Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amefanya ziara katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam, huku akiahidi kuwa Serikali itawapa nguvu kuhakikisha wanazalisha bidhaa bora za kibiashara.
Prof. Mkenda alifanya ziara hiyo jana Januari 28, 2022 ikiwa ni muendelezo wa kutembelea Taasisi za Elimu nchini ili kupata uzoefu na kuona shughuli zinazoendelea.
Amesema vyuo vya ufundi kama DIT ni muhimu katika maendeleo ya kiuchumi kwa sababu vinazalisha ajira kwa vijana, pamoja na kuimarisha uwezo wa teknolojia nchini.
Prof. Mkenda ameeleza kuwa kutokana na kile alichokiona, ikiwamo uvumbuzi wa vitu mbalimbali vilivyofanywa na wanafunzi, atakaa na uongozi kuona jinsi ya kuwasaidia kujiendeleza.
Amesema kuwa wana mpango wa kufanya mkutano na Watanzania wabobezi wanaofundisha vyuo vikuu vya nje ya nchi ili kuona jinsi ya kuwawezesha na kuwasaidia wahitimu hapa nchini kujiendeleza.
“Nilichopenda hapa DIT, tayari wana kampuni tanzu ambayo kazi yake sasa ni ubunifu na uvumbuzi. Ubunifu unaofanyika hapa unaweza kufanyika kibiashara wakaanza kuzalisha kwa bidii zaidi.
“Tunachohitaji ni sisi kuwapa nguvu kuzalisha, tunataka bidhaa aina ya vipuri, tuna magari mengi ambayo tunanunua vipuri kutoka nje, lakini kampuni kama hii inaweza kuanza kuzalisha,”amesema Prof. Mkenda.
Aidha ameupongeza uongozi wa chuo hicho baada ya kushudia vitu mbalimbali vilivyopuniwa na wanafuzi hao ikiwamo kiti maalum cha kumuwezesha mtu mwenye ulemavu kufanya shughuli zake kwa urahisi na kusimama ambacho kimebuniwa na Joan Mohammed.
Pia mwanafunzi aliyemaliza Diploma mwaka jana,
Emmanuel Alexander ambaye amevumbua mfumo wa kumuwezesha daktari kumfuatilia mgonjwa aliyepo wodini na kujua maendeleo yake kiafya bila kumfuata kitandani.
Akielezea jinsi alivyofanikiwa kubuni kiti hicho cha walemavu, mbele ya Waziri huyo, Joan amesema huo ni mwanzo tu kwani anatarajia kuvifanya viwe katika ubora zaidi kwa awamu tofauti.