Na EDITHA KARLOÂ -KIGOMAÂ
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameanza ziara ya siku moja mkoani Kigoma kwa ajili ya kugawa miche ya michikichi kwa makundi mbalimbali ya wakulima ikiwa ishara ya kuanza rasmi utekelezaji wa mkakati wa Serikali kuelekea kujitegemea kwa mafuta ya kula yatakayokuwa yakizalishwa kupitia zao la michikichi.
Mkuu wa Mkoa Kigoma, Emanuel Maganga akizungumza na waandishi wa habari Kigoma alisema mpango wa ugawaji wa miche hiyo utafanyika katika Gereza la Kwitanga Halmashauri ya wilaya Kigoma na kambi ya JKT Burombola kikosi cha 821 wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma.
Akizungumzia nafasi ya mkoa katika kusimamia utekelezaji wa mpango huo
Mkuu wa mkoa Kigoma, Emanuel Maganga alisema wataalam na watendaji wa mkoa huo wakishirikiana na taasisi mbalimbali wamejipanga kufanya uhamasishaji kwa wananchi, kutoa maelekezo na kufanya tathmini juu ya mpango huo na kwamba tayari wananchi wameonyesha ari kubwa ya
kushiriki kwenye utekelezaji huo.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Gerlad Kusaya alisema tayari miche milioni 1.8 ipo tayari kwa ajili ya kupandwa
mashambani ikiwa ni sehemu ya mpango wa uzalishaji na usambazaji kwa wakulima.
Alisema miche milioni tano itapandwa kwenye mashamba ya
wakulima ili kufikia lengo la Tanzania kulima zao la michikichi kwa
wingi kwa ajili ya kujitegemea katika uzalishaji wa mafuta ya mawese na kuondoa hali ya sasa ya kutumia shilingi bilioni 445 kuagiza mafuta hayo nje ya nchi.
Alisema katika mpango wa muda mrefu wa serikali kupitia wizara hiyo wanatarajia kuzalisha miche milioni 15 kwa mwaka na kuisambaza kwenye mashamba ya wakulima na kuwezesha Tanzania kufikia
lengo la kuzalisha tani 570,000 kwa mwaka ambazo zitatimiza ndoto ya nchi kuacha kuagiza mafuta hayo nje ya nchi.
Hii ni ziara ya nne ya Waziri Mkuu, Majaliwa kutembelea Mkoa Kigoma kwa ajili ya kukagua, kuhamasisha na kuona hatua zinazofikiwa katika utekelezaji wa mpango wa Serikali wa kuuchagua
Mkoa Kigoma kama mkoa kiongozi katika kilimo cha zao la michikichi na uzalishaji wa mafuta ya mawese.