea katika utendaji wake wa kazi zipo sheria za kazi zinazoongoza jinsi mtendaji wa aina hiyo anavyopaswa kutendewa kwa mujibu wa sheria. Pia kuna haki za asili zinazoitaka mamlaka husika kufuata utaratibu wa kumsikiliza kabla ya kufanya chochote kwa mtumishi huyo.

Kawaida tukijaribu kutoa ufafanuzi huu wapo wanaodhani kuwa tunatetea wakosaji na hatutaki waadhibiwe. Hii si kweli mtu anapokosea na hasa makosa haya yanayokera sana ya wizi wa mali za umma ya ufisadi na kutojali kazi ni muhimu na ni sawa kabisa wachukuliwe hatua lakini kwa nchi yenye mfumo wa kisheria  lazima sheria hizo zifanye kazi na zifuatwe. Iwapo sheria zina matatizo basi na zirekebishwe.

Ukweli ni kwamba hali hii haijafuatwa sana katika Awamu hii ya Tano ya Serikali ya nchi yetu. Pamekuwa na matukio mengi yaliyoripotiwa  ambayo watumishi  wamesimamishwa au kuachishwa kazi kwa kauli tu ya kiongozi na mara nyingi papo kwa papo bila kutoa fursa ya utetezi  au hata maelezo. Wengine wameachishwa kazi  kiholela kiasi ambacho wakiamua kwenda mahakamani kudai haki hiyo huweza kuifanya serikali ilipe fidia kubwa sana. Jambo hili natumaini ndilo lililomsukuma Waziri Mkuu kutoa  tamko kwa watendaji walioko chini yake kuwa waache kuachisha watu kazi bila kufuata utaratibu.

Tamko hili limekuja kutoka kwa Waziri Mkuu  akiwa ndio mtendaji mkuu katika Serikali. Tunajua kabisa  Waziri Mkuu ameitazama hali halisi na kuona inavyoweza kuleta shida katika Serikali iwapo watendaji wanaotumbuliwa kiholela wanavyoweza kuishtaki Serikali. Waziri Mkuu ameitambua dhana ya Utawala wa Sheria na pia  ameona umuhimu wa kuijali dhana kuu ya Utawala Bora. Kutokana na kauli hii ya Waziri Mkuu  tunatarajia kuwa hali itabadilika na watumishi serikalini wanaofanya vitendo vya ubadhirifu wasiojali taamula zao na kazi walizopewa kufanya watachukuliwa hatua lakini kwa kufuata  utaratibu uliowekwa  katika maeneo husika.

Kwa kufuata utaratibu na sheria Serikali inajijengea heshima na wale wote waliokosea wanajua kabisa kuwa watatiwa hatiani kwa  kufuata utaratibu na pia mifumo ya kisheria nayo inabidi ifanye kazi na kwa wepesi ili haki itendeke kwa wakosaji na waliokosewa ambao ni umma wa Watanzania

Tunampongeza sana Waziri Mkuu kwa kukumbuka  umuhimu wa utawala wa sheria ambao ni msingi mkuu wa utawala bora

Imeandaliwa na Dkt.Helen KijoBisimba Mkurugenzi Mtendaji LHRC

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles