26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Tamko la vyama lamponza Rungwe, aitwa polisi

Na ASHA BANI

-DAR ES SALAAM

SAA chache baada ya kumaliza kutoa tamko la msimamo wa vyama nane vya siasa vya upinzani kuhusu wakurugenzi wa halmashauri kuendelea kusimamia uchaguzi mdogo, Mwenyekiti wa Chauma, Hashim Rungwe  ametakiwa kuripoti Kituo cha Polisi Oysterbay leo.

Polisi waliingia eneo la mkutano na kumkuta Rungwe akiwa na Mwenyekiti wa UPDP, Fahm Dovutwa na wanachana wengine.

 Ofisa mmoja wa polisi baada ya kujitambulisha, alimtaka Rungwe kuripoti polisi leo kwa maelekezo zaidi.

Awali katika mkutano wao na waandishi wa habari, Rungwe alisema Tume ya Uchaguzi (NEC) ilitangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo katika kata 32 utakaofanyika Juni 15, lakini walishangazwa na tangazo la wakurugenzi mbalimbali wa hamashauri nchini kuandika barua kwa vyama vya siasa juu ya mchakato wa kuchukua na kurudisha fomu hizo licha ya kuzuiwa na amri ya mahakama.

Akisoma tamko hilo, alisema wanatambua kuwa uchaguzi wa madiwani unasimamiwa na Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, licha ya kufanyika sambamba na Uchaguzi wa Rais na Wabunge ambao umekuwa ukifanyika chini ya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 1985.

“Na itakumbukwa mnamo Mei 10, mwaka huu, Mahakama Kuu ilitoa uamuzi wa kuvifuta vifungu vya sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambavyo vilikuwa vinawapatia mamlaka wakurugenzi wa halmashauri nchini kuwa wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo yao.

“Hivyo basi kutokana na hukumu hii ya Mahakama Kuu, sisi vyama vinane ambavyo tumetia saini katika tamko hili, tunaitaka NEC kutumia mamlaka yake iliyopewa na Katiba ya Jamhuri ya Muungano Ibara ya 74 (15) (e) na kuteua wasimamizi wa uchaguzi huu nje na si wakurugenzi wa halmashauri.

“Kama NEC itaendelea na msimamo wake wa kuidharau mahakama na kudharau amri halali, sisi vyama nane tutachukua hatua mbalimbali ikiwemo kutoshiriki uchaguzi,’’ alisema Rungwe.

Aliongeza kuwa pia wamekubaliana kufanyika kwa mashauriano ya kina na wanaharakati waliofungua kesi, wakiongozwa na Chacha Wangwe, kuwapa ushirikiano wa kina ili waweze kuwasilisha shauri hilo Mahakama Kuu kukazia hukumu ya mahakama na kuitaka kuichukulia hatua tume hiyo.

Tamko hilo lilitiwa saini na vyama hivyo nane ambavyo ni ACT Wazalendo, CCK, Chadema, DP, NCCR-Mageuzi, NLD, UPDP na Chauma.

NEC YANENA

Kutokana na madai hayo, MTANZANIA ilimtafuta Mkurugenzi wa NEC, Dk. Athumani Kihamia, ambaye alisema kuwa hawajaingilia wala kudharau mahakama bali wametumia utaratibu mwengine ambao hautaathiri uchaguzi.

“Sisi NEC tupo sahihi, hatujadharau mahakama na wala hatutadharau amri ya mahakama yoyote itakayotolewa kwa maana kwa mujibu wa kifungu cha 7(1) na 7 (3) vya sheria ya sura ya 343 hatujagusa wala hatujaathiri uchaguzi, utafanyika kwa utaratibu mwengine mpaka rufaa itakapoisha,’’ alisema Dk. Kihamia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles