31.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Siku 28 kuamua hatma wanafunzi kidato cha sita

 RAMADHAN HASSAN– DODOMA

BAADA ya wanafunzi wa kidato cha sita kukaa nyumbani kwa miezi miwili na siku 14 tangu Machi 17, sasa watakuwa na siku 28 za kukaa pamoja na kujiandaa kabla ya kuanza mitihani ya kumaliza elimu ya sekondari Juni 29.

Rais Dk. John Magufuli juzi alitangaza kuwa wanafunzi wa vyuo vyote nchini na wale wa kidato cha sita, watarudi darasani Juni mosi.

Machi 17, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alitangaza kufungwa kwa shule na vyuo ikiwa ni siku chache baada ya mgonjwa wa kwanza wa corona kubainika nchini.

Juzi Rais Magufuli mara baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali Ikulu Dodoma, alitangaza kufungua vyuo na kidato cha sita na kusema hali ikionekana kuwa sawa, hatua nyingine za kufungua shule na shughuli nyingine zitaendelea.

Rais Magufuli alizitaka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na ile ya Fedha na Mipango kuhakikisha zinafanya maandalizi ili pale vyuo vitakapofunguliwa kusiwe na kero kwa wanafunzi.

“Sasa kutokana na hii hali kwamba inaenda vizuri na waziri amezungumza hapa, tumeamua vyuo vyote vifunguliwe Juni mosi, mwaka huu.

“Kwa hiyo, niwaombe wizara zinazohusika, hasa ile ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na ile ya Fedha na Mipango ambayo inahusika sana katika kutoa mikopo kwa ajili ya wanafunzi, leo (juzi) tuna siku tisa, hivyo zijiandae ili hivi vyuo vitakapofunguliwa pasije tena pakawa na kero nyingine, ili kama mwanafunzi anastahili kupata mkopo wake uwe umeshaandaliwa mapema.

“Sababu kwa wizara ambayo iko makini haiwezi ikashindwa kumaliza haya na kufanya maandalizi, na ndiyo maana nimetangaza mapema kwamba walau siku tisa hizi zitatusaidia kujipanga vizuri,” alisema Rais Magufuli.

Aidha, mbali na wanafunzi hao wa elimu ya juu, Rais Magufuli pia alitangaza kuanza masomo kwa wanafunzi wa kidato cha sita ili kutokuathiri ratiba ya kujiunga na chuo kikuu.

“Lakini mbali ya vyuo hivyo, vijana waliokuwa kidato cha sita nao watarudi kwenye shule zao Juni mosi, mwaka huu na Wizara ya Elimu ipange mikakati yao ili vijana hawa wafanye mtihani wao wa kidato cha sita bila kuharibu utaratibu wao wa kuingia chuo kikuu kama ilivyokuwa imepangwa, ugonjwa wa corona usiwacheleweshe vijana hawa.

“Kwa zile shule zingine za sekondari na za msingi tujipe muda kidogo, tuangalie awamu hii ya vyuo kwa sababu wanachuo ni watu wanaojitambua, ni watu wazima tofauti na mtoto mdogo wa darasa la kwanza, tujipe muda tutaona hali inavyoenda na wao baadaye tutawapa nafasi kadiri tutakavyokuwa tunaendelea kupambana na ugonjwa huu wa corona,” alisema Rais Magufuli.

MITIHANI JUNI 29

Jana Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alisema mitihani ya kidato cha sita mwaka 2020 itaanza Juni 29 hadi Julai 16.

Awali kabla ya kuibuka kwa corona, mitihani hiyo ilikuwa ifanyike kuanzia Mei 4 mwaka huu, lakini ikasitishwa baada ya Serikali kutangaza kuzifunga shule zote za msingi na sekondari ili kuepusha kuenea kwa virusi vya corona

Hatua hiyo ya kuzifunga shule hizo, ilitokana na kuripotiwa kwa mgonjwa wa kwanza wa corona Machi 16, mwaka huu jijini Arusha.

Jana Profesa Ndalichako alisema shule zinapaswa kuanza maandalizi mapema ili kuanzia Mei 30, wanafunzi wanaosoma bweni waanze kuripoti na Juni mosi masomo yaanze rasmi.

Alisema shule za kutwa nazo zianze maandalizi mapema kama ambavyo Rais Magufuli ameelekeza.

“Nisisitize kwamba shule ambazo zinafunguliwa ni za kidato cha sita tu,” alisema Profesa Ndalichako.

KUHUSU KIDATO CHA SITA

Profesa Ndalichako alisema mtihani rasmi utaanza Juni 29 hadi Julai 16, huku akilitaka Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kusambaza ratiba ya mitihani hiyo.

“Baada ya kufunguliwa, wanafunzi watajisomea hadi tarehe 28 Juni, 2020 na mitihani itaanza rasmi tarehe 29 Juni hadi 16 Julai, 2020 na mitihani hii itakwenda sambamba na mitihani ya walimu.

“Natoa wito kwa Baraza la Mitihani kusambaza ratiba ya mitihani hii na ihakikishe matokeo yake yatoke kabla ya tarehe 31 Agosti ili kutokuathiri mihula ya vyuo vikuu,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema baada ya kutoka kwa matokeo, wanafunzi watapata fursa ya kufanya maombi katika vyuo mbalimbali wanavyovipenda.

KUFIDIA MASOMO YA VYUO

Katika hatua nyingine, Profesa Ndalichako aliviagiza vyuo na mamlaka za vyuo vikuu kwa maana ya mabaraza na seneti kufanya maandalizi ili kuhakikisha masomo yanaendeshwa kwa kufidia muda ambao vyuo vilikuwa vimefungwa.

“Ni lazima ratiba zibadilike ili kuwe na muda wa zaidi wa kusoma ili kufidia,” alisema Profesa Ndalichako.

Pia alisema mabaraza na seneti za vyuo zinapaswa kuweka utaratibu huo na ziwasilishe mabadiliko hayo kwa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte) ifikapo Juni 27 ili kufahamu wamepanga na Bodi ya Mikopo ifahamu ratiba ya kila chuo.

“Tunasisitiza kwamba hakutakuwa na muda wa ziada, ratiba zao ziweze kufidia ili kutokuathiri mzunguko wa masomo mwaka ujao,” alisema Profesa Ndalichako.

MIKOPO

Profesa Ndalichako alisema Serikali inazo Sh bilioni 122.8 kwa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu.

“Kama alivyosema Rais Magufuli, wajiandae. Ningependa kuwahakikishia Watanzania kwamba fedha kwa ajili ya kulipa tunazo Sh bilioni 122.8,” alisema Profesa Ndalichako. 

Alisema ifikapo Mei 28, vyuo vyote viwe vimewasilisha nyaraka muhimu Bodi ya Mikopo ili kufikia Mei 30, fedha ziwe zimetolewa.

“Mara nyingi ucheleweshaji umekuwa ukitokea vyuo, wanafunzi wamekaa nyumbani muda mrefu na sitarajii kuona usumbufu ukitokea, vyuo vijipange, ikiwemo kuweka maofisa wa kutosha vyuoni,” alisema Profesa Ndalichako.

KUHUSU CORONA

Profesa Ndalichako aliwataka viongozi wa vyuo na shule kuhakikisha wanaweka mazingira salama ya kujikinga na corona, ikiwamo maeneo ya kunawa mikono kwa maji tiririka.

Alisema pamoja na maelekezo hayo, Serikali pia inaandaa mwongozo, ambapo amefanya mazungumzo na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ambaye ameshamwagiza Mganga Mkuu wa Serikali kuandaa mwongozo mahususi kwa vyuo na shule.

Alitoa wito kwa viongozi wote kuanzia mabaraza na bodi za shule kuhakikisha wanasimamia kikamilifu tahadhari ambazo zinatolewa na mamlaka zinazohusika.

“Wizara tutafanya ziara kuangalia vyuo na shule zilivyojipanga kupokea wanafunzi hao ifikapo Juni mosi mwaka huu,” alisema Profesa Ndalichako.

MADARASA MENGINE

Kuhusu madarasa mengine, Profesa Ndalichako alisema: “Utaratibu wao utaelekezwa baadaye, hivyo asije akatokeza mwanafunzi mwingine wa kidato cha kwanza au cha pili na vingine ambavyo havijaelekezwa kurejea shuleni.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles