Na MWANDISHI WETU -LINDI
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameushukuru uongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Lindi kwa kutoa sehemu ya eneo lake na baadhi ya majengo kwa ujenzi wa shule.
Jimbo Katoliki la Lindi, limetoa eneo hilo lililopo katika Parokia ya Mnacho wilayani Ruangwa, ambalo awali ilikuwa Shule ya Msingi ya Mnacho ambayo sasa imebadilishwa na kuwa sekondari.
Waziri Mkuu alitoa shukurani jana, alipokwenda Kanisa Katoliki la Theresia wa Mtoto Yesu, Parokia ya Mnacho kuwasalimia waumini.
Alisema lengo la kuibadilisha shule hiyo kuwa Sekondari ya Wasichana ya Lucas Malia ni kuwawezesha watoto wa kike wa wilaya hiyo kusoma katika mazingira mazuri.
Waziri Mkuu ambaye ameambatana na mkewe Mary, alisema shule hiyo ya bweni itawapunguzia vishawishi watoto wa kike, hivyo kuwawezesha kutimiza malengo yao.
Awali uongozi wa parokia hiyo uliipongeza Serikali kwa kuboresha huduma za jamii zikiwemo za afya, elimu pamoja na miundombinu katika wilaya hiyo.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa aliwaomba viongozi wa dini washikamane na wahakikishe wanatatua changamoto ya mmomonyoko wa maadili.
Alisema changamoto ya mmomonyoko wa maadili katika jamii, hususani kwa vijana ni kubwa, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha kwamba wanawarejesha kwenye maadili bora.
Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Lucas Malia na alisema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi wake.
Shughuli zinazoendelea katika shule hiyo, ni pamoja na ujenzi wa mabweni, vyumba vya madarasa, maabara na nyumba nne za walimu ambazo tayari ujenzi wake umekamilika.